Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Ali Hassan Omar King

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Jang'ombe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. ALI HASSAN OMAR KING: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa hii. Mimi la kwanza kabla sijamshukuru Mungu niseme Subhanallah min-dhalika.

Mwenyezi Mungu ametakasika na yote ambayo yamesemwa na mtu ambaye hajielewi, ametakasika. Mungu hakosolewi kwenye imani yoyote ile. Sasa waone Watanzania jinsi gani kwamba mtu kama huyu ndio awe wanamwamini kwamba kumfuata maneno yake ikiwa kwamba kauli zake ndiyo hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa hii nafasi. Pili, namshukuru Mwenyezi Mungu na naomba Mwenyezi Mungu aniongoze, anitoe kile kitanzi wanachotiwa wenzetu wanapojikakamua sauti kali na halafu haitoki, kile kitanzi Mungu mimi aniondoshee nizungumze hivi taratibu ili message yangu ifike vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wengi wanazungumza matukio lakini wanashindwa kusema sababu. Wanataja kulaumu lakini wanashindwa kutaja sababu zilizowapelekea au zilizowafikisha watu pale wao wanapolaumu. Wanalilaumu Jeshi la Polisi lakini wanasahau kwamba kuna mambo yalifanyika Kibiti wakidhibitiwa, mambo yalifanyika Tanga wakidhibitiwa, mambo yanayohamasisha maandamano, mambo ya watu wanaozungumza tofauti, ni sawasawa na kusema kwamba lawama sasa zinahama kwa mjambaji zinakwenda kwa mtema mate. Hivi ndivyo walivyo wenzetu, lawama zinahama kwa mjambaji sasa zinaenda kwa mtema mate, kwa sababu wahamasishaji wa ubaya ni wao. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mimi niongee ya kwangu kwa Jeshi la Polisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa masikitiko makubwa sana kusikitikia Wizara hii ya Mambo ya Ndani na huzuni kubwa sana, mwaka wa tatu huu haya ninayoyasema leo nayasema tena. Hakuna hata moja ambalo limefanyika kwangu na mimi sasa nazungumza masikitiko yangu Jeshi la Polisi kwangu mimi natokea Jimbo la Jang’ombe, kuna Ziwani Polisi, Jeshi la Polisi kwangu ni sawasawa na double edged sword, upanga wenye ncha mbili. Ncha ya kwanza ni sehemu ambayo tunapata ulinzi na usalama kwa Tanzania nzima na hiyo tunanufaika katika Jimbo letu, lakini ncha ya pili kwa Jeshi la Polisi kwangu mimi ni wapiga kura wangu Mkoa mzima wa Mjini Magharibi Unguja askari wake wanakaa Ziwani Polisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimefanya ziara tarehe 7 Januari, 2018 kwenda Ziwani Polisi nikakuta pale kuna zile nyumba ambazo za single wanakaa mtu mmoja mmoja kutokana na ukosefu wa nyumba, zile nyumba zinakaa familia, zile nyumba zipo 15 kila nyumba moja ina familia nane kuna familia 120, kule kwetu sisi mashallah watu wanazaa. Tukimpa kila mmoja watoto wanne wanakaa watu wanne ndani basi watu 480 wanakaa, lakini wanatumia choo kimoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hili nimeshalisema na lilianza kusemwa na Mbunge aliyepita mwaka 2011 halijafanyiwa kazi. Pale kuna choo kimoja kiliwahi kujengwa na Mheshimiwa Nyanga aliyekuwa Mwakilishi wa Jimbo la Jang’ombe. Nampa tena Mheshimiwa Waziri hii taarifa tena, je, likitokea la kutokea choo kimoja watu 480 wanatumia vipi askari hawa. Masafa ya kufuata choo ni mita 100 mpaka mita 200; kila mmoja anatoka na kopo la maji na ndoo, ukitokea ubakaji pale tutasemaje? Yakitokea maradhi ya mlipuko katika choo kile kimoja tunafanya nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri hili naomba nitekelezewe na nimepeleka kwa DCP Malika, Kamishna wa Ujenzi wa Polisi Makao Makuu nimepeleka mwenyewe kwa mkono. Tunahitaji milioni 50 kujenga vyoo pale vya askari, kama kuna dharura basi tuje tusubiri dharura ya kupata maradhi watu