Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Atupele Fredy Mwakibete

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Busokelo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. FREDY A. MWAKIBETE: Mheshimiwa Naibu Spika, asante sana kwa kunipa fursa na mimi niweze kuchangia katika hotuba hii ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano. Kabla ya yote kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa namna ambavyo anafanya maamuzi yaliyo mengi mazuri katika sekta hii ya uchukuzi na mawasiliano. Lakini pia niipongeze Wizara hii pamoja na Waziri, Naibu Mawaziri na watendaji wake wote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto kubwa katika Jimbo la Busokelo ni barabara ambayo imeahidiwa kwa miaka mingi na Marais wote waliopita ukiachana na Baba wa Taifa ambayo ni Katumba – Lwangwa – Mbambo – Tukuyu yenye kilometa 85. Bahati nzuri sana nimeenda mara nyingi kwa Katibu Mkuu na amekuwa akiniahidi mara kwa mara lakini mara nyingi pia nimewasiliana na Waziri, nimepeleka mpaka maandiko lakini hadi hivi leo ninavyozungumza katika bajeti yake hakuna jambo ambalo limefanyika ambalo lilitakiwa lifanyike mwaka jana kwa bajeti ya mwaka 2017/2018. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii ni muhimu sana kwa wananchi wetu wa Busokelo na Rungwe kwa sababu kwanza gesi asilia aina ya carbon dioxide inapatikana kule lakini pia kuna aina mbalimbali ya mazao kama ndizi, viazi na maziwa kwa ajili ya ufugaji lakini barabara hii hata hivi ninavyozungumza wiki iliyopita tulikuwa na Mheshimiwa Waziri wa Nishati, tulikwama kwa zaidi ya dakika kadhaa kwa sababu ya barabara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba Serikali na Wizara hii ichukulie umuhimu mkubwa barabara hii kwa sababu hata Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 28 Agosti, 2015 saa 6.30 pale viwanja vya Tukuyu Mjini aliahidi barabara hii kwamba ataitengeneza kwa kiwango cha lami. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niombe sana Mheshimiwa Waziri utakapokuja kujibu useme kwamba barabara hii itaanza lini kutengenezwa kwa sababu mwaka huu wa fedha unakwisha na bajeti ilishatengwa hakuna lolote ambalo limefanyika, sielewi ni nini kinachoendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni barabara ya kutoka Luteba (Mbeya) – Makete – Njombe, ni barabara mpya ambayo inaunganisha mikoa yote miwili. Nikiwa Mbunge nimekuwa mbele pamoja na wananchi wangu kulima kwa jembe la mkono. Je, Serikali inatusaidiaje katika barabara hii kuhakikisha kwamba tunaunganisha mikoa yote miwili ya Njombe pamoja Mkoa wa Mbeya kupitia Luteba mpaka Makete. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama Serikali haitakuwa na fedha basi nikuombe Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu wako na Katibu Mkuu twende wote tukalime kwa kushika jembe la mkono kwa sababu ninaona kila mara nikiandika hata maandiko tangu mwaka 2016 bado haya mambo hayaendi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo, kuna barabara pia ya mchepuo wa kutoka Uyole kwenda Mbalizi barabara hii ni muhimu sana kwa wananchi wa Mbeya Jiji. Kwa sababu mahali pale katikati ya Jiji kumekuwa na foleni kubwa ukizingatia kwamba ule mji unakua kwa kasi. Kwa hiyo, tunaomba mchepuo wa barabara itakayoanzia Uyole kwenda Mbalizi na Songwe airport iweze kukamilika ili magari makubwa yawe yanapita ile diversion. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna jambo kubwa hili la Uwanja wa Ndege wa Songwe. Bahati nzuri sana Kamati yetu ya PIC tulikwenda kutembelea ule uwanja na kila mara nimemsikia Mheshimiwa Waziri hapa akijibu kwamba tunatengeneza taa za kuongozea ndege. Kwa bahati mbaya sana anasema ni shilingi bilioni nne lakini kwenye bajeti hapa ipo shilingi bilioni 3.7 na hizi fedha hazitatosha kutengeneza taa za kuongozea ndege pamoja na kujenga ukuta na runway, haitawezekana kwa fedha ambazo zipo hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tuiombe Serikali kwamba iweze kutenga fedha za kutosha katika uwanja huu wa kimataifa na ikizingatiwa kuwa katika nchi yetu ya Tanzania kuna viwanja vikubwa vinne ambavyo vinaweza kusaidia viwanja vingine. Zaidi ya viwanja 54 vinahitaji kupata mapato kutoka viwanja vya Julius Kambarage Nyerere, Songwe, KIA na Mwanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwahiyo, ningeishauri Serikali kwamba laiti kama tungeweza kuviwezesha hivi viwanja na vikaweza kukamilika ili fedha zile sasa ziweze kusaidia viwanja vingine ambavyo vipo kwenye mpango wa kutengenezwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine muhimu ni suala la mawasiliano, katika sekta ya mawasiliano inachangia asilimia 13.1 ya pato la Taifa na kwa msingi huo tumeona mara nyingi database zetu ama software ambazo zinatumika katika mawasiliano zinatumia commercial software. Nikiwa mdau wa mawasiliano (TEHAMA) ningeshauri kwamba ianze kutumia open source kama vile Firefox, Fidora, Tomcat, http server na nyinginezo nyingi ili kuipunguzia gharama Serikali wakati wa kuendesha hii mifumo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu open source ni mifumo ambayo inakuwa ni wazi kwa maana kwamba own source code anaweza aka-edit mtu yeyote yule, lakini ukitumia commercial software maana yake unahitaji kununua license na zinakuwa na expiring date na running cost yake inakuwa ni kubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia niweze kuzungumzia suala zima katika suala hilo hilo la mawasiliano tumeona pia katika hii issue ya commercial software kuna baadhi ya pirates software ambazo zinatumika kwenye taasisi za Serikali ambazo hazijalipiwa license na gharama yake ni kubwa sana. Ni kubwa kwa maana kwamba wale ambao wanatengeneza software incase wakijua kwamba taasisi za Serikali zinatumia software ambazo hazina license, Serikali lazima itakuja kulipa fedha nyingi. Kwa hiyo, nitoe tahadhari hiyo kwamba haitakiwi tuingie kulipa huko wakati tungeweza kutumia hizi open source software.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, ninapenda kuunga mkono hoja, lakini nimuombe mheshimiwa Waziri aje na majibu yaliyo sahihi sana juu ya barabara ya kutoka Katumba – Luangwa – Mbambo – Tukuyu na ikibidi barabara ya kwenda Makete kutoka Busokelo twende wote tukalime kwa jembe la mkono kama fedha hazitapatikana hapa, ahsante sana.