Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Andrew John Chenge

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bariadi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. ANDREW J. CHENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana kwa kunipatia nafasi hii. Nianze kwa kumpongeza sana mtoa hoja Mheshimiwa Profesa Mbarawa kwa hoja yake nzuri ambayo inatoa matumaini kwa Watanzania katika sekta zote tatu muhimu ambazo anaziongoza. Niwapongeze pia Naibu Mawaziri na watendaji wote wa Wizara hii kwa kazi kubwa wanayoifanya. Tanzania inafunguka na inaunganishwa, sote tunaona, hongereni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitasema kwa kifupi katika maeneo ambayo nadhani ni muhimu. Moja ambalo nadhani tusaidiane Waheshimiwa Wabunge ni hili la TANROADS na TARURA kwa upande wa financing. Nimesikia mawazo mazuri tu ya Waheshimiwa Wabunge kuhusiana na kuongeza nguvu ya financing lakini kwa kupendekeza kwamba asilimia 70 ambayo ndiyo inakwenda TANROADS na 30 inakwenda TARURA tufanye uwiano mzuri, ni wazo zuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachotaka kusema, ukiangalia mtandao wa barabara zetu hizi za lami ambazo tunajenga kwa gharama kubwa, barabara kuu na za mikoa, sehemu kubwa ni kama asilimia tunayoweza kugharamia kwa matengenezo/matunzo ya kila mwaka haifiki asilimia
60. Sehemu kubwa ya barabara hizi hazitunzwi, sasa ukipunguza tena ukasema upeleke TARURA ujue network kubwa ya nchi hii ambayo tumeijenga kwa gharama kubwa itaharibika haraka sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tuendelee kuishauri vizuri Serikali, tutafute vyanzo vipya vya mapato badala ya kwenda na approach hii. Najua zoezi hili limekuwa linafanyika, tufike mahali basi tuone hii road users’ fee or charges, mapendekezo yaliyokuwa yanafanyiwa kazi tumefika nayo wapi? Mimi naliona hilo ni bora kuliko hii ya kusema tukagawane mbao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuanzia mimi nachokoza tena, hii source ya shilingi ya mafuta nasema kwa sasa tujaribu kuiangalia tena. Maana yake nasema tuangalie kuongeza katika bajeti ya Serikali mwaka huu ili tukatunishe TARURA kwa kuanzia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza juhudi za Serikali kwa kazi inayofanyika Simiyu sasa hivi. Barabara ya Lamadi – Bariadi imekamilika, Mwigumbi – Maswa imekamilika, sehemu ya Bariadi – Maswa mkandarasi yuko site na bajeti tunaiona, shilingi bilioni kumi hizo zimetengwa na Serikali kwa mwaka ujao wa fedha. Matarajio yangu ni kwamba hata hicho kidogo kitapatikana ili mkandarasi afanye kazi na tuone kazi hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Mto Sibiti, daraja hilo linalotuunganisha sisi kwenye barabara ya kutoka Bariadi - Singida - Arusha linaendelea vizuri, tunaipongeza Serikali. Tunataka tuone barabara unganishi kwa pande zote mbili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe radhi sana Mheshimiwa Waziri, jana wakati na-chair Kikao nilisoma kwa harakaharaka nikamwandikia ki-note kwa sababu nilikuwa sijaisoma vizuri hotuba yake, ilikuwa ni barabara ya zaidi ya miaka 30. Tunaongelea barabara ya kutoka Kolandoto – Lalago – Mwanhuzi – Matala – Mang’ola – Oldeani Junction, kila Waziri aliyepita pale Wizarani barabara hii ipo. Najua pesa ndiyo hivyo, ombi langu kwa sababu imo kwenye mpangokazi wa TANROADS, tufike basi mahali vipande ambavyo vimekamilika tuanze kuvitengeneza kwa kiwango cha lami. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye ukurasa wa 32, baada ya kumwomba samahani Mheshimiwa Waziri kwa mkanganyiko wangu wa jana, barabara ya Karatu – Mbulu – Haydom - Mto Sibiti - Lalago – Maswa, mimi sina problem kwa sababu nataka tufungue nchi hii lakini unapoiangalia pale sehemu kubwa ya barabara hiyo kuanzia Kolandoto – Munze – Lalago – Mwanhuzi - Sibiti - Mang’ola - Oldeani Junction tumeshafanya upembuzi yakinifu na detailed design, sasa wanapoichanganya hivi wanatuchanganya, si kweli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama KfW wanatoa hizi pesa tunawapongeza na tunawashukuru, lakini sehemu kubwa imeshafanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina. Waheshimiwa napenda waje wanisaidie kwa maelezo yanayotosheleza kwenye eneo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda tusaidiane kuelewa. Hii barabara inayopendekezwa ya kutoka Karatu – Endebash, ninavyoifahamu ni kansa, unashuka nayo unakuja mpaka Kilimapunda pale, unashuka nayo Mbulu unakwenda Dongobesh unakwenda Haydom. Sasa napenda tusaidiane, ikitoka Haydom inaelekea wapi, inaenda Matala au Kidarafa? Napenda tuelewane maana hatuwezi kuwa tunafichana njia hii inapita wapi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naungana na wazo la Serikali kwamba ikitoka pale tunarudi sasa Sibiti tunapandisha kwenda Mwanhuzi anayetaka kwenda Shinyanga anakata mpaka Lalago lakini ukifika pale Lalago unapandisha kwenda Maswa. Ndiyo utamu wa mapendekezo haya. Nadhani ma-engineer wote hebu waliangalie hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baadaye tungependa tuone barabara inayounganisha upande wa Singida, barabara ya kutoka Sibiti maana chemchemi unaiona pale, unashuka kuja Mkalama, si ndiyo hivyo, halafu unakuja Gamanga, Ilemo huku au unaweza ukaja moja kwa moja mpaka Iguguno, tusaidiwe kuelewa barabara unganishi ni ipi? Nataka tu wanisaidie lakini nataka maendeleo ya haraka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hizi tunazijenga kwa gharama kubwa. Nisingependa tugombanie fito, lakini angalau kama hii ya Kolandoto nairudia sana, tuwe na muono wa pamoja hasa katika maeneo ambayo hayana connectivity nzuri kama Mkoa mpya wa Simiyu. Nadhani Mheshimiwa Profesa Mbarawa atanielewa kwa nini nalisema kwa uchungu namna hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, napongeza sana upande wa reli, napongeza sana reli ya kisasa kiwango cha kimataifa. Ombi langu kwa Serikali na nalisema kwa kujivuna, twendeni tukakope tushambulie maeneo yote kwa pamoja tusiende kwa spidi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.