Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Eng. James Fransis Mbatia

Sex

Male

Party

NCCR-Mageuzi

Constituent

Vunjo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Kwa heshima kubwa kabisa hili ni Bunge na tukishatamka Bunge Tukufu linatakiwa lioneshe utukufu wake.
Hii si sehemu ya matusi na ukisoma Zaburi 1:1 inasema “Heri watu wale wasiokwenda katika shauri la wasio haki, wala hawakusimama katika njia ya wakosaji, wala hawaketi barazani pa watu wenye mzaha.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi tukafanya Bunge hili ni sehemu ya mzaha wakati kuna issues serious za kitaifa za kuzungumza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli ukishaitwa Mbunge halafu unaleta matusi ya nguoni ndani ya Bunge, si jambo la heri kabisa kwa yeyote yule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwa heshima kubwa kabisa, sisi ni watu wazima, tuheshimiane, tusikilizane. Pia ukisoma Mithali 18:13 inasema:-

“Kujibu kabla ya kusikiliza ni upumbavu na jambo la aibu”

Mheshimiwa Mwenyekiti, kujibu kabla ya kusikiliza ni upumbavu na jambo la aibu na hii ni Mithali 18:13. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nijikite kwenye mchango wangu, baada ya kusema hayo, ni angalizo tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wahandisi katika Taifa letu wanafanya kazi nzuri na niwapongeze sana na hasa Mhandisi au Meneja wa TANROAD wa Mkoa wa Kilimanjaro, tunashirikiana naye vizuri, anafanya kazi vizuri na tunamtia moyo na tutaendelea kufanya naye kazi vizuri. Hata hivyo, niwatahadharishe tu Wahandisi kwamba taaluma ya uhandisi duniani leo ni taaluma shirikishi. Huwezi ukajiita mimi ni engineer kwamba basi ile taaluma yako huwezi ukashirikisha wengine la hasha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza na hilo kwa sababu ukiangalia adui mkubwa wa barabara leo hii ni maji; na mwaka jana nilisema tena namna gani Wizara hii inashirikiana na TAMISEMI na kutoa elimu ya kutosha namna ya uhifadhi mzuri wa barabara zetu na hasa kwenye suala la drainage system. Kwa sababu tunakubali Serikali haina fedha za kutosha kwa ajili ya maintenance ya barabara, sasa Local Government wanasafisha namna gani hii mitaro, kilimo cha matuta, mmomonyoko unavyotokea, maporomoko yanavyotokea barabara zetu zinaharibika kwa haraka sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Kilimanjaro uko kwenye mwinuko wa hali ya juu, hali ya barabara sio nzuri. Changamoto kwa wahandishi wetu, kwamba ni namna gani wanakuja na ubunifu mpya wa kupata material mpya ambayo inatumika kwenye hizi barabara badala ya kuweka kokoto zile zile au moram ya aina ile ile, lazima kuja na material nyingine labda moram mnachanganya na lime au moram mnachanganya na material mengine kwa ajili ya muda na uimara wa barabara zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijasahau kuna barabara moja tuliomba, barabara inayoenda Kilema Hospitali ambayo ni hospitali ya wilaya. Barabara hii inahudumia watu wengi, tunaomba ipewe nafasi. Milioni mia mbili ishirini iliyopewa barabara hii kusema ukweli na ina kilomita zaidi ya 13, hazitatosheleza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni zungumze suala la ujumla la miradi hii hasa sekta ya ujenzi. Nikizungumzia miradi ya Mkoa wa Dar es Salaam kwa mfano na Dodoma nayo imeshaambukizwa na majiji mengine. Ukiangalia Master Plan ya Mkoa wa Dar es Salaam, ukizungumzia magari yaendayo mwendo kasi, Dar es Salaam Rapid Transport (BRT). Mradi ule wa Reli wa Dar es Salaam, flyovers, suala la usafiri wa majini kutoka Dar es Salaam kwenda Bagamoyo, boti ya Bagamoyo sijui imeishia wapi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la barabara za kutoka Dar es Salaam – Chalinze – Morogoro ambapo watu wamevunjiwa nyumba zao. Benki ya Dunia imesitisha, hakuna fidia na maumivu ni makubwa. Mambo hayo ya kujenga mambo ya namna hii si mema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la upanuzi wa Julius Kambarage Nyerere International Airport, ring roads za kutawanya traffic katika Jiji la Dar es Salaam na miradi mingine mingi. Hainiingii akilini nikizungumza masuala ya majanga leo hii; mafuriko Dar es Salaam ni majanga makubwa lakini juzi tumeshuhudia pale Jangwani wanakoegesha au depot ya Dar es Salaam Rapid Transport. Serikali inawezaje ikasema watu watoke mabondeni na wao wakaenda wakawekeza pale? Future Plan iko wapi, UDA waliweza kujenga Ubungo walijenga Kurasini UDA wakati wa Mwalimu Nyerere.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamata walijenga kule barabara ya Nyerere lakini leo hii depot ya Jangwani mafuriko yaliyotokea juzi mradi huu mkubwa uliowekezwa pale, nguvu iliyowekezwa pale, investment iliyowekezwa pale, nani anawajibika kwa kushauri ujinga huo wa depot ya Dar es Salaam Rapid Transport? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema kwa pamoja kwa sababu zaidi ya asilimia 96 ya majanga ya dunia hii yanasababishwa na binadamu. Najua Wahandisi wengine wanafanya kazi vizuri tu; lakini wanasiasa wanaingilia Wahandisi, matamko ya kisiasa; huku wamenipa kura wasibomolewe na huku hawajanipa kura wabomolewe. Sasa mambo ya namna hii, Tanzania ni yetu sote, hatuwezi kuangamia kwa ajili ya kukosa maarifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia miradi hii ukisema ni ipi ya PPP, ukiangalia ni miradi ipi ya BOT ni investor gani ambaye ni makini serious investor atawekeza Dar es Salaam, huku kuna reli inayojengwa kwa standard gauge sawa tunaunga mkono itoke Dar es Salaam na isafirishe abiria kwa kasi kuleta Morogoro. Dar es Salaam Chalinze mradi huo, magari yaendayo kwa kasi, je, wanakaa pamoja na kuratibu miradi hii yote kwa pamoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii Dodoma imeanza tena, ukifika St. Gasper traffic imeanza, asubuhi na jioni, mvua ikinyesha Dodoma mafuriko yameanza area D na maeneo mengine. Sasa future plan yetu tuna design namna gani? Hii miradi return period yake tunaifanya kwa kiasi gani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema haya ni majanga na ni majanga makubwa kweli kweli. Kwa mfano, ukisoma ile taarifa ya CAG na hili ni janga la kitaifa, ni janga pia la 1.5 trillion. Ukichukua majimbo yote ya uchaguzi Tanzania yako 264 ukigawanya kwa kila kilomita moja ya lami ya shilingi milioni mia saba kila jimbo la uchaguzi lingepata zaidi ya kilomita 8.12 za lami nchi nzima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa haya ni vema tukayasimamia vizuri kwa sababu kashfa juu ya kashfa hakuna mwendelezo hakuna sustainability. Sasa sustainability haitakuwepo tukitoka kwenye ule mradi wa kutoka Dar es Salaam Bagamoyo Boat kashfa, sasa hivi kashfa nyingine ATCL, nayo tumeona matatizo yakijitokeza sasa hivi, kashfa juu ya kashfa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niseme tu, maandiko matakatifu yanasema watu wangu wanaangamia kwa kukosa maarifa. Haya tunayoyasema; Isack Newton anasema katika kila kani mkabala kuna kani mrejeo sawa na kinyume na anasema vile kwa sababu lazima kukubali mawazo mbadala tushirikiane vizuri, tufanye kazi vizuri, kwa kuwa Tanzania ni yetu sote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tusipokuwa makini tukafuta Katiba, tukafuata sheria, tukafuata taratibu, Bunge likajua nafasi yake, a democratic principle inayosema no taxation without representation. Ndiyo maana Wabunge tuko hapa kwa ajili ya kuisimamia na kuishauri Serikali, kuangalia kodi za Watanzania zinatumika vizuri la sivyo Bunge hili litakuja kuhukumiwa kwa nini haya yanatokea kwa kiasi hiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nimwombe Mheshimiwa Waziri, ukiangalia ule Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, lift pale tu ni tatizo lift. Wagonjwa wanatoka na ndege huko wananyanyuliwa na viti kana kwamba wananyanyuliwa kwenye machela wanawabeba mzoba mzoba. Watu wa nje wanatuonaje. Hilo lilinikumba mimi mwenyewe mwaka juzi tarehe 2 Disemba, mwaka juzi. Juzi tarehe 30 Ijumaa Kuu uwanja ule lift zilikuwa hazifanyi kazi. Yaani tunaonekana ni watu wa ajabu lift tu Uwanja wa Ndege wa Kimataifa hakuna.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa lazima tu-think dunia wanatuonaje. Waziri with due respect, kazi yote mnayoifanya ni kazi kubwa, miaka miwili mmepewa zaidi ya trilioni tisa katika miundombinu ya nchi hii, lakini ni namna gani tunaipa kipaumbele miradi yetu ya sekta ya ujenzi, mawasiliano na uchukuzi. Kupanga ni kuchagua, sasa sisi tunapanga vipi? Kama tunasema sungura ni mdogo, basi twende kwenye idea ya concept mpaka formalization.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe sana Serikali kwamba lazima tukubali taaluma za watu lazima ziheshimike. Pia naomba Wahandisi wasikate tamaa, waendelee kushauri vizuri na sisi wanasiasa tupate takwimu kutoka kwao ili tuweze tukazungumza na kuwasimamia vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana.