Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Eng. Atashasta Justus Nditiye

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muhambwe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi ya kuchangia kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mwasiliano.

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kwanza kabisa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunipa uhai na kunifanya niweze kusimama mbele ya Bunge lako tukufu. Lakini nichukue nafasi hii vilevile kumshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuniamini na kuniteua niweze kumsaidia katika nafasi aliyonipatia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee kabisa namshukuru Waziri wangu Profesa Makame Mnyaa Mbarawa (Mbunge) kwa ushirikiano na muongozo anaonipatia mara kwa mara katika utendaji wa shughuli zangu. Nawashukuru vilevile watendaji, Dkt. Leonard Chamuriho - Katibu Mkuu wa Uchukuzi, Engineer Nyamuhanga - Katibu Mkuu wa Ujenzi na Dkt. Maria Sasabo - Katibu Mkuu wa Mawasiliano pamoja na Engineer Madete - Naibu Katibu Mkuu wa Mawasiliano kwa ushauri wanaonipatia katika kutenda majukumu yangu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii vilevile kuwashukuru wapiga kura wa Jimbo la Muhambwe ambao najua kabisa kwamba sasa hivi wanani-miss, lakini niwahakikishie kwamba niko nao katika majukumu yote ya Jimbo vilevile pamoja na kwamba siendi mara kwa mara. Naishukuru vilevile na familia yangu. (Makofi)

Mheshimia Naibu Spika, nitachangia kuhusu sekta ya mawasiliano pamoja na sekta ya uchukuzi kwa haraka haraka. Nimepata concern nyingi sana za Waheshimiwa Wabunge kuhusu masuala ya mawasiliano kwenye maeneo yao. Ni kweli kabisa kwamba takwimu za kiserikali zinaonesha kwamba nchi yetu tunawasiliana kwa asilimia 94, nitafafanua.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaposema kwamba tunawasiliana kwa asilimia 94 ni kwamba karibu maeneo mengi sana ya nchi yetu yanapata mtandao wa mawasiliano ya simu isipokuwa baadhi ya maeneo wanakuwa wako selective wanataka labda wapate na Vodacom, Tigo, Airtel pamoja na Halotel sasa Kiserikali hiyo hatuizuii ni kitu kizuri lakini sisi tunachosema kwamba eneo likipata huduma ya mawasiliano kama ni Halotel tunatia tiki kwamba hapo wanaweza wakawasiliana na kwa kweli katika hali ya kawaida kama kuna dharura yoyote wanaweza wakapata mawasiliano.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunao Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote unaitwa UCSAF ambao kazi yake kubwa unapeleka mawasiliano sehemu zile ambazo hakuna mvuto wa kibiashara. Tukumbuke siku za nyuma tulikuwa tunategemea sana hizi Kampuni za Simu kupeleka mawasiliano au minara sehemu ambazo wao wanaona kwamba zinafaa na zitawapatia faida katika majukumu yao ya kibiashara, lakini kutokana na hilo Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliamua kabisa kwamba tuunde Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote ambao sehemu ambazo hazina mvuto wa kibiashara basi wale UCSAF wataweza kupeleka mawasiliano. Hii ndiyo kazi maalum kwa ajili ya kupeleka mawasiliano kwa Watanzania wote.

Kwa hiyo majuku yake makubwa kwanza ni kupeleka mawasiliano sehemu ambazo hakuna mvuto wa kibiashara na ambako hakuna kabisa mawasiliano na hilo jukumu limeendeelea kufanyika maeneo mbalimbali ya nchi yetu. Tumegundua sehemu nyingi sana zimeshapelekewa minara hasa ya Halotel na hawa UCSAF wameingia mkataba na Halotel kwa ajili ya kupeleka mawasiliano sehemu hizo ambazo hakuna mvuto wa kibiashara.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vilevile kuna maeneo ya mipakani, Wabunge wengi sana waliochangia hasa wanaokaa maeneo ya mipakani kama mimi wamezungumzia kwa kirefu sana kwamba kuna maeneo ambayo wakiingia mtandao unaosoma ni wa nchi jirani. Hilo Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote umeliona, lakini kwa kushirikiana na TCRA kuna mpango mkakati unafanywa kuhakikisha tunapeleka minara yenye nguvu lakini na kuangalia masafa yanayozingatiwa ili kuhakikisha kwamba Watanzania wanapata mawasiliano ya Tanzania na hao wengine wanaendelea kupata mawasiliano ambayo yanawahusu kwa nchi zao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile eneo la tatu ambalo linasumbua ni minara iliyopo sasa hivi kutokuwa na nguvu, ni kweli kabsia maeneo mengi ya nchi yetu baadhi hayajapata huduma za umeme na ndiyo maana kupitia mpango wa umeme wa vijijini Awamu ya Tatu (REA III) tuna uhakika kwamba matatizo yatapungua.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwa kushirikiana na TCRA na UCSAF wameendelea kupeleka ujumbe kwa makampuni hayo ya simu yale ambayo yamepeleka solar waongeze nguvu ya hizo solar energy ili at least mawasiliano yaweze kupatikana masaa yote. Kwa sababu tumegundua kabisa ni kweli kwamba kama siku mvua imekuwa ikinyesha labda toka asubuhi mpaka mchana zile solar zinakuwa haziwezi ku-charge kwa sababu jua hakuna matokeo yake ikifika saa 12 jioni mawasiliano ya simu maeneo hayo yanakuwa hayapatikani.

