Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Hamidu Hassan Bobali

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Mchinga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. HAMIDU H. BOBALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuwa mchangiaji wa mwanzo katika kipindi hiki cha jioni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajadili bajeti ya Wizara ambayo inachukua takribani theluthi moja ya bajeti yetu ya nchi. Kwa hiyo, tunavyojadili bajeti ya Wizara hii kwanza ni vizuri ingependeza tukaondoa ushabiki tulionao badala yake tukachukua dhima na kazi yetu kama Bunge ya kuishauri na kuisimamia Serikali kwa sababu ni Wizara ambayo inatengewa fedha nyingi za kodi za walipa kodi wa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na suala la barabara zetu kujengwa na kuharibika mara kwa mara. Ni jambo la aibu sana kwamba barabara za nchi hii zinapojengwa kila ukifika wakati wa masika zinaharibika, kana kwamba wakandarasi wanaojenga barabara za Tanzania hawajui kama Tanzania inapata mvua kila mwaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, inatia hasira wakati mwingine ukiona kwamba barabara za Tanzania zilizojengwa kwa kiwango cha lami, ukifika wakati wa masika mvua zikinyesha basi zinabadilika na balaa lake katikati ya barabara utakuta madimbwi ya maji, kitu kinachopelekea kuchangia ajali mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi juzi nilikuwa nasafiri natoka Lindi nakuja Dar es Salaam, barabara ambayo imejengwa si zaidi ya miaka sita, miaka mitano iliyopita sasa hivi karibu barabara nzima inahitaji repair. Ni barabara ambayo nadhani imejengwa mwishoni kabisa mwa kipindi
cha Rais Kikwete, lakini ukipita sasa hivi ukitembea bila kuwa na tahadhali ni jambo la hatari sana. Sasa nashangaa kwamba tunapojenga barabara zetu hivi hakuna chombo kinachodhibiti ubora wa ujenzi wa barabara hasa hizi barabara za lami?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hakuna chombo nashauri, kwa kuwa tunatumia bilions of money kwenye suala la ujenzi wa barabara za lami, nashauri Bunge kama kuna nafasi ya kuunda Kamati Bunge lingeweza kuunda Kamati ya kuchunguza mikataba ya barabara hasa hizi trunk road ambazo zimejengwa ni barabara kubwa na zina umuhimu mkubwa katika uchumi wa nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haiingii akilini kuona barabara ya Lindi - Dar es Salam imejengwa juzi, leo hii barabara nzima ina viraka na kwa kweli ni barabara ambayo inatia kichefuchefu kabisa ukiwa unatembea kwenye ile barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni suala la ufufuaji wa shirika la ndege. Tunapaswa tuelewane humu kwamba hakuna mtu ambaye anakataa au anapinga shirika la ndege lisifufuliwe hakuna. Tunachopenda kushauri ni namna na njia inayotumika kulifufua shirika la ndege. Mathalani nyie wote mashahidi na Naibu Mawaziri wapo hapa wanasoma ripoti za IATA (Shirika la Ndege la Duniani) mnaona nini kinachoendelea kwenye mashirika ya ndege mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa takwimu zilizopo kwa mwaka mmoja mashirika ya ndege duniani yanapata hasara ya dola za Kimarekani bilioni nane kwa mwaka. Kwa Afrika pekee mwaka uliopita mashirika ya ndege yalipata hasara ya dola milioni 600, kwa Afrika pekee. Sasa ikiwa hali ndio hii tunapokwenda kulifufua shirika letu la ndege lazima tuwe na tahadhari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tahadhari mojawapo wako Wabunge wamechangia hapa walikuwa wanahoji kwamba hivi inakuwaje tuna ndege ambazo zinasafiri ndani ya nchi tu lakini wateja wetu wako mikoani tuna viwanja vya ndege havina taa, ndege hazitui usiku. Ni kana kwamba wakati tunanunua ndege tulijua labda tutasafiri kwenye viwanja vya kimataifa vya nje ya nchi, lakini najua kusudio la kununua bombadia zitumike ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama tumenunua ili zitumike ndani, kwa nini zaidi ya viwanja vya ndege zaidi ya asilimia 70 viwanja vya ndege nchi hii havina taa za usiku. Ndege zinapumzika, Mzee Zungu alikuwa anasema hapa ndege sio chombo kinachohitaji kupumzika, kwamba kimefanya kazi mchana usiku kipumzike hapana ndege zinasafiri wakati wote mchana, asubuhi, jioni, usiku, alfajiri wakati wote na nyie wote mnasafiri ni mashahidi mnajua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa inakuwaje ndege za Tanzania zinafanya kazi asubuhi, zinafanya kazi mchana ikifika usiku zinapumzika ni kama mabasi ya abiria vile, kwamba ikifika saa sita usiku basi yaache kusafirisha abiria labda wanaogopa kutekwa mimi sijui. Kama kweli tumekusudia kufufua shirika la ndege, jambo la kwanza lilipaswa kujenga miundombinu, tulitakiwa tujenge miundombinu ambayo itaendana na ufufuaji wa Shirika la Ndege. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitawapeni mfano, wote mnasafiri, ukifika Ethiopia pale Addis Ababa pale Bole International Airport jambo la kwanza utakaloliona ule uwanja wa ndege umezungukwa na hoteli kubwa za kifahari. Hii maana yake ni nini? Ni kwamba wanatoa picha kwamba Ethiopia Airlines inachangia kwa kiasi kikubwa sana biashara ya utalii na biashara ya hoteli ndio jibu wanalotoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi shirika letu la ndege hatuna hoteli ambazo ni nzuri tumezijenga ama zipo tumezi- attract, pia ndege zenyewe zinasafiri kuanzia saa 12 asubuhi mwisho saa 12 jioni maana yake ni kwamba tunatoa huduma kama huduma ya zahanati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukianza kufanya upembuzi yakinifu na tukaondoa ushabiki tukapima tunachokiingiza kwenye shirika letu la ndege tutakuwa tunapata hasara kubwa sana mimi sijawahi kuona shirika la ndege ambalo hili leo tunataka tulifufue, liwe linafanya kazi wakati wa mchana tu, tutapata hasara kubwa sana. Kwa hiyo, lazima tuchukue precaution kubwa kwamba kwa kuwa tunetenga pesa nyingi za walipa kodi wa Tanzania, basi haya mengine yaendane ili tuweze kupata faida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, faida ya mashirika ya ndege siku hizi watu hawaangalii tiketi , hawaangalii collection yatransport,ukiangalia huko hakuna Shirika la Ndege linazalisha pote, hata hiyo unayosikia Emirate unasikia Dubai Air, unayosikia Quatar Airlines, hawaangalii fedha ya tiketi wanaangalia income inayopatikana kutokana na sekta zingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivi kwa kuwa Shirika la Ndege ni catalyst ya maendeleo, iwe inachangia maendeleo kwenye sekta ya utalii, iwe inachangia maendeleo kwenye sekta zingine, ndio kinachoangaliwa, huangalii tiketi za ndege, hakuna shirika la ndege linapata faida kwa kuangalia tiketi, hakuna. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka nizungumzie ni suala la upandishaji wa barabara zetu, mimi nina barabara pale jimboni kwangu, ina miaka kadhaa tunaiombea ipande lakini sijaona hapa inapandishwa. Naomba sana barabara yetu ya Chikonji - Nangalu kwenda Milola ina urefu wa zaidi ya kilometa 100, waipandishe, watu wa TARURA hawaiwezi na nature ya ile barabara angekuwepo Mheshimiwa Waziri Mkuu hapa yeye ni shuhuda mkubwa sana kwa sababu wakati mwingine anaitumia kwenda kwake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nature ya ile barabara ni lazima iingie TANROAD ndio inawezekana ikafanyiwa marekebisho lakini hivi sasa inafika wakati kwamba tumeitumia season, kuna wakati hatuwezi kuitumia kabisa kwa sababu kuna madaraja makubwa yamekatika na inahitaji ukarabati mkubwa fedha za TARURA haiwezi kabisa kujenga ile barabara, kwa hiyo naomba hilo jambo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili nimepitia bajeti ya ukarabati wa hizi barabara za TANROAD ukiangalia hii bajeti na nimepitia vizuri sana kwa mikoa, mkoa ambao umepunjwa sana kuliko yoye ni Mkoa wa Tabora na bahati nimewasikia Wabunge wa Tabora wakisemea jambo hili, lakini mkoa uliofuatia ni Mkoa wa Lindi, yaani sisi Lindi tuna kilometa za barabara TANROAD kilometa 629 lakini kwa bahati mbaya tumepewa shilingi milioni 800.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili jambo linasikitisha sana kwamba ukiangalia mikoa mingine ambayo wana kilometa 400, wana kilometa 300, wanapewa fedha nyingi, sisi wenye kilometa 600 tunapewa shilingi milioni 800. Jamani mtuangalie na sisi Lindi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo inayosemwa korosho, ufuta inahitaji ipite kwenye barabara, inahitaji isafirishwe. Kwa mazingira haya tuliyonayo hivi sasa maana yake ni kwamba utafika wakati tutashindwa kusafirisha mazao yetu ya biashara na huo uchumi unaosemwa hautaweza kukua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho, ni suala la mitandao, tunao Mfuko wa Mawasiliano, hebu na sisi tuleteeni, nimeona kwenye ripoti yao nimepata angalau vijiji viwili pale jimboni kwangu, lakini uhalisia ni kwamba zaidi ya vijiji 15 vinahitaji kupata minara ambayo itawezesha wananchi kupata mawasiliano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba sana waingize kwenye record zao Vijiji kama vya Mputwa, Kiwawa, Namkongo, Nyamnyangala, Kijiweni, Mvuleni na Ruvu; hivi vijiji waviingize kwenye orodha ili viweze kupata fedha ya Mfuko huu na sisi tuweze kujengewa minara ili na sisi tuwe tunaishi katika Tanzania hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.