Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Silafu Jumbe Maufi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi nami kuzungumza na Bunge lako Tukufu. Awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipatia afya ya kuweza kusimama leo hii katika kuzungumzia suala zima la Wizara ya Mambo ya Ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa, napenda kutoa pongezi za dhati kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jinsi alivyojitokeza mbele kabisa kuhakikisha ya kwamba anaboresha na kuweka maisha bora kwa askari wetu Polisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jamani mnyonge mnyongeni na haki yake mpeni. Wizara ya Mambo ya Ndani inafanya kazi kwa hali ngumu sana, lakini inafanya kazi kwa weledi na kuthibitishia Watanzania kuwa katika amani na utulivu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hao Wanajeshi, Polisi, Zimamoto, Uhamiaji na Magereza, wote hawa wako karibu na wananchi wa kawaida na wanashirikiana na wananchi wa kawaida. Kwa hiyo, Mambo ya Ndani ni msingi wa amani na utulivu wa nchi yetu. Bila hawa, hii amani tunayojivunia hivi sasa tusingejivunia hata kidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba kusema kwamba Waheshimiwa Wabunge wenzangu, tusione kigugumizi na wala tusione aibu, ni lazima tuseme kwa ukweli kabisa kwamba Wizara ya Mambo ya Ndani inafanya kazi yake vizuri na kwa weledi, iliyobakia kwetu sisi ni kuwaunga mkono ili bajeti yao hiyo wanayoipata na hiyo walioyoiunda iweze kuongezeka na waweze kufanya kazi yao vizuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuzungumzia suala zima la bajeti. Bajeti ya 2017/2018 tuliweza kutenga, lakini Wizara ya Fedha imetoa kwa asilimia 28 tu kwa miradi ya maendeleo. Naomba Wizara ya Fedha, hii asilimia 28 ni ndogo sana, naomba wajitahidi kwa Jeshi la Polisi ama kwa Wizara ya Mambo ya Ndani waweze kupata bajeti yao kamilifu. Hawa watu wanafanya kazi kubwa sana. Bila usalama na amani hata hayo mengine tusingeweza kuyafanya. Mengi wameyasema wenzangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba Wizara ya Fedha, Wizara ya Mambo ya Ndani ipatiwe kwa asilimia mia moja bajeti yao wanayoipanga na kwanza hata hii bajeti tuliyoiweka haikidhi mahitaji ya Wizara ya Mambo ya Ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuzungumzia suala la makazi. Napenda ku-declare interest kwamba mimi ni Mjumbe katika Kamati hii ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama. Tumetembelea Mikoa ya Lindi na Mtwara; nyumba za Wanajeshi wetu kwa kweli siyo nzuri, haziridhishi, ni kwa nchi nzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali itoe maamuzi magumu, kama ilivyotolewa maamuzi kwa Uhamiaji hapa Dodoma kuhusu kununua nyumba pale Iyumbu, basi tunaomba na Wizara ya Mambo ya Ndani wachukue jukumu la kununua nyumba kwa Askari wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna nyumba zilizojengwa na National Housing ambazo wanasema kwa bei nafuu, lakini siyo bei nafuu na wananchi wameshindwa kuzinunua. Naomba hizo nyumba zinunuliwe na Serikali kwa Wanajeshi wetu ambao hawana nyumba za kukaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, naomba zitolewe ramani maalum za kujenga nyumba za Wanajeshi yetu kwa sababu nyumba zile walizonazo siyo za kuishi binadamu ni nyumba za kuishi mifugo. Tunaomba nyumba za kuishi binadamu zitolewe kwa kila mkoa na kila mkoa upewe idadi maalum kwa kila mwaka wajenge nyumba ngapi; ili tuweze kutathmini baada ya hii miaka miwili na nusu ni mkoa upi utapata ushindani wa kujenga nyumba za kutosha za Wanajeshi wetu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ninalopenda kulizungumzia ni kuhusu kupandisha madaraja Askari. Kwa kweli inachukua muda mrefu sana kupandishwa madaraja Askari hawa na wale wanopandishwa madaraja inachukua muda kuwapatia fedha zao stahiki kwa daraja walilopandiswa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, kuna Askari ambao wanastaafu. Mtu anapostaafu kwa mujibu wa Jeshi wanapewa likizo ya kustaafu. Likizo ya kustaafu ni miezi minne. Kipindi hiki cha miezi minne kinatosha kabisa kumwandalia mafao yake ili akimaliza tu likizo yake, anapoanza kustaafu, fedha yake inapatikana; lakini tangu mwaka jana, Askari wamestaafu mpaka hivi leo wanatimiza sasa ni mwaka hawajapata mafao yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Jeshi liweze kuwapatia fedha yao. Hii ni kutokana na kwamba kile kifungu cha matumizi ya kawaida na matumizi mengineyo hakifiki kwa wakati kwa Wizara ya Mambo ya Ndani na kinafika kikiwa hakikidhi mahitaji kwa wenyewe katika kutekeleza mahitaji hayo yote. Kwa hiyo, nawaomba Wizara ya Fedha, wawape fungu hili katika ukamilifu wake ili waweze kulipa madeni ya hao Maaskari wanaolalamika; wengine wana hali duni na wanaweza wakapoteza maisha kabla hawajapata stahiki zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Wizara iweze kuhakikisha kwamba fungu hili kwa Majeshi yote; Zimamoto, Uhamiaji, Magereza