Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Hawa Abdulrahiman Ghasia

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Mtwara Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema nami kuweza kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu ili kuweza kuichangia bajeti hii muhimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nianze kwa kuipongeza Serikali ya Awamu ya Tano na kumpongeza Waziri pamoja na Manaibu wake na watendaji wote wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nianze kwa kuishukuru Serikali kwa upanuzi wa Bandari ya Mtwara ambao unaendelea vizuri. Ni imani yangu kwamba upanuzi ule utakamilika kwa wakati na hivyo kuwezesha huduma za usafirishaji katika mkoa wetu hasa za zao la korosho kwenda kwa ufanisi zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia niishukuru Wizara hii kwa kuanza upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Mtwara. Juzi nimetoka Mtwara nimeona magari pale yapo, nina imani kabisa kwamba kazi ile itaanza kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepitia katika kitabu cha hotuba na nimeona kazi zitakazofanyika. Napenda kupendekeza kwamba pamoja na kazi walizojiwekea ikiwa ni pamoja na kuweka taa katika uwanja ule, naomba pia suala la kujenga jengo la abiria na lenyewe liwekwe kwa sababu jengo lililopo lipo ndani ya uwanja. Kwa hiyo, ningeomba Mheshimiwa Waziri, yeye mwenyewe ameenda na ameona na pia lile jengo lililopo ni dogo na halitoshi kutokana na upanuzi ambao unataka kufanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda niipongeze Serikali kwa kununua ndege, sasa hivi tuna ndege ya tatu. Nina uhakika kabisa kwamba ufanisi wa Shirika la Ndege la Tanzania utakuwa ni wa kiwango cha juu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kutoa masikitiko yangu kwamba Bombadier zilikuwa zinakuja Mtwara lakini sasa hivi huu ni mwezi safari za Mtwara zimefutwa eti kwa sababu Kiwanja cha Ndege cha Songea ni kibovu. Sasa Kiwanja cha Ndege cha Songea kimeanza juzi, Kiwanja cha Ndege cha Mtwara kilikuwepo enzi na enzi na kilikuwa kinafanya kazi bila Kiwanja cha Ndege cha Songea. Sasa kama Kiwanja cha Ndege cha Songea kina matatizo, hakuna sababu yoyote ya kufungia ndege za ATCL kwenda Mtwara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama mnasema abiria ni wachache ni kutokana na ratiba zenu ambazo kwa kweli haziwavutii abiria. Mnaunganisha abiria wa Mtwara na Songea. Unaruka Dar es Salaam saa 6.30 unafika Mtwara saa 9.15, zaidi ya saa 2.45 wakati kutoka Mtwara mpaka Dar es Salaam ni dakika 50 kwa Bombadier. Hivi unafikiri kweli utaweza kushindana na Precision?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kawaida sisi kama ni kuunganishwa, tunaunganishwa na abiria wa Hahaya kule Comoro kwa sababu kutoka Comoro mpaka Mtwara ni dakika 25 mpaka dakika 30. Kwa hiyo, niwaombe warejeshe ndege Mtwara lakini watuunganishe na Comoro na nawahakikishia watajaza ndege kwa abiria kutoka Mtwara kama watakuwa na ratiba zilizo…

T A A R I F A . . .

MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, huyo ni mtani wangu, kwa hiyo sipendi kubishana na mtani wangu lakini ukweli anaujua na ninaozungumza nao nadhani wananielewa. Isipokuwa tu labda nimsaidie niseme uboreshaji wa Kiwanja cha Songea ufanyike kwa kasi ya hali ya juu ili mtani wangu naye aendelee ku-enjoy kwenda na ndege kwa sababu kwa sasa hivi hata wakiturudishia sisi hawezi kupata. Kwa hiyo, uboreshaji wa Kiwanja cha Ndege cha Mtwara uende sambamba na Songea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo nataka nilizungumzie ni suala la uunganishaji wa barabara zetu. Sera ya nchi ni kuunganisha barabara za nchi na nchi, lakini sasa hivi katika Mkoa wa Mtwara tunayo barabara ya kutoka Mtwara - Mozambique kupitia Kilambo ambayo ndiyo barabara inatumiwa na wananchi wengi wanaokwenda Mozambique.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaishukuru Wizara hii imetuwekea kivuko pale cha kisasa na watu wanatumia sana lakini barabara hii bado haijajengwa kwa kiwango cha lami. Kwa hiyo, niiombe Serikali iijenge barabara ya kutoka Kilambo kwenda Mtwara kwa kiwango cha lami kwa sababu inatuunganisha na majirani zetu wa Mozambique na ni sera ya nchi kuunganisha nchi kwa nchi kwa barabara za lami. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kuiomba Serikali kuharakisha mchakato wa kujenga reli ya kutoka Mtwara kwenda Mbamba Bay na matawi yake yanayokwenda Liganga na Mchuchuma. Upanuzi wa Bandari ya Mtwara kama hakutakuwa na reli itakuwa ni kazi bure. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Mtwara tuna kiwanda kikubwa sana cha Dangote, magari ya kiwanda kile hakuna lililo chini ya tani 30. Sasa hivi zile barabara zetu za udongo ni mahandaki. Ndiyo kusema bila kuwa na reli tunategemea Dangote achukue makaa ya mawe kutoka Ngaka na saruji isafirishwe kupelekwa Songea na mikoa mingine na tuchukue chuma na makaa ya mawe ya Liganga na Mchuchuma kwenda Mtwara bila kuwa na reli barabara zile kwa kweli zitaharibika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaipongeza sana Serikali kwa kuikamilisha barabara ya kutoka Dar es Salaam – Songea. Sasa hivi watani zetu wale wanaoogopa milima wanaitumia sana, mabasi karibu yote ya Songea yanapita barabara ya kutoka Mtwara ya Kilwa Road – Masasi - Tunduru - Ruvuma lakini bila kuwa na reli nina uhakika barabara ile itadumu kwa muda mfupi tu. Sasa hivi kwa ushahidi barabara ya Masasi – Mangaka - Tunduru imeshaanza kuharibika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niombe mchakato uharakishwe kuhakikisha kwamba ujenzi wa reli ile unakamilika. Upembuzi yakinifu ulishakamilika, tathmini ya mimea ya maeneo inapopita ilishakamilika na tunachoomba siyo lazima tutumie pesa za Serikali, tunaweza kujenga barabara ile kwa njia ya PPP na njia hii ndiyo itakayotusaidia pia kupunguza deni la Serikali kwa sababu hatutakopa. Tunaweza tukaingia ubia, sisi tukaweka mchango wetu na mwekezaji akaweka mchango wake na bado tukanufaika na matunda ya reli ile. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nimalizie kwa kuipongeza Serikali kwa kuanza ujenzi wa barabara ya kutoka Mtwara – Nanyamba - Tandahimba-Newala - Masasi. Sasa hivi tuko katika kilomita 50, nimeangalia katika kitabu cha bajeti sijaona ile barabara kuongezewa pesa. Mheshimiwa Rais alituahidi kwamba akishinda vipande vilivyobaki atatafuta wakandarasi wengi zaidi ili barabara ile ikamilike kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Profesa Mbarawa asimuangushe Rais wetu, nia yake ni njema kwa wananchi wa Mkoa wa Mtwara na Lindi kwa sababu barabara ile itakwenda mpaka Nachingwea na kutuunganisha pia na mikoa ya jirani zetu, watani zetu Songea, naomba aitekeleze kwa ufanisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja.