Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Goodluck Asaph Mlinga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ulanga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa muda huu mchache ulionipa ngoja nifafanue masuala machache. Kwanza nilipongeze Jeshi la Polisi kwa kazi nzuri wanayoifanya lakini kuna upungufu mchache ambao unasababisha Jeshi la Polisi kupata madoa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ni rushwa. Kwa research ambayo nimeifanya 85% ya wanaopata huduma ya Jeshi la Polisi wanaipata kwa rushwa. Hawawezi kupata huduma hiyo mpaka watoe rushwa. Mfano mlalamikaji akifika kituo cha polisi hawezi kupata huduma yoyote atatengenezewa mazingira mpaka atoe hela ndiyo ahudumiwe, wataambiwa karatasi hakuna, gari halina mafuta au askari wachache.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili mlalamikiwa, huyu ndiyo balaa kabisa. Ukiwa mlalamikiwa yule askari mpelelezi inatakiwa umuheshimu kama baba mkwe wako, atakuita muda wowote, mahali popote anapotaka. Anaweza akakuita baa akakwambia lipia vinywaji, anaweza akakuita wapi akakwambia toa hela hii hapa. (Kicheko/ Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu dhamana. Dhamana haipatikani bila ya kutoa rushwa. Hilo ni suala la kwanza nililotaka kuchangia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ni ubambikiaji wa kesi. Ubambikiwaji wa kesi ni pale Polisi anapo-exaggerate, yaani anapoikuza ile kesi tofauti na ilivyokuwa. Kwa mfano, kesi ya madai inageuka kuwa ya jinai, Polisi anafanya hivyo ili kutengeneza mazingira ya kupata pesa. Pili, kesi ya uzururaji inakuwa ya ukabaji. Tatu kesi ya kuku inakuwa ya ng’ombe. Nne kesi ya matusi inageuka kesi ya kuua kwa maneno. Niwapongeze askari wanawake kwenye hili hawapo. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine traffic. Traffic ni janga lingine la Taifa. Kwa Dar-es-Salaam wanawaita wazee wa Max Malipo na mikoani wanawaita TRA ndogo. Traffic wameacha kazi yao ya kuangalia usalama barabarani sasa hivi wanakusanya mapato na nimethibitisha mmewawekea malengo. Makosa ambayo wanatoza fine ni ya uonevu. Unaenda kumtoza bodaboda Sh.200,000/= fine na ndiyo maana sasa hivi bodaboda zimejaa kwenye vituo vyote vya Polisi. Kwa hiyo, tunaomba waliangalie hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ni makosa ya mitandaoni. Makosa ya mitandaoni saa hizi imekuwa too much. Kwenye mtandao hajulikani kiongozi au mtu wa kawaida, wanatukanwa wananchi, wanatukanwa Wabunge wetu, Mawaziri hadi Rais anatukanwa. Mheshimiwa IGP yupo hapa tumemwekea nyota mabegani hizo ni nguvu, atumie nguvu zake wasimchezee. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, natoa account ambazo kwenye mitandao ya kijamii zinamtukana Rais. Kuna Kwinyala, Malisa GJ, CHADEMA in Blood, Yeriko Nyerere na dada yao Mange Kimambi, wamekuwa wakimtukana Rais. Jamani hakuna nchi ambayo Rais anachezewa, nitolee mfano Kagame, umeshawahi kusikia mtu anamtukana Kagame? Polisi tumieni nguvu zenu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, ni hayo tu.