Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Richard Mganga Ndassa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sumve

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyotangulia kusema, ni kazi kubwa inayofanywa na Rais wetu ambaye ni mzalendo namba one katika kuvifufua vyombo vyetu vya usafiri kama ndege, meli na ujenzi wa reli (SGR). Niliwahi kusema na kuomba kuhusu TRL mara itakapokamilika naomba treni hiyo katika safari zake isimame katika kituo (station) ya Bukwimba, kwa kuwa jiografia ya Bukwimba ni eneo linalofaa kuwa na bandari kavu. Hii itasaidia kwa station ya Fela na Mwanza South kupumua. Stesheni ya Mwanza pamejaa, ukiweka bandari kavu Bukwimba itasaidia kwa wafanyabiashara wenye mizigo yao kuichukulia Bukwimba badala ya Fela au Malampaka. Miundombinu ya Bukwimba inajitosheleza.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri naomba nipate majibu hii railway levy ambayo ni tozo ya 1.5% kwa mizigo inayopitia bandarini (magari, container na kadhalika) kutozwa hiyo asilimia, mfuko huu ulianza mwaka 2015/2016 na mara ya mwisho Serikali ililipa shilingi bilioni 38.41 kama advance kwa mkandarasi Dar es Salaam – Morogoro na hizo pesa tulikubaliana ziwe refenced kwa matumizi yaliyokusudiwa. Naomba kujua mambo mawili; je, hadi sasa ni kiasi gani cha pesa kimeshakusanywa kufuatia tozo hiyo? Ni kwa nini kiasi hicho hakipelekwi moja kwa moja kunakokusudiwa kama Bunge lilivyopitisha mwaka 2015/ 2016? Naomba kupata majibu kutoka Serikalini kuhusu mambo hayo mawili na ombi la bandari kavu Bukwimba station.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono na kuwapongeza Mheshimiwa Waziri na timu yake yote na Wizara yake. Mheshimiwa Waziri naomba kutoa ushauri katika maeneo yafuatayo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, TCRA ni moja ya taasisi muhimu sana katika uchumi wa nchi yetu. Yapo makampuni ya simu ambayo baada ya agizo la Mheshimiwa Rais alipozindua National Data Center na kuyataka makampuni ya simu kujiunga ili kubaini kama makampuni hayo yanalipa VAT inayotakiwa; lakini hadi leo baadhi yao hayaja-comply. Naomba kujua kwa nini makampuni hayo yameshindwa kutekeleza agizo la Rais wetu?

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara na madaraja; mwaka 2017 Serikali ilitenga zaidi kilometa 200 za kufanya upembuzi yakinifu kwa barabara ya Ilungu(Magu) Bukwimba – Ngudu – hadi Hungumalwa. Katika kitabu chake cha bajeti sijaona popote pesa zilizotengewa kwa ajili ya barabara hiyo. Naomba kujua ni kwa nini barabara hiyo haijatengewa pesa?

Mheshimiwa Naibu Spika, Daraja la Mto Simiyu (barabaraya Magu - Mara); daraja hilo ni muhimu sana. Ikumbukwe kuwa daraja hilo limecheza, hivi sasa kwenye daraja hilo magari hayaruhusiwi kupita nyakati za usiku kutokana na mvua. Lakini ukweli na watalam wako wanajua kuwa daraja hilo limechoka, ipo haja ya daraja hilo kujengewa upya.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu TTCL huyu ni mtoto wetu lazima tumbebe kwa mbeleko ya Taifa. TTCL ni Shirika linalotoa huduma, lakini pia kupitia Mkongo wa Taifa tuutegemee kiuchumi na kiusalama, Serikali lazima tulilinde.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu DMI na NIT; vyuoni hivi viwanda vya kuzalisha wataalam wa kwenye maji na barabarani, Serikali iviimarishe vyuo vyetu kwa kuzipa hela za kutosha kutokana na bajeti yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa ATCL, nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa upendo mkubwa sana kwa Taifa. Rais Magufuli ni mzalendo number one kwa nchi yake, hasa katika kulifufua shirika. Ushauri wangu kwa Bodi ya Wakurugenzi katika kulisimamia vizuri shirika kwa kushirikiana na uongozi wote wa shirika. Hii ni katika kumuunga mkono Mheshimiwa Rais. Tuachanena wanaobeza jitihada za shirika, tunalitaka shirika letu la ATCL lisiwasikilize wapinga kila kitu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.