Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Mbaraka Kitwana Dau

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafia

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa fursa hii. Nianze kwa kuunga mkono hoja. Nimpongeze Mheshimiwa Waziri, Profesa Makame Mbarawa kwa hotuba nzuri yenye kuleta matumaini kwa Watanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Mafia ambayo kijiografia ni kisiwa ina tatizo kubwa la usafiri wa bahari kutoka na kuingia Mafia kupitia Bandari ya Nyamisati iliyopo Wilaya ya Kibiti. Tunaishukuru Serikali katika bajeti hii tumeona zimetengwa shilingi bilioni tatu kuanza ujenzi wa meli ya kisasa. Kwa kuwa mchakato wa kujenga meli hii utachukua muda wa miaka takribani miwili tunaiomba Serikali itupatie kivuko/meli ya muda wakati tunasubiri mchakato wa kujenga kivuko chetu ukiendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, tunaiomba Serikali iagize SUMATRA waje kuangalia upya katazo waliloliweka la kupakia abiria 50 tu kwa boti zinazofanya kazi sasa hivi ambazo uwezo wake wa kupakia abiria ni mkubwa sana mpaka kufikia abiria 200. Kwa hali ilivyo sasa wananchi wanalazimika kusubiri mpaka wiki nzima, jambo ambalo linaleta usumbufu hususani kwa wagonjwa na wenye dharura mbalimbali. Tunaiomba SUMATRA waje Mafia na kuliangalia suala hili kwa kushirikiana na wadau wa Mafia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu uwanja wa ndege wa Mafia ni muhimu sana katika kukuza utalii nchini, Wilaya ya Mafia inapokea watalii zaidi ya 10,000 kila mwaka na wote hao wanatumia uwanja huu wa ndege. Mafia imejaliwa vivutio vingi vya utalii ikiwemo maeneo ya scuba diving, sports fishing, fukwe nzuri na samaki wa ajabu aina ya potwe (whaleshark) ambaye anapatikana katika nchi chache duniani lakini hali ya uwanja wa ndege wa Mafia ni mbaya sana, hakuna jengo la abiria (terminal building),barabara ya kutua na kurukia (runway) ni fupi yenye urefu kiasi cha mita 800 hali ambayo hairuhusu ndege kubwa aina ya Boeing kutua na kusababisha kukosekana kwa safari za moja kwa moja kutoka nchi za ughaibuni kuja Mafia.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya kutoka Kilindoni mpaka Ras Mkumbi kilometa 55 ipo katika Ilani ya CCM 2010 – 2015 na ahadi ya Rais wa Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Kikwete. Hali ya barabara hii ni mbaya sana na nyakati za masika inakatika na kuvunja mawasiliano baina ya Tarafa ya Kaskazini na Tarafa ya Kusini. Vilevile udongo unaotumika katika kufanya matengenezo ya kawaida (periodical maintenance) unapatikana kwenye vijiji viwili tu vya Bweni na Jimbo, udongo huo unakaribia kuisha na wahandisi wanasema umebaki udongo wa kutumika kwa miaka mitatu tu, baada ya hapo tutalazimika kutoa udongo kutoka Rufiji. Njia nyepesi ni barabara hii kuwekwa lami ili kuepusha gharama kubwa ya matengenezo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru na naunga mkono hoja.