Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

Hon. Cosato David Chumi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafinga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nami nashukuru kwa kupata nafasi na kama mdau wa michezo napenda kuishukuru Wizara na Watendaji wake wote kwa maandalizi ya hii hotuba yao. Pia napenda kushukuru vyombo vya habari vya Serikali, hasa Daily News kwa sababu sasa hivi wamekwenda digital, wanatusaidia kueneza Kiswahili kwa kuchapisha lile jarida lao linalotoka kwa ajili ya nchi za Afrika Mashariki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda kupongeza Idara ya Habari Maelezo kwa wepesi wake wa kutoa taarifa mara kwa mara kwa Umma wa Watanzania. Nawaomba waendelee kwa sababu hii ndiyo idara ambayo inategemewa kutoa matamko na maelezo mbalimbali, kinyume chake kutakuwa na vacuum ambayo inaweza kujazwa na taarifa ambazo zinaweza zikapotosha wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya pongezi hizo, niende kwa haraka sasa katika mchezo unaopendwa na watu wengi duniani, mchezo wa mpira wa miguu. Hapa naipongeza TFF, angalau baada ya mwaka 2017 kuchangia na kutoa takwimu za ushiriki wa Timu ya Taifa katika michezo ile kulingana na kalenda ya FIFA, naona TFF angalau walizingatia ule ushauri na sasa hivi Timu ya Taifa inashiriki kadri ya kalenda ya FIFA katika mechi za majaribio au za kujipima nguvu au za kirafiki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii imesaidia mpaka wiki iliyopita angalau tumepanda kutoka nafasi ya 146 mpaka 137. Hata hivyo, bado kuna kazi inatakiwa ifanyike, tuendelee kukutana na timu ambazo angalau ziko kwenye viwango vya hamsini bora kwenye FIFA ranking maana yake ile inatusaidia sisi kupata angalau points nyingi na hivyo kuisogeza Timu yetu ya Taifa katika viwango bora vya FIFA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, mojawapo ya vitu vilivyotusaidia ni kuwafunga Congo DRC ambao wako nafasi ya 38 katika FIFA World Rankings. Kwa hiyo, tusiandae mechi kucheza tu na ambao niseme ni kama wachovu wenzetu, hapana. Tukabiliane na hao ma-giant kama tulivyofanya kwa Algeria, hata kama tulipoteza. Maana yake ni kwamba tunaendelea kuijengea uwezo Timu yetu ya Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naipongeza Timu ya Ngorongoro, Timu ya Serengeti na Timu za Wanawake. Kimsingi TFF naona inajitahidi kuhakikisha kwamba timu zetu zinashiriki katika michuano ya Kimataifa kadri inavyowezekana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, la pili ambalo linaweza kusaidia Timu yetu ya Taifa iwe na ushindani, ni ligi yetu kuwa na ushindani. Sasa hivi kanuni inasema timu inaweza ikaajiri wachezaji saba wa kigeni, lakini je, ni wachezaji wa kiwango gani? Kwa hiyo, napenda kushauri TFF, mfano Ligi Kuu ya Uingereza ili ucheze, lazima uwe umethibitisha ubora yaani lazima uwe timu yako iko katika viwango.

Kwa mfano, kiwango cha kwanza mpaka nafasi ya kumi mchezaji lazima awe amecheza angalau asilimia thelathini (30) ya mechi za Timu ya Taifa kwa miaka miwili. La, kama unatoka katika timu ambayo kwenye FIFA Ranking iko nafasi ya 21 mpaka 30, lazima mchezaji uwe umecheza angalau asilimia 60 katika timu yako ya Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa sisi inawezekana kuna wachezaji wanatoka nchi za Afrika Magharibi kweli kiasi fulani zimepiga hatua, lakini hata wachezaji wanaotoka kwenye Ukanda wetu wa Afrika Mashariki na Kati hebu basi TFF iweke vigezo, isiwe tu bora mchezaji. Maana yake nimefuatilia kalenda ya FIFA, hakuna wachezaji walioitwa kwenda kuchezea timu zao za Taifa lakini hapa tunawaita ma- professional. