Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Desderius John Mipata

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nkasi Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. DESDERIUS J. MIPATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru, nadhani ninazo dakika kumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kupata nafasi pia namshukuru Mwenyezi Mungu kutulindia afya zetu. Natambua sana kazi za Mheshimiwa Rais anazozifanya katika nchi yetu lakini pia natambua kazi nzuri inayofanywa na Wizara. Mheshimiwa Waziri anafanya kazi vizuri Manaibu wake wawili pamoja na watendaji wa Wizara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mchango kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina shida kubwa sana ya mtandao katika Kata ya Kala na jambo hili nimekuwa nikizungumza zaidi na Mheshimiwa Waziri, vile vile na watendaji. Kata ya Kala ina Vijiji vya King’ombe, Kilambo, Mlambo, Kapumbuli, Mpasa, Lolesha, Tundu pamoja na Kala, vijiji vyote hivi havina mtandao na vijiji viko mpakani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ukiacha tena hiyo kuna vijiji viko Kata ya Sintali, Kijiji cha Kasapa, Kata ya Ninde, Kijiji cha Kisambala na Msamba, lakini vilevile Vijiji vya Nundwe, Mlalambo, havina mtandao, naomba Serikali itupelekee mtandao mara moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Mheshimiwa Waziri atusaidie vilevile barabara. Barabara sasa hivi sisi baada ya TARURA kuanza tulikuwa na mategemeo makubwa sana, lakini bajeti ya mwaka huu ya TARURA haipendezi hata kuiona kwa wale ambao wameziona. Unaweza ukaona hata halmashauri wakati fulani waliweza kuchukua hata own sources wakafungua barabara zinazojifunga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninavyozungumza hivi barabara zangu kadhaa zimejifunga. Naomba fedha za dharura zipelekwe, ili ziweze kupitika. Kuna Barabara ya Kisura – Junction – Malongwe, kuna Barabara ya Nkana – Kala kilometa 68 mabasi hayaendi, Barabara ya Kilambo – Mpasa – Junction haipitiki sasa, kuna barabara ya Kitosi – Wampembe, Barabara ya Katongoro - Namasi, barabara zote hizi hazipitiki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile niishukuru Serikali imetupatia hela kidogo kujenga barabara ya Katali – Miyula ambapo Vijiji vya Katani, Chonga, Makupa, Chelatila na Miyula vitaweza kuunganishwa vizuri na ni eneo la uzalishaji mzuri sana. Naomba Serikali ujenzi uanze mara moja ili kazi iweze kukamilika na wananchi wafaidi matunda ya Serikali yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Nkasi Kusini vilevile lina miji midogo iliyoko mwambao wa Ziwa Tanganyika; kuna Mji wa Kala, kuna Mji wa Wampembe. Mji wa Wampembe umeshakuwa mkubwa kiasi kwamba kuna shughuli nyingi za kibiashara na tunaomba tupate bandari, sio gati, tupate bandari Wampembe. Ni muda muafaka sasa, kuna biashara nyingi na ni makutano ya watu wa kutoka nje. Vilevile Kala kuna shughuli nyingi tunaweza tukapata bandari, kama sio bandari, basi tupate gati, itaweza kutusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona juhudi za Serikali katika kuimarisha usafiri wa majini. Nimeona nia njema ya Serikali ya kuimarisha usafiri wa majini kwani, katika kitabu chake Mheshimiwa Waziri tumeona kwamba, tarehe 18 mwezi huu kuna zabuni ya ununuzi wa meli mpya ya Ziwa Tanganyika imefunguliwa. Kwa hiyo, naomba mchakato huu uendelee, lakini vilevile nimeona kuna mchakato unaoendelea wa kutengeneza meli ya zamani ya Lihemba, jambo hili ni jema tunalifurahia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia, nifurahi kusema kwamba, tumeona juhudi ya kututengenezea uwanja wa ndege wa Sumbawanga ambapo tumetengewa zaidi ya bilioni 12. Hii sio kazi ndogo, kazi inayoenda kufanyika hapa ni fidia, kujenga uwanja pamoja na maeneo ya parking, ambapo ukikamilika tutaanza kuona Bombadier zinatua sasa. Ambazo sasa ni matunda ya Mheshimiwa Rais na Wanarukwa ambao hatujawahi kufaidi kwa kule, sasa tukitengenezewa huu uwanja wataweza kupata nafasi ya kufaidi na kuziona Bombadier. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia kusema kwamba, pamoja na ujenzi wa barabara ya lami kutoka Sumbawanga kwenda Mpanda kuna vijiji vilirukwa kwa barabara ya zamani iliyokuwa inaenda Mpanda. Kuna Vijiji vya Londokazi mpaka pale Palamayo kuna vijiji vingi hapa katikati, Vijiji kama vitatu vinne vya Mtenga, Mwai, Mashete, ni vijiji vya uzalishaji mkubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona pia kwenye bajeti hii kuna pesa nyingi inatengwa kwa ajili ya ukarabati wa eneo lile, Serikali ingefikiria eneo hili nalo iwekee lami. Kuna wananchi wa Londokazi waliniambia wanafurahi, tuwaombee kwamba, kwa vile lami imefika Chala ipite tu pale iunganishe, ili wananchi wote wa pale wanaolima mazao ya chakula katika maeneo hayo waweze kupata usafiri wa uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudie kupongeza utekelezaji wa ilani unaofanywa na Serikali ya Chama cha Mapinduzi. Rais wetu ni Rais wa Kimataifa kwa msingi kwamba, anazungumzwa ndani ya nchi na nje ya nchi na mikakati yake ni ya kipekee. Yale mambo ambayo yalionekana kushindikana wakati ule ndio hayo yameweza kushamiri na kufanya kazi vizuri zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hatushangai wanapompinga kupindukia kwa sababu, hoja zinaendelea kwisha, hawana namna nyingine ya kufanya lazima kupinga. Kwa sababu, kama wewe kazi yako ni kupinga hata jambo zuri utaendelea kupinga tu. Unaweza ukapinga kununua ndege, unaweza kupinga kujenga reli katika standard gauge, unaweza ukapinga mambo mazuri yanayofanywa katika nchi hii, jambo ambalo sio zuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba kuunga mkono hoja, naomba Mheshimiwa Waziri ahakikishe kwamba, ananipelekea mawasiliano Kata ya Kala na TARURA ipewe hela za dharura. Barabara hizo zimejifunga na ni wakulima, hawana namna nyingine ya kufanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. Ahsante.