Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Victor Kilasile Mwambalaswa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lupa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kunipa nafasi niweze kuchangia hoja ambayo ipo mezani. Napenda kuchukua nafasi hii kuwapongeza sana Mheshimiwa Profesa Mbarawa na timu yako yote, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu wote; Wizara yenu kubwa sana lakini mnachapa kazi kweli kweli. Nimewahi kukuona Profesa Mbarawa unasafiri kutoka Mbeya kwenda mpaka Itigi kwa barabara ambayo ni mbaya sana ili uione barabara ile ilivyo, uje utujengee, hongereni sana na endeleeni kuchapa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na wahenga wanasema mfinyanzi huulia gaeni, lakini kwa hapa Dodoma Area D Site II TBA angalieni pale maana yake barabara ya kuingia pale ni mahandaki, gari limezima, naomba TBA mtengeneze barabara ile ya kwenda Site II. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naishukuru sana Serikali kwa kujenga barabara ya lami kutoka Mbeya kwenda Chunya kuelekea Makongorosi, barabara imekamilika nauli zimeshuka na usafiri upo siku nzima kati ya Mbeya na Chunya, nawashukuru sana kilometa 72 zimekamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi Serikali imetenga fedha za kuanza ujenzi kutoka Mbeya kwenda Makongorosi kilometa 43, asanteni sana. Pia mmetenga fedha za kuanza ujenzi kutoka Mkiwa kwenda Itigi ili baadaye Chunya mtapopanda na Itigi wanashuka tukutane katikati, naishukuru sana Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo lipo moja, hii barabara ya Mbeya – Chunya kwetu sisi ni tunu (master piece) imeturahisishia maisha mno, lakini sasa bahati mbaya Chunya kuna mazao mawili ambayo yanaharibu barabara; kuna mazao ya miti (mbao) na kuna tumbaku. Wachukuzi wanaochukua mizigo hiyo wanabeba malori ya lumbesa ili wakifika Mbeya ndio wagawe yawe magari mawili, wanaharibu barabara.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba Mheshimiwa Waziri utuwekee weight bridge hata kama ni mobile weigh bridge tuweze kuyadhibiti magari hayo maana yanasafiri usiku, ahsante sana najua utatufanyia hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia ninaipongeza Serikali kwa kuiboresha Tanzania – Zambia highway, mmejenga vizuri sana kuanzia Makuyuni mmekwenda mpaka Igawa sasa hivi ni barabara nzuri sana. sasa hivi kutoka Igawa kwenda Mbeya iko kwenye usanifu na kutoka Mbeya kwenda Tunduma ipo kwenye usanifu. Kama alivyosema Mheshimiwa Mwakibete, ninaomba mtakapokuwa mnajenga sasa kutoka Igawa kwenda Mbeya mkifika Mlima Nyoka mfanye bypass ya kwenda kutokea Mbalizi tujaribu kupunguza congestion katika Jiji la Mbeya. Tuiboreshe hiyo barabara ya katikati ya Mbeya lakini hiyo ya Mlima Nyoka kwenda Mbalizi iwe bypass, naomba muifikirie hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nataka niongelee kama walivyoongea wenzangu Mheshimiwa Njeza na Mheshimiwa Mwakibete, Uwanja wa Songwe. Kwanza ninaiomba Serikali Mkoani ianze mchakato wa kubadilisha jina kwamba isiitwe Uwanja wa Songwe, tutafute jina lingine maana yake Songwe ni Mkoa mwingine, kwa hiyo, tutakuwa tunatangaza mkoa mwingine. Samahani Mheshimiwa Naibu Waziri wa Michezo sikubagui, lakini ni mkoa mwingine, tuite jina lingine lakini uwanja huo umekamilka upo vizuri. Sasa hivi ndege wakati wa mvua zinakwenda pale wakati mwingine zinashindwa kutua pale zinarudi kwa sababu hakuna taa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hela imetengwa humu, ninaomba taa za kuongoza ndege na ukuta ujengwe naomba jengo la abiria likamilike. Ninajua Serikali imevunja mkataba na mkandarasi aliyekuwepo kwa sababu za kiufundi, ninaomba mteue mkandarasi mwingine haraka ili tukamilishe uwanja huo uanze kusaidia wana Mbeya kwa kiuchumi, tuna mazao mengi, parachichi, ndizi, viazi, mpunga na kila kitu, tuutumie uwanja huo vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, yapo mashirika mengi ya nje kama Emirates yapo tayari kwenda kuchukua mizigo Uwanja wa Songwe, lakini mpaka taa ziwepo na uzio wa uwanja uwepo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ninaiomba sana Serikali katika bajeti hii ya mwaka huu ikamilishe vitu hivyo vitatu; taa za kuongoza ndege, jengo la abiria na uzio katika uwanja huu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana kunipa nafasi hii, ninaunga mkono hoja, ahsante sana.