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiacha Juuko Murushid, Emmanuel Okwi, ukiacha Dany Usengimana na yule wa Singida United na ukiacha, siku za nyuma, Haruna Niyonzima, hakuna mchezaji yeyote ameitwa kwenye timu yake ya Taifa, lakini sisi hapa tunamlipa fedha nyingi. Kwa hiyo, naiomba TFF i-set standard kwamba ili mchezaji acheze Ligi Kuu hapa nyumbani, lazima kuwe na vigezo fulani, hatuwezi kuwa na vigezo kama vya Spain au vya England au vya Italy, lakini lazima tu-set standard ili hapa isiwe soka ambayo imekuwa kama vile ni soka holela holela tu, kwamba watu wanakuja kujifunzia mpira hapa. Hilo litasaidia kuleta ligi yenye ushindani, lakini kutokana na ligi yenye ushindani maana yake tutakuwa na timu ya Taifa ambayo ni bora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe mfano, Uingereza sasa hivi kuelekea Kombe la Dunia 2022 wameamua kuongeza kwamba kila timu lazima iwe na wachezaji wa ndani kutoka nane mpaka 12. Sisi tunasema wachezaji wa kigeni wawe saba; ni vizuri, hatuwezi kuiga kila kitu kutoka kwa wenzetu waliopiga hatua sana, lakini angalau tu-set hizo standards. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, Kamati imezungumzia hapa kuhusu Timu ya Taifa kwamba maandalizi yanakuwa ni duni; naiomba Serikali, pamoja na kwamba mambo haya yanasimamiwa na TFF, lakini hakuna namna. Kama tunataka kufanya kweli michezo ni biashara, tutangaze utalii kama Mheshimiwa Waziri alivyosema, kwamba Serikali ikakaa pembeni katika uandalizi wa timu za Taifa. Tumeona tumeenda juzi Jumuiya ya Madola imeendelea kuwa vichekesho vilevile. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ili tufanye hivyo hakuna namna, ni lazima Serikali kwa kushirikiana na wadau kwa namna yoyote, ni lazima i-take lead, tusiviachie Vyama vya Michezo, lazima Serikali i-take lead ndiyo tutavuna matunda mema. Vinginevyo tutajadili hapa, tutapiga madongo vyama vya michezo, bila Serikali kuweka mkono wake hakuna namna tutapiga hatua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, napenda kuhoji Mheshimiwa Waziri, wakati Serikali ikijibu swali Na. 62 hapa, ilieleza masuala ya udhamini ambao inaupata TFF kutoka kwa vyombo mbalimbali hapa nchini. Kama hii taarifa ni kweli na naiamini, kwa sababu ni ya Serikali, katika sehemu ya jibu ilisema; “aidha, TFF iliingia mkataba na Kampuni ya Bia ya TBL mwaka 2013 - 2017 kwa thamani ya Dola za Kimarekani milioni kumi kwa ajili ya Taifa. Mkataba huo ulishamalizika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, TFF imeingia mkataba wa ufadhili na Kampuni ya Bia ya Serengeti kwa miaka mitatu; 2017 - 2019, wenye thamani ya shilingi milioni 700 na milioni 450 kwa ajili ya Ligi Kuu ya Wanawake. Maana yake kimahesabu kati ya 2013 - 2017 ilikuwa dola milioni kumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kati ya 2017-2019 ni dola milioni moja. Hivi gharama za maisha zinapanda au zinashuka? Maana yake hii nimeitoa kwenye Hansard, kwamba mwaka 2013 - 2017 unaingia udhamini wa dola milioni kumi, 2017 - 2019 unaingia udhamini wa dola milioni moja. Sijui, yaani najaribu kufikiri, kwa kweli sipati picha na ningependa kwenye majumuisho Mheshimiwa Waziri atusaidie kutueleza jambo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, entertainment and media industry, kwa mujibu wa PWC, Tanzania ni kati ya nchi tano ambazo entertainment industry inakuwa kwa kasi sana. 2016 mapato yalikuwa dola milioni 504, sawa na shilingi trilioni 1.1. Kufikia 2021 inatarajiwa mapato yatakuwa dola bilioni 1.1, sawa na shilingi trilioni 2.4. Where is our stake? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wasanii wetu wananufaikaje katika hizi trilioni zinazoingia? Au ni fedha tu zinaishia kwenye makampuni ya kuuza data, kwenye makampuni ya promosheni? Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri hii vacuum ambayo inatokea kwenye media and entertainment industry naomba atakapokuja ku-wind up, atusaidie, Serikali ina mpango gani kuhakikisha kwamba wasanii wanaendelea kunufaika na hizi trilioni ambazo Taifa linaingiza? Kwa sababu katika 2.4 trillion mpaka mwaka 2021 hapa wasanii wakipata japo asilimia 20 tu, maana yake ni kwamba utakuwa umeongeza ajira ngapi katika Taifa? Wengi wanaofanya shughuli hii ni vijana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri, this entertainment and media industry is very potential. Hebu tutazame, tukae na hawa wasanii, tuwaelekeze tamaduni zetu, tuwape miongozo ili waendane na tamaduni na mila zetu lakini at the same time waweze kunufaika na kile kinachopatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya haya, napenda kuunga mkono hoja na nawatakia wapenzi wote na mashabiki wote wa Simba na Yanga mchezo bora Siku ya Jumapili. Ahsante sana.