Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Fakharia Shomar Khamis

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona. Kwanza sina budi kuwasifu Wizara, Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Watendaji wao wote kwa kazi nzuri na hasa Kamishna wangu Bwana Mohamed Hassan ambaye anafanya kazi nzuri na uteuzi wake ameupata hivi karibuni na tunamwona jinsi anavyojitahidi kwa utendaji wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jeshi la Polisi tumelipa majukumu makubwa, majukumu ya kutulinda sisi raia na mali zetu lakini kwa kweli utendaji wao wa kazi na vitendea kazi walivyokuwa navyo siyo rafiki. Kwanza anapokuwa anaenda kazini, baadhi ya sehemu anazofanyia kazi yake siyo nzuri, anaporudi kazini kachoka, sehemu anapoishi au anapokaa sio rafiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, sisi Kamati yetu tulikwenda kutembelea Mtwara, Lindi pamoja na Kilwa, jamani nyumba tumezikuta huwezi kuamini kwamba kweli nyumba hizi wanaweza kukaa binadamu na wakafanya kazi na wakaweza kutulinda na kuwa wako kwenye nafasi ya kufanya kazi kwa weledi ambao tunauona hivi sasa majeshi kwa kazi zake nzuri wanazotufanyia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli utasikitika na utawaona hawa watu wana shida katika utendaji kazi wao lakini wanajitahidi kuweza kutufanyia kazi na kuweza kuturidhisha. Wanapokuwa katika doria wana matatizo ya mafuta, bajeti yake inakuwa ndogo. Wao wenyewe kimafao pia malimbikizo yao wanakuwa hawayapati kwa wakati. Sasa haya yote yanakuwa ni mtihani kwao ina maana lazima Mheshimiwa Waziri awatazame hawa watendaji wetu kwa jicho la ziada ili waendelee kufanya kazi zao nzuri wanazotufanyia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulitembelea majengo ya Uhamiaji yaliyokuwepo Lindi na Mtwara. Majengo hayo kwa kweli yanasikitisha na kama ulifika kule, maana kipindi kile ulikuwa kwenye majukumu mengine hatukuwa na wewe lakini sisi Kamati tumeona na hatukupendezwa nayo na kwa sababu tumekuta kikwazo ni pesa za maendeleo haziendi kwa wakati na badala ya kupata kitu kizuri mtapata hasara.

Maana yake majumba yanavyopata mvua na miti ishaoza ina maana itafika wakati patabakia kiwanja badala ya kumalizia zile nyumba. Mheshimiwa Waziri aliangalie suala hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni ajira za Jeshi la Polisi ambapo tayari hivi sasa zimeshatangazwa na tayari vijana wetu wameshaanza kuomba kwa mujibu wa utaratibu. Kwa upande wa Zanzibar hizi nafasi hatujui zitagawiwa vipi lakini najua utaratibu wanao na wakija hapa watatueleza jinsi wenyewe taratibu zao walivyozipanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunasisitiza vijana walioko JKU Zanzibar tayari ni wakakamavu, wameshakaa chuoni kule, washasomeshwa na baadhi yao elimu zao zinafika degree, vijana hawa wasiwasahau waweze kuwachukua. Wengine wamewekwa kama wakufunzi ili wawepo pale JKU waweze kujitolea pia waweze kuwasaidia waweze kupata kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo nataka kulizungumza ni malipo ya askari wastaafu. Kwa kweli askari wastaafu wanapata shida Zanzibar na shida wanazozipata kwamba kule Zanzibar hakuna ofisi inayoshughulikia mambo ya pensheni, inabidi waende Tanzania Bara. Mtu unapokuwa tayari umeshaastafu hata ile haiba yako kwa wenzio inapungua, sasa wanahangaika kupata pesa kwa wakati hawapati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tungeomba ofisi kama hiyo iwepo na Zanzibar kwa wale wanaomaliza Zanzibar walau waweze kuhangaikiwa palepale na mambo yao yaweze kuwa pale pale. Kwa kipindi hiki wanakuwa hata pesa za kupanda boti kwenda na kurudi hawana tena. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nazungumzia kuhusu Makao Makuu ya Polisi Ziwani, wazee wetu walikuwa wanaita bomani. Mimi nimefunua macho boma lile nimeliona liko vilevile na hadi hivi sasa ni bovu, ukiangalia senyenge iliyozunguka boma ni mbovu, ukiangalia majumba yenyewe ni mabovu ambayo yapo kabla ya 1964 toka ukoloni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Zanzibar pana historia na maboma yale na kuna nyimbo inaimbwa tarehe 12 bomani tuliiingia. Sasa kwa nini hatulipi hadhi yake ya boma hilo tuliloingia ili likaweza kuonekana? Kwa sababu kila anayekuja historia pale anaiona. Ukiingia ndani majengo mabovu, njia za kupitia usafiri wa ndani mbovu, unachokiangalia hata kama mtu anataka kwenda toilet pia atafute vipi apenye aingie ili akajisaidie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ningeomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja atuelezee katika bajeti yake ya maendeleo kwa upande wa Zanzibar na boma lile lililokuwepo Ziwani watalisaidia vipi ili historia iweze kujiendeleza? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine nashauri kwamba hawa wastaafu wetu ambao niliowazungumzia jamani wanateseka, wazidi kuwaangalia. Kama hawatowaangalia baadaye watakuja kujuta waje kuwasifu au wasikie wamefanya vitu vingine havistahili kumbe njaa mtu imemkabili mtu na njaa kwa kweli ni mbaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa haya machache, naunga mkono hoja.