wakafa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, nyumba ya Kilimanjaro Ziwani Polisi, hii nyumba imejengwa tokea kwenye miaka hiyo ya 1980, hii nyumba inatakiwa kukarabatiwa, nyumba inakaa 12, tukimpa kila mmoja watoto wanne, nyumba inavuja na inakaribia kuanguka. Hivi leo ndio tunataka mpaka nyumba ianguke askari wafe tulete mfuko wa maafa. Tunahitaji milioni 68 kukarabati kuweka paa ili kudhibiti vitu ambavyo vinatokea pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi mvua za juzi, familia mbili zinazokaa juu kwenye jengo la Kilimanjaro Ziwani Polisi zimehama kwa sababu jengo linavuja, je, tunasubiri lianguke? Kama hiki sio kipaumbele, kipaumbele ni kuzika askari wetu? Kipaumbele ni kwenda kuzika familia askari wetu kama hiki sio kipaumbele. Kwa hiyo, nazungumza leo kwa uchungu kabisa katika Jeshi la Polisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeangalia katika Vote 28 subvote 2005 ya Zanzibar nimeona kuna fedha pale za maintenance and repair of building kwamba imewekwa ni milioni 22. Fedha hizi haziwezi kutosha kwa kufanya hili jambo. Kwa hiyo, naomba Waziri atakapokuja hapa aje anipe maelezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumetajwa katika ukurasa wa tisa wa hotuba ya Waziri miradi ya ujenzi mpya wa nyumba za polisi. Tuliahidiwa tutajengewa nyumba 423 mwaka juzi kukawekwa na bajeti, mwaka jana hakukuwekwa bajeti, mwaka jana kuliwekwa milioni 200 kukarabati kituo cha Mkokotoni, mwaka huu nimeangalia kwenye development hakuna lakini tunaambiwa kuna bilioni 10 ya Mheshimiwa Rais itatokea kwenye bajeti gani, kwanza nataka niambiwe hapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia zitajengwa nyumba 400, tulikuwa tunataka tuambiwe kwa Mjini zitakuja ngapi, kila siku unatajwa ujenzi lakini haziji fedha. Sasa na hili vipi tunataka Mheshimiwa Waziri waje watuambie ukweli wanaposema hapa tunayapeleka majimboni kwetu na mimi naishi na askari kule au hawataki nirudi mwenzao hapa. Hakuna jambo hata moja nililotekelezewa tokea mwaka wa kwanza nakuja hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, Ziwani Polisi kuna hospitali, kwa nini tusiipelekee ambulance kama inavyokuwa kwa majeshi, ikitokea dharura ya kuhamisha mgonjwa pale tunafanya nini? Ziwani Polisi wamejenga kituo cha afya kipo kinaendelea kama hospitali nyingine katika kambi lakini katika kituo hiki cha afya wamejenga maternity pale mradi ule haujaisha. Kwa hiyo, je, hapa tunafanya nini katika kuwa- support kwenye hii? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie jambo ambalo amelizungumzia Mheshimiwa Khatib, kwa mujibu wa Sheria ya Jumuiya (The Society Ordinance) ya mwaka 1954, Wizara ya Mambo ya Ndani ndiyo ambayo inatakiwa kuwa na usimamizi wa jumuiya hizi za kidini. Sasa hapa kifungu kinataka kuteuliwa kwa Msajili wa Jumuiya, msajili huyu hajateuliwa, watu sasa hivi wanafanya hayo mambo chini ya kitengo cha sheria cha polisi, kwa hiyo kifanyike hicho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Wizara inao uwezo wa kupendekeza hilo jina la Msajili likateuliwa lakini pamoja na kuanzisha Ofisi ya Msajili. Kwa hiyo, hili linatakiwa pia nalo lifanyike. Mheshimiwa Waziri amshauri Mheshimiwa Rais amchague Msajili wa mambo haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ninalotaka kuzungumzia ni kuhusu umeme, askari wanalipa wenyewe umeme. Bajeti iliyopita ya mwaka 2016/2017, ilikuwa actual milioni 74 zilizoenda Zanzibar zimeshushwa sasa hivi milioni 24, je, matumizi ya umeme yamepungua? Mwaka jana zimewekwa milioni 24, mwaka huu milioni 24. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri aje aweke sawa katika suala hili, sisi tunapokea malalamiko ya askari polisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja na nashukuru.