Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Bonnah Ladislaus Kamoli

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Segerea

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. BONNAH M. KALUWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwanza napenda nichukue nafasi hii kuipongeza sana Serikali kwa miradi mikubwa ambayo inaendelea ikiwemo kwenye Mkoa wangu wa Dar es Salaam na mikoa mingine. Hongera sana kwa Mheshimiwa Waziri pamoja na watendaji wote ambao wanatoka katika Wizara yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi hizo, nataka niongelee kuhusiana na TARURA. Asilimia 80 ya barabara ziko TARURA, lakini Mfuko wa Barabara unaipa TARURA asilimia 30. Tumekuwa na barabara mbovu ambazo haziwezi kutengenezwa, zinaishia tu kwenye kuandikwa na kuwekewa bajeti, matokeo yake hazitengenezwi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri na Wizara nzima waangalie ni jinsi gani watakavyoisaidia TARURA kwa sababu, wanavyoipa asilimia 30 hakuna kitu chochote ambacho kinaendelea. Kwa mfano, barabara zangu, barabara ya Airport, Mheshimiwa Waziri anajua kabisa ndege nyingi zinaletwa, tunaenda tunazindua na kila kitu lakini barabara ni mbovu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiwa unatoka Airport unaingia pale opposite na Airport barabara ambayo inakwenda Karakata Kipawa ni mbovu sana na kule watu wamejenga hoteli na vitu vingine ambavyo vingeweza kuongeza uchumi kwa wananchi wetu, lakini watu hawawezi kwenda kulala kule kwa sababu barabara zetu ni mbovu. Kwa hiyo, naomba sehemu ambazo wanaona kwamba zinaleta maendeleo at least zile sehemu ambazo wanaona ziko karibu na Airport basi mngeweza kuzifanyia mpango au strategy maalum kwa ajili ya kuzipendezesha ili watu wanaokuja hapa nchini kwetu wakitoka tu Airport sio wanakutana na barabara mbovu, wakutane na barabara nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine nataka kuongelea wananchi wangu wa Kata ya Kipawa, Mtaa wa Kipunguni na Magharibi. Nimeshafanya mikutano tofauti na Waheshimiwa Mawaziri wawili au watatu juu ya madai yao ya mwaka 1992, mimi bado niko shule, lakini mpaka sasa hivi hao wananchi hawajalipwa. Mheshimiwa Waziri kila siku namwambia kwamba wale wananchi wanaendelea kuwa maskini kwa sababu tangu wamefanyiwa tathmini mwaka 1992 mpaka leo hawajalipwa, wanakuja wanawalipa watatu, wanaondoka, wanakuja wanawalipa wanne wanaondoka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, wakati anakuja ku-wind up naomba aseme kwamba hao watu atawalipa au waendelee na shughuli zao zingine, kwa sababu kuwaweka wanavyowaweka, hawawaambii kama wanawalipa, hawawaambii kwamba waondoke, wapo tu kwenye njia panda hawajui kinachoendelea. Naomba sasa awaambie waendelee na shughuli zao kwa sababu mpaka sasa hivi kuna wengine wamekufa na wengine bado wanaendelea na wao wamesema kwamba watu wasijenge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine la tatu nataka niongelee kuhusiana na wananchi wangu aliowabomolea wale waliokuwa kandokando ya reli. Sheria inasema kwamba mjini ni mita 15, kijijini ni mita 30, lakini cha ajabu wananchi wa Kata za Kipawa, Buguruni na Ilala kwa Mheshimiwa Zungu wote wamekwenda kuwabomolea mita 60. Tunajua kwamba wanafanya maendeleo, wanataka treni ipite lakini sasa hawa wananchi wamebaki maskini. Hilo naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kufanya majumuisho anielezee hawa wananchi wangu watalipwa au hawalipwi ili sasa tujue kama tunaenda sehemu nyingine ili tuweze kupata msaada. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine niongelee kuhusiana na madaraja. Kuna madaraja ambayo yako mpaka kwa mpaka. Naongelea daraja la seminari yaani daraja linalounganisha Segerea pamoja na Kipawa. Hili daraja tangu mwaka 2012 baada ya mafuriko yale Mbunge akiwa Makongoro Mahanga mpaka leo halijawahi kutengenezwa. Kila siku namwambia Mheshimiwa Waziri hili daraja inaonekana utengenezaji wake kiwango chake cha pesa ni kikubwa, naomba walichukue TARURA kwa sababu Manispaa ya Ilala haiwezi kulitengeneza, haina uwezo. Sasa Mheshimiwa Waziri…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. BONNAH M. KALUWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.