Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Rukia Ahmed Kassim

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. RUKIA AHMED KASSIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kuweza kunipa nafasi jioni hii ya leo nami niweze kuchangia katika Wizara hii ya Mambo ya Ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza na Jeshi la Polisi. Wakati mwingine Jeshi la Polisi wanakwenda tofauti na dhana ambayo tumeizoea. Jeshi la Polisi tunasema kama ni wanaolinda usalama wa raia na mali zao, lakini inakuwa ni tofauti kabisa na mambo wanayoyafanya, kwa sababu kuna baadhi ya Vituo vya Polisi unapokwenda, kauli wanazozitumia mtu anapokwenda pale ana tatizo, siyo nzuri. Kwa hiyo, tunaomba wajirekebishe. Hili nalisema nikiwa na ushahidi kamili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kituo kimoja cha Polisi Zanzibar, Kituo cha Mazizini. Mheshimiwa Waziri ananisikia na namwomba hili jambo alifanyie kazi. Hili lilinitokea hata mimi mwenyewe binafsi nilikwenda pale. Ilikuwa ni kesi ndogo tu ya traffic, lakini nilipokwenda, huyo niliyemkuta, aliniuliza: “Mama wewe unahoji neno hili;” kwanza kauli aliyoitumia mimi kama mtu mzima siwezi kuitaja hapa. Kwa sababu mtu
mzima unapotukanwa, unapovuliwa nguo unatakiwa uchuchumae siyo unyanyuke. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maneno aliyoyatumia kwa kweli ni kumkashifu mtu au kuwakashifu baadhi ya watu na pia ingeleta uchochezi ndani ya nchi. Kwa sababu mimi ni mtu mzima, sikutaka maneno yale niyarudie wala niyaseme hapa. Finally, aliniambia “wewe mama unataka nikuheshimu au nikuvunjie heshima?” nikamwambia nitafurahi sana kama ukinivunjia heshima, lakini bahati nzuri sana nafikiri baada ya kujiamini kumwambia vile aliogopa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema sitaki niwataje wala sitaki niongeze la ziada hapo, ila hiki Kituo cha Polisi kimekaa kama ni kijiwe labda cha wacheza Keram au wavutaji wa bangi. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri akifutalie sana kituo hiki. Hata baadhi ya majina ya hao Polisi waliopo pale, ni ya ajabu ajabu na yanaashiria shari kwa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nasema kama Jeshi la Polisi ni usalama wa raia na mali zao, lakini wakati inapotokea operation, kwa nini Jeshi la Polisi linatumia nguvu kubwa? Ni sawa na kumuua labda inzi kwa kutumia bunduki jambo ambalo siyo sahihi. Inapotokea operation watumie nguvu za kiasi ili wananchi wetu wajenge imani na Jeshi letu la Polisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna baadhi ya vituo anakamatwa mtu pengine kwa shinikizo tu la mtu fulani, anawekwa lockup zaidi ya siku saba, wakati Sheria inaeleza wazi kwamba mtu anaweza kukaa lockup kwa muda wa masaa 48. Kwa hiyo, naiomba Serikali waliangalie hili ili haki itendeke katika vituo vyetu vya Polisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hapo, nataka nijielekeze kwenye Jeshi la Zimamoto. Katika Wilaya zetu, hakuna Ofisi wala vituo vya Zimamoto, viko katika Mikoa. Unapotokea moto katika Wilaya zetu inakuwa ni shida na kwa kweli inakuwa ni janga kubwa sana. Hata hapo inapopatikana hiyo gari, pengine itafika katika eneo la tukio lakini hawana maji. Kwa hiyo, naishauri Serikali katika Wilaya zetu waweke vituo na Ofisi za Zimamoto. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kutoka hapo, nitajielekeza sasa kwenye vitambulisho vya NIDA. Bunge limepitisha pesa nyingi sana kupeleka katika zoezi hili, lakini utendaji kazi wa NIDA unasuasua. Inachukua muda mrefu kupatikana kwa vitambulisho. Kwa hiyo, naishauri Serikali iangalie sana jambo hili ili ituambie hasa, Mheshimiwa Waziri atakapokuja atueleze, baada ya muda gani watu watakuwa wamepata vitambulisho? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kutoka hapo, nataka nijielekeze katika Jeshi la Polisi vilevile. Askari wetu wanaishi katika mazingira magumu sana. Ni ushahidi, hata hapa Dodoma tunawaona wanaishi katika nyumba za mabati, nyumba zimeezekwa kwa mabati na pia hazikukandikwa, zina mabati, joto tupu. Jamani hawa ni binadamu kama sisi, wanastahili na wao wakae sehemu nzuri. Wanapopata utulivu wa mwili na akili ndiyo wataweza kufanya kazi vizuri. Leo wanaishi mle kama wanyama, ni kuwadhalilisha na kulidhalilisha jeshi letu. Kwa hiyo, naishauri Serikali tuanze na hapa Dodoma kwanza kuwarekebishia makazi yao Askari wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wakuu wa Vituo tunawapa mizigo mikubwa. Hakuna mgao wa fedha kwa ajili ya umeme wala maji. Unapomalizika pengine umeme katika kituo, Mkuu wa kitengo kile cha mahabusu, kunakuwa pengine ndani kuna mahabusu chungu nzima, hawawezi kuwacha wale na giza, wanaweza wakadhuriana, kunaweza kukatokea neno lolote. Mkuu wa Kituo anajilazimisha kutoa hela yake mfukoni, mshahara wenyewe tunaujua haukidhi haja, ana watoto, ana familia; jamani wenzetu tuwaoneeni huruma na Serikali ihakikishe kila Kituo cha Polisi kinaweka fungu la fedha kwa ajili ya maji na umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.