Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Susanne Peter Maselle

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. SUSANNE P. MASELLE: Mheshimiwa Naibu Spika, ni jambo lililo wazi kabisa kwamba kutokana na maendeleo ya kasi ya teknolojia ambayo yameathiri nyanja mbalimbali za maisha, ikiwemo sekta ya mawasiliano na uchukuzi, mtazamo na tafsiri katika sekta hizi umechukua wigo mpana sana. Kwa sasa ukizungumzia mawasiliano na uchukuzi unazungumzia ulinzi na usalama, unazungumzia haki na uwezo wa kupata taarifa na maarifa (elimu na ulinzi) kwa haraka, unazungumzia mwingiliano wa maisha ya kila siku ya binadamu katika nyanja zote zinazojulikana kuanzia uchumi, siasa, jamii na kila kitu kingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na ukweli huo, kupitia bajeti hii ya mwaka 2018/2019 ni vema Serikali ikalieleza Bunge ni kwa namna gani nchi yetu imejipanga katika sekta ya mawasiliano na uchukuzi katika zama hizi za mapinduzi makubwa, tumejipanga vipi kuyatekeleza hayo kwa vitendo?

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kupitia bajeti hii ya mwaka 2018/2019, sijaona mahali ambapo mipango na mikakati ya Serikali imeonesha kuwa Mkoa wa Mwanza unapaswa kuwa eneo la kimkakati katika nyanja za mawasiliano na uchukuzi hasa kwa eneo la Maziwa Makuu na kipekee kwa Afrika Mashariki. Nilitarajia Serikali hii ingetumia kadri inavyowezekana kimkakati ili Mwanza iwe kitovu cha usafiri kwa maana ya anga, maji na nchi kavu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ningetazamia katika nyakati hizi za ushindani mkubwa wa kibiashara na kiuchumi Serikali ingejikita katika kuimarisha na kuboresha miundombinu ya uchukuzi ili Mwanza kuwe kitovu cha usafiri kwa nchi za EAC, kwa maana ya kuunganika kwa njia ya barabara na nchi za Burundi, DRC, Uganda, Kenya, Rwanda na Sudani ya Kusini, na hii ni ahadi iliyowahi kutolewa na Rais Dkt. Magufuli mwenyewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali iwaambie wananchi wa Mkoa wa Mwanza ahadi hiyo imefikia wapi? Lakini wanataka kujua pia mikakati ya kuboresha na kurejesha reli yao, je, upo au ndiyo wasahau kabisa kama walishawahi kuwa na treni ambayo ndiyo usafiri rafiki kwa maendeleo ya kiuchumi duniani kote?

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, kumekuwepo na taarifa nyingi kuhusu dhamira ya kujengwa kwa daraja katika eneo la Kivuko cha Busisi – Kigongo. Ningependa kupata kauli ya Serikali suala hili limepewa uzito kiasi gani katika bajeti ya mwaka 2018/2019? Ili sasa isiwe tu maneno bali tuone utekelezaji, wananchi wa Mwanza hususani wanaotumia kivuko hiki kwa ajili ya kuingia na kutoka Jijini Mwanza kuelekea Sengerema, Buchosa au Mikoa ya jirani ya Geita, Kagera hadi nchi jirani za Rwanda, Burundi, Uganda hadi DRC na kwingine wanataka kujua, je, ujenzi huu unaanza na kukamilika lini? Je, daraja litakalojengwa litakuwa la namna gani? Na sasa tuko katika hatua gani?

Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na mipango ya ujenzi wa meli, vivuko, kukarabati meli na vivuko vinavyofanya kazi katika maeneo mbalimbali ya Ziwa Victoria ikiwemo pamoja na baadhi ya maeneo ya visiwa 36 vilivyoko ziwani humo, nataka kusikia kutoka Serikalini, je, kwa mwaka huu unaoisha wamefanya ukaguzi wa vivuko au meli ngapi ili kupima uimara wake na ufanisi wake au tunasubiri kufanya ukaguzi pale tunapopata majanga? Je, mipango ya ujenzi wa meli na vivuko na ukarabati wa meli na vivuko unahusiana na vivuko vingapi na katika maeneo yapi hasa?

Mheshimiwa Naibu Spika, je, katika vivuko hivyo Serikali ina mpango gani kukifanyia ukarabati mkubwa Kivuko cha Kome – Nyakalilo ambacho ni wazi kabisa kimeshaonesha dalili zote za kuchoka, kinaelemewa na abiria na mizigo hivyo kusababisha adha ya usafiri wa majini na usalama wa abiria na mali zao kutokuwa wa uhakika? Serikali inasubiri hadi maafa yatokee ndiyo iweze kukifanyia kazi?

Mheshimiwa Naibu Spika, hali ya Kivuko cha Kome – Nyakalilo inavikabili vivuko vingi mathalani Kivuko cha Luchelele na mahali pengine, nasisitiza Serikali itoe takwimu ya jumla ya vivuko vinavyofanya kazi ndani ya Ziwa Victoria na viko katika hali gani kwa kila kimoja. Vivyo hivyo, takwimu za meli zinazofanya kazi Ziwa Victoria na hali zake.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) ulitoa ruzuku kwa makampuni ya simu ili kufikisha na kuboresha huduma za mawasiliano vijijini na kwenye maeneo yasiyokuwa na wa kibiashara, kwa Kanda ya Ziwa Mikoa iliyobahatika ni Mwanza na Mara. Ningependa kujua mpango huo umekuwa na mafanikio kiasi gani? Ruzuku hiyo ilitolewa kwa namna gani na kwa utaratibu upi na ilikuwa kiasi gani na makampuni yapi yaliyopewa?

Mheshimiwa Naibu Spika, nauliza hivyo kwa sababu hali ya mawasiliano katika maeneo mengi ya vijijini bado siyo nzuri huku maeneo mengine yakiwa hayana mawasiliano kabisa, hasa maeneo ya visiwani ambayo yana vivutio vya kibiashara.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.