Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Japhet Ngailonga Hasunga (CPA)

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Vwawa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote naomba nichukue nafasi kwanza kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi nzuri ambayo ameendelea kuifanya na kuingoza nchi yetu ili tuweze kufikia katika uchumi wa kati. Pia naomba nichukue nafsi hii kumpongeza Waziri wa Ujenzi Mawasiliano na Uchukuzi pamoja na Naibu Mawaziri na Viongozi wote wa Wizara hii kwa kazi nzuri ambayo wameendelea kuifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ya muda nitazungumza kwa kifupi nitazungumza hoja chache. Waheshimiwa Wabunge katika kutoa michango yao wamechangia katika maeneo mengi, lakini moja ya maeneo ambayo wameyazungumzia kwa kiwango kikubwa ni pamoja na miundombinu ambayo inaenda katika hifadhi zetu, inayokwenda katika vivutia mbalimbali vya utalii nchini kwetu, wengi wametoa malalamiko na wamezungumzia. Naomba nichukue nafasi hii kusema kwamba nchi yetu ukiangalia maliasili tulizonazo, ukiangalia malikale tulizonazo, ukiangalia hifadhi tulizo nazo milima, maziwa na mambo mengine yote lazima kama Serikali tuwekeze vibaya sana katika maeneo haya ili tuweze kuvutia utalii na tuweze kupata mapato ya kutosha yanatokana na utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuona kwamba hii ni sehemu pekee tunayoweza kupata mapato makubwa tumeamua kuweka nguvu kabisa katika kuimarisha miundombinu ambayo inaunganisha vivutio vyetu vya utalii katika maeneo mengi. Ndiyo maana utaona tunajenga viwanja vya ndege tumezungumzia Uwanja wa Ndege wa Iringa, Uwanja wa Ndege wa Chato ambao utafufua utalii katika maeneo yote yale na katika hifadhi zote zinazoonekana Selous na maeneo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo lazima Serikali iwekeze katika miundombinu ya barabara tunataka watalii wa nchi hii wanaokuja katika maeneo yetu wawe na uwezo wa kwenda kwa barabara, wawe na uwezo kwenda kwa ndege, wawe na uwezo wa kwenda kwa kutumia reli, wawe na uwezo wa kwenda kwa kutumia boti na vitu vingine vyote kila mtu atajipima uwezo wake yeye mwenyewe. Ndiyo maana Serikali inawekeza katika maeneo haya, uwekezaji wa namna hii tutapata mavuno makubwa sana baada ya miaka miwili/mitatu inayokuja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na hali hiyo ndiyo maana Serikali sasa tumeamua kununua ndege za kutosha, ndege hizi zitafanya kazi kubwa katika kuvutia utalii na kuimarisha utalii wa nchi yetu. Wapo watu wataongea maneno mengi, ndugu zangu utajiri huu tulio nalo mimi naamini kwanza hizi ndege tunazonunua ni chache ukiangalia hali tuliyonayo bado ni chache, tunahitaji nyingi zaidi. Mimi nadhani tungehitaji tuwe na Dream Liner angalau nne kwa pamoja; mbili ziwe zinaenda Marekani zinapishana kuleta watalii moja kwa moja kuja hapa, mbili ziwe zinaenda bara la Asia kuleta watalii moja kwa moja sasa hivi tunayo moja bado hazitoshi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, watu wanazungumzia hii moja/mbili sijui taratibu, taratibu zipi unachozungumzia hapa ni kuwekeza ili tupate mapato ya kutosha yanayotokana na sekta ya utalii na mambo mengine katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Watanzania, naomba Wabunge wenzangu tuyaangalie mambo haya kwa mtazamo mpana ili nchi yetu iweze kusonga mbele tuweze kupata mapato ya kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia watalii sasahivi walioko kwenye nchi yetu ambao wamekuja kwa mwaka 2016 tulipata watalii 1,284,279 ambao walituletea bilioni 2.1 dola za Marekani, mwaka 2017 tumepata watalii 1,324,143 wametuletea bilioni 2.3 dola za Marekani; bado ukiangalia vivutio tulivyonavyo watalii hawatoshi. Nchi ya Italia peke yake ukichukua lile Jimbo la Platino peke yake lenyewe lina watu laki sita, lakini linapata watalii milioni sita kwa mwaka sisi ukichukua vyote bado hatuna. (Makofi)

Kwa hiyo, ndiyo maana tunasema lazima tuwekeze, hii reli ya kati standard gauge kwetu sisi ni fursa ya utalii, italeta watalii wengi itatusaidia sana. Kwa hiyo, naomba wale wanaozungumzia sijui ATC imepata hasara, siyo wakati huu sasa hivi ndo tunawekeza hatuwezi kuzungumzia hasara leo, baada ya muda tutapata muda wa kutosha wa kuweza kutathaimini na kuona kwamba hasara ipo au haipo sasa hivi ni wakati wa uwekezaj. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja naipongeza sana Serikali.