Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Capt. Abbas Ali Mwinyi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Fuoni

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. ABBAS ALI HASSAN MWINYI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili nami nichangie hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano. Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uhai na kutuwezesha kukutana asubuhi ya leo kwa lengo la kujadili maendeleo ya sekta ya ujenzi, uchukuzi na mawasiliano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii ya adhimu na adimu ya kumshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Joseph Pombe Magufuli na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mheshimiwa Ali Mohamed Shein kwa kutekeleza kwa umahiri mkubwa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Awamu ya Tano imefanya kazi kubwa ndani ya kipindi cha muda mfupi sana na baadhi ya mambo waliyofanya yaliyoleta tija kubwa ni pamoja na kupata mafanikio katika sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya afya, bajeti imeongezeka kwa kiasi kikubwa sana na sasa hivi hata hospitali zetu za rufaa msongamano wa wagonjwa umepungua kwa kiasi kikubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii inatokana na kuimarisha hospitali zetu za wilaya na vituo vyetu vya afya. Sio hayo tu bali hata wale wagonjwa waliokuwa na matatizo ya kuwekewa figo (kidney transplant) na wale ambao walikuwa na matatizo ya moyo hali kadhalika sasa huduma tunazo hapa hapa nchini na kwa hali hiyo basi Serikali imeweza ku- save pesa nyingi za kuwapeleka nje ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nichukue fursa hii ya kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano pamoja na Naibu Mawaziri wake wawili, Mheshimiwa Nditiye na Mheshimiwa Kwandikwa kwa kazi nzuri sana ambayo wanaifanya na kutekeleza wajibu wao ipasavyo, nawapongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, asubuhi ya leo mchango wangu utajielekeza katika maeneo matatu: usafiri wa anga ambapo mimi ni mdau mkubwa; Mamlaka ya Viwanja vya Ndege - TAA (Tanzania Airport Authority) pamoja na Mamlaka ya Udhibiti - TCAA (Tanzania Civil Aviation Authority). Kama muda utabakia basi nitazungumzia ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kimataifa cha standard gauge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuanze na usafiri wa anga. Nichukue tu fursa hii kumshukuru na kumpongeza sana Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la ATCL na timu yake kwa kazi nzuri sana wanayoifanya na kuandaa mpango mkakati wa muda mrefu wa kujiendesha. Naamini ukitekelezwa vizuri basi kutakuwepo na matunda mazuri ambayo yatazaliwa kutokana na mpango huo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina shauku kubwa sasa kuelewa, je, shirika hili lini hasa litaanza kujiendesha lenyewe? Narudia tena swali hilo kwa Mheshimiwa Waziri, lini shirika hili litapata uwezo wa kujiendesha lenyewe? Sio hilo tu, muda gani sasa itatuchukua kurudisha gharama za uwekezaji ambao umewekezwa na Serikali? Nalo hilo ni swali la pili ambalo napenda kujua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeshawahi kufanya kazi katika shirika hilo kwa muda wa miaka nane. Kwa kweli kipindi ambacho nilikuwa nafanya kazi, shirika hilo lilikuwa limegubikwa na ukata mkali, hata fedha ambazo ilikuwa tunapaswa sisi wafanyakazi kupelekewa katika Mifuko ya Hifadhi kama PPF zilikuwa haziendi kutokana na ukata huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuarifu kwamba sasa ukata huo na mwaka mmoja tu baada ya uwekezaji mambo yamekuwa mazuri zaidi. Sasa fedha zinapelekwa katika mifuko hiyo kwa wakati, shirika linaendesha mipango yake vizuri kabisa kwa maana ya kwamba linalipa kodi za Serikali na baadhi ya madeni ya shirika yamelipwa, kwa hiyo, hilo ni jambo jema sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna faida nyingi sana za kuboresha shirika hili la ndege. Faida ambazo zimepatikana ni pamoja na gharama nafuu za usafirishaji kwa kutumia anga na safari hivi sasa ni za uhakika kuliko ilivyokuwepo siku za nyuma. Kubwa zaidi ni kutengeneza ajira, tunategemea baada ya mwaka huu kumalizika shirika litakuwa limeajiri wafanyakazi takribani 600 ambapo hii ni utekelezaji wa moja kwa moja wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya 2015. Kwa hiyo, hili ni jambo jema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna tatizo kidogo pale la kulipwa marubani. Marubani sasa hivi katika shirika letu wanapokea mishahara ambayo ipo chini kidogo na soko la ajira la ndani lilivyo, hili linashusha kidogo morali yao. Kwa hiyo basi, ningemwomba Mheshimiwa Waziri angalau basi awaongezee mishahara marubani wetu angalau ikubaliane na soko la ajira ya ndani. Kwa hiyo, hilo litakuwa ni jambo zuri sana na wenzetu wale watapata motisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ilivyo sasa ni kwamba shirika au nchi kwa ujumla wake imepungukiwa na kada hii ya wafanyakazi (marubani) kwa sababu hakuna succession plan nzuri kati ya wale marubani ambao wanamaliza muda wao na wale ambao wanaajiriwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina taarifa kwamba kila shirika la ndege kwa maana ya waajiri kuna tozo la asilimia nne ambalo linakwenda kwenye programu ya SDL (Scheme Development Levy) ambapo sijui fedha hizi zinatumikaje au zimenufaisha marubani na ma-engineer wangapi. Kwa hiyo, napenda kujua manufaa ya hii SDL ambayo inatolewa na waajiri wote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala la viwanja vya ndege, Tanzania Airport Authority inasimamia viwanja 58. Kati ya hivyo vitatu tu ndiyo ambavyo vina manufaa kwa maana vinaweza kujiendesha vyenyewe, vilivyobakia vyote 55 haviwezi kujiendesha vyenyewe vinategemea faida ambayo inazalishwa na hivi viwanja vitatu ambavyo ni cha Mwanza, Arusha na Kilimanjaro nafikiri. Kwa hiyo, hii inapelekea mamlaka hiyo kupata fedha chache sana ya kuweza kutekeleza majukumu yake. Kwa hiyo… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. ABBAS ALI HASSAN MWINYI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.