na Polisi wapelekewe katika ukamilifu ili waweze kuondoa matatizo ya Wanajeshi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni kuhusu suala la kiwanda. Tunacho kiwanda Morogoro kinachotengeneza sare za Polisi na wafungwa. Tunaomba viwanda hivi viweze kuongezwa au viwezeshwe na Serikali ili viweze kuzalisha kiasi cha kutosheleza wananchi na Wanajeshi wetu katika nchi yetu. Tunawajua idadi yao. Wanajeshi hawa wakipata angalu pair mbili zinaweza zikawasaidia. Vile vile kiwanda cha viatu kiongezwe ili kiweze kutoa viatu kwa Wanajeshi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekwenda Lindi na Mtwara, tumekuta baadhi ya Askari viatu vyao kwa kweli tulisikitika sana. Tulisikitika mno! Kwa hiyo, tunaomba hiki kiwanda kinachotaka kujengwa hivi sasa kitakachoweza kuzalisha jozi 4,000, naomba kianzishwe mara moja ili Wanajeshi wetu waweze kupata vifaa vya kutumia katika nchi yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, nashukuru na kutoa pongezi sana kwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi nzuri anayoifanya. Ila naomba kwa Serikali yangu sikivu, suala la mazingira yetu Mkoa wa Rukwa, Bonde la Rukwa, Bonde la Tanganyika, kwa kweli hali siyo nzuri kimiundombinu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo, tunahitajika tupate Vituo vya Polisi. Vituo vya Polisi vipo lakini havina amari. Kwa hiyo, wako Askari wanalinda bila kuwa na silaha, lakini wananchi wao wa kule wanazo silaha na ndiyo maana mauaji katika Bonde la Rukwa yanaendelea. Kwa sababu hakuna amari katika vituo vyetu, inaweza kuleta matatizo, Polisi wetu wanashindwa kufanya kazi iliyokuwa katika ukamilifu wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Wizara ya Mambo ya Ndani ione umuhimu wa kuweka amari katika hivi Vituo vyetu vya Polisi vilivyokuwa kule Bonde la Rukwa. Vinginevyo, nadhani zile silaha zao wanaweka mahali pasipokuwa salama na kwa maana hiyo inahatarisha vile vile katika suala zima la ulinzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine naomba Wizara yetu ya Mambo ya Ndani iweze kupewa fedha kamilifu katika mwaka huu wa 2018/2019 ili iweze kutimiza majukumu yake katika ukamilifu wake. Kutokana na kazi ngumu wanayoifanya Polisi wetu, ndiyo maana maneno mengi yanazungumzwa. Daima mti ukiwa na matunda hupopolewa na mawe, mti usiokuwa na matunda mazuri hakuna mtoto hata mmoja atakayeupopoa mawe. Kwa hiyo, maneno mengi haya tunayozungumza Waheshimiwa Wabunge wote humu ndani ni dhahiri kusema kwamba Wizara ya Mambo ya Ndani inafanya kazi yake vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba ndugu zangu wa Zimamoto waweze kuongezewa vituo na vile vile waweze kupewa magari angalau nusu ya vituo viwepo na nusu ya magari ya vituo hivyo yaweze kupatikana, kwa sababu wananchi wetu wanaendelea kujenga majumba na hatimaye kufikisha miji yetu kuwa scattered, inakosekana miundombinu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, likitokea la kutokea, Zimamoto hawawezi kuingia kwa urahisi mle ndani. Kwa hiyo, tunachokiomba ni kwamba, hawa watu wa Zimamoto wapewe vituo vya kutosha angalau nusu ipatikane na hali kadhalika magari yaweze kupatikana ili waweze kutusaidia vizuri ndugu zetu hawa wa Zimamoto. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine la mwisho ni kuhusu watu wa Uhamiaji. Watu wa Uhamiaji kwa kweli katika nchi yetu hii ya nchi nane zinazotuangalia wanahitaji kupewa nguvu ya ziada na nguvu ya ziada ni kuhusu na magari yao na nyumba zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ninachokiomba ni kwamba hawa watu wana doria, Polisi wana doria, Magereza wana doria, Zimamoto wana doria na Uhamiaji wana doria. Vile vile wana suala la kufuatilia makosa mbalimbali katika kufanya msako wa kuangalia Wahamiaji, wahalifu na kadhalika. Sasa watu hawa wana dharura mbalimbali, lakini hawana magari na wala hawana mafungu ya mafuta ya kukamilisha shughuli zao hizo na ni shughuli muhimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Wizara ya Mambo ya Ndani waone umuhimu kwamba sasa umefika wakati wa kuhakikisha watu hawa wanapata magari ya kutosha, mafungu ya mafuta ya kutosha. Vile vile wanafanya kazi na baada ya saa za kazi, pamoja na kwamba ni saa 24, lakini hawa ni binadamu, tujaribu kuweka na motisha kwa watu hawa wakati wa kufanya kazi zao ili waweze kufanya kazi kwa ufanisi zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo hivyo pia naomba ndugu zangu Serikali, najua kila Wizara huwa inapewa ukomo wa bajeti, lakini kwa majeshi yetu tunaomba ukomo uangaliwe kwa Serikali. Ukomo ni mdogo na kazi wanayoifanya ni kubwa zaidi. Kwa hiyo, naomba ukomo wa miradi ya maendeleo, ukomo wa shughuli za kawaida uangaliwe upya na kuwaongeza nguvu ili waweze kufanya kazi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa naomba kuunga mkono hoja na nawapongeza sana Makamishna wote, Waziri na Naibu wake na wataalam wote wa Wizara ya Mambo ya Ndani, aluta continua, big up!