Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Salome Wycliffe Makamba

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kunipa nafasi niweze kuchangia. Mwaka jana tulipitisha bajeti na tukakubaliana kwamba ili tuelekee Serikali ya viwanda, Tanzania ya viwanda, kuna baadhi ya maeneo ni lazima tuyaboreshe. Tukasema tutaboresha reli, tukasema tutaboresha barabara, bandari na maeneo mengi yenye vichocheo vya uchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa ya Kamati inaonesha kwenye ukurasa wa nne, Serikali haijapeleka bilioni 14 ambazo zilipitishwa kwa ajili ya sekta ya mawasiliano, haijapeleka bilioni sita ambazo tulipitisha kwa ajili ya kuboresha bandari ya Mwanza, hawajapeleka hata senti tano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali haijalipa Wakandarasi jambo ambalo limetuingiza kwenye deni la riba ya 3.9 bilioni, pesa hii tulipitisha lakini hazijapelekwa. Leo ni 2018 Watanzania wanaaminishwa tunakwenda kwenye Serikali ya Viwanda ilhali vichocheo ambavyo vinaweza kwenda kuhudumia viwanda kwa kusafirisha malighafi, kwa kuongeza utaalam mpaka leo havijapelekewa senti tano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulipitisha hapa bilioni mbili ikiwa ni pesa kwa ajili ya feasibility study ya uwanja wa ndege wa Chato, feasibility study, lakini leo tunaongea Bunge hili halikukaa halikupitisha popote uwanja wa ndege wa Chato umepelekewa bilioni 42 na completion stage ya project ya uwanja wa ndege wa chato ni zaidi ya asilimia 62, ilipitishwa wapi Bunge halikukaa, hatukuridhia, hakuna utaratibu wowote wa Serikali wa kimanunuzi ambao ulifanyika kupitisha ujenzi wa kiwanja hiki, leo tunacheka tu hapa na Serikali. Serikali inadharau Bunge, hakuna heshima kwa Bunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, CAG anasema asilimia 35 ya maoni yake aliyoyatoa katika ripoti yake mwaka jana haijafanyiwa kazi, Serikali imepuuza na wala hawaoni umuhimu wa kufanya hivyo, iko kwenye ripoti ya CAG. Bunge linalalamika asilimia kubwa ya bajeti yake iliyopitishwa humu Bungeni haijatekelezwa leo tunakaa hapa tunasema tunakaa kuishauri Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulizungumza hapa habari ya TARURA, tukasema tatizo la barabara za Wilaya sio chombo cha kutengeneza barabara, changamoto ni pesa katika maeneo haya. TARURA leo inatengewa asilimia 30, TANROAD inapewa asilimia 70, matokeo yake ni nini? Matokeo yake imeshindwa ku-perform kufanya kazi kwa sababu hawajapelekewa pesa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kahama ninakotoka mimi hakuna barabara inayopitika sasa hivi, ni mafuriko kila mahali, kwa sababu barabara zimeshashindwa kufanyiwa maintenance, pesa Serikali inapelekea inapotaka, halafu wanakuja hapa wanajifanya kichwa chini mikono nyuma, eti tuwape bajeti tuwapitishie, hakuna wanachokwenda kufanya ambacho tunashauri hapa Bungeni, wanatekeleza mambo yao wanayoyajua wao wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mawaziri hawa ni Mawaziri welevu sana, yaani mimi leo ningekuwa ni hawa Mawaziri ningeomba nipumzike, kwa sababu hakuna wanachofanya pale ofisini zaidi ya kutekeleza miradi ya kuletewa na sio miradi ambayo inatokana na michango ya wananchi kupitia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo kwa sababu tu, sio kwamba hakuna makusanyo, kwa sababu pesa haziendi kwenye miradi. Wanawalazimisha wataalam wetu watafute njia mbadala ya kupata pesa.