Kwa hiyo, tumewashauri haya makampuni ya simu wamepele aidha, generator na hasa hasa wapeleke generator au waongeze nguvu ya zile solar kuhakikisha kwamba Watanzania wote wanapata mawasiliano.

Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote tunaendelea kufanya jitihada za kuhakikisha kwamba maeneo yote ambayo hayana mawasiliano yanapelekewa mawasiliano na hivi karibuni nimekuwa nikiongea na Wabunge na niliwaeleza waniletee tu maeneo ambayo wana uhakika kabisa hakuna mawasiliano ili kupitia mfuko wa mawasiliano kwa wote tuweze kuwapeleka minara waweze kupata mawasiliano.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitaongelea kiasi kwa haraka haraka kuhusu TCRA na majukumu yake. Waheshimiwa Wabunge mbalimbali wameizungumzia sana TCRA na ninashukuru sana kwa pongezi mbalimbali ambazo Waheshimiwa Wabunge mmezitoa kwa TCRA, kwa kweli tunazipokea na tunashukuru sana kwamba TCRA inaendelea kufanya kazi nzuri sana. Lakini niwakumbushe tu Wabunge kwamba pamoja na majukumu mbalimbali, TCRA vilevile inaendelea kuhakikisha tunadhibiti usalama wa mitandao yetu na tunasimamia masafa ili kuhakikisha kwamba nchi yetu inapata faida kutojua na masafa ambayo ilipangiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vilevile, TCRA imeendelea kusimamia upatikanaji wa mapato stahiki ya Serikali kutokana na matumizi ya mawasiliano na hasa kwa kutumia ule mtambo wetu ambao tumeufunga wa TTMS ambapo kwa kupitia TTMS tunapata telecommunication trafficking yote ya ndani na ya nje kwamba mtu anapopiga simu kutoka nje na watu wanaopiga simu kutoka ndani tunaona wametumia dakika ngapi, wametumia shilingi ngapi kwa hiyo stahiki ya Serikali ni kiasi gani na stahii ya hayo makampuni y simu ni kiasi gani.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kupitia hiyo nina uhakika kabisa TCRA wameendelea kuisaidia Seriakli na wananchi kwa ujumla lakini vievile wameendelea kuhakikisha kwamba wanapunguza matukio ya uhalifu kwenye mitandao.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi karibuni kutokana na mtandao kukua sana tumekuwa na changamoto mbalimbali za matumizi mabaya mitandao yetu ambako hata viongozi wamekuwa wakitukanwa, sisi wenyewe Wabunge tumekuwa tukidhalilishwa hapa na pale, lakini kupitia TCRA wametengeneza muundo ambao tunaendelea kuwadhibiti hawa wahalifu wa mitandao na hasa wale ambao wanaleta lugha ambazo hazina maadili kwenye nchi yetu kuhakikisha kwamba tunashirikiana na Jeshi la Polisi Kitengo cha Cybercrime kuhakikisha kwamba tunawadhibiti na matukio hayo kiasi fulani kwa kweli yamepungua na hata yanatokea mara nyingi tunao uwezo wa kuyafutailia na kuwakamata. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niongelee kwa haraka haraka kuhusu Data Centre, tunacho kituo cha Data Centre, kuna baadhi ya Wabunge wameliongelea. Kituo hiki kinaendelea kutumika vizuri ambapo hadi sasa tunavyoongea taasisi za Serikali 41 tayari zinakitumia kituo hiki na taasisi 11 za binafsi na zenywe zinakitumia.

Mheshimiwa Naibu Spika, umuhimu wa kituo hiki ni kuhakiakisha kwamba matumizi yote yale yanayofanywa kwa transaction, wka mfano, unapohamisha pesa kutoka kampuni ya simu kwenda benki, benki kwenda kampuni ya simu au unapolipia EWURA, unapolipia TANESCO na mambo mbalimbali kuna tozo zile za Kiserikali ambazo zinatakiwa zirudi Serikalini. Kwa kutumia Data Centre ni rahisi sana kwa TRA kuweza kuona mapato hayo na kweza kuyadai kutoka kwenye taasisi husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikuhakikishie tu kwamba kituo kinafanya vizuri na ninatoa wito kwa Makapuni mbalimbali kuendelea kujiunga na Data Centre ili kujiridhisha na kuhakikishiwa kwamba wanapata pesa na tender nyingi kutoka Serikalini kwa sababu Serikali inahitaji kuona pesa inayoitoa ione matumizi yake lakini ipate stahiki kutokana na pesa inayoitoa.

Mheshimiwa Naibu Spika, niongelee kwa haraka haraka kuhusu sekta ya uchukuzi…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha muda wa Mzungumzaji)

NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.