Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Esther Lukago Midimu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia. Kwanza kabisa naipongeza Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi kwa kazi nzuri inazozifanya. Sisi Mkoa wa Simiyu katika majimbo yote tumeletewa gari za kubeba wagonjwa, hongera sana Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili nampongeza Mheshimiwa Ummy kwa kazi nzuri anazozifanya pamoja na Naibu Waziri, kwa kweli wanafanya kazi nzuri. Waheshimiwa Wabunge juzi juzi tu tumeshuhudia Serikali inakabidhi magodoro, vitanda pamoja na mashuka, hongera sana kwa Serikali kwa kazi nzuri inazozifanya.Pia Serikali yetu inajitahidi sana dawa kwenye hospitali zetu, asilimia 85 mpaka asilimia 90 ya dawa zinapatikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naishukuru Serikali yangu kwa kutuletea pesa za ujenzi wa hospitali ya mkoa, naishukuru sana. Serikali imetuletea pesa tumemudu kulipa eneo la hospitali ya mkoa, ni ekari 121, fidia tumelipa zaidi ya milioni mia mbili, ujenzi wa ground floor tumelipa zaidi ya milioni mia tano, ujenzi wa kumalizia ghorofa moja tumelipa zaidi ya bilioni moja, jumla kuu ya pesa tulizolipa zaidi ya bilioni mbili tulizotumia kwenye ujenzi. Naishukuru sana Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi, sasa hivi jengo la OPD limekamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana Serikali yangu; naiomba sasa iweze kutujengea wodi za wagonjwa. Wodi ya wazazi, wodi ya watoto na wodi ya akinamama. Hospitali ya mkoa bila wodi itakuwa bado haijakamilika, nashukuru sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hospitali teule ya mkoa haina gari la kubebea wagonjwa kuwapeleka Hospitali ya Rufaa ya Bugando. Tunaiomba Serikali itununulie gari la kubebea wagonjwa ituletee ili tuweze kupeleka wagonjwa katika Hospitali ya Rufaa Bugando na hospitali nyinginezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naiomba Serikali ituletee gari la mpango wa damu salama. Akinamama wengi wanapoteza damu kwa ajili ya kujifungua; inaweza ikanusuru akinamama pamoja na watoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hospitali yetu ya mkoa ina upungufu sana wa watumishi, tunaiomba Serikali ituletee watumishi. Watumishi waliopo katika hospitali ya mkoa ni watumishi asilimia 25, asilimia 75 hawapo. Tunaomba watuletee Madaktari Bingwa ili waweze kuhudumia na kukidhi mahitaji ya hospitali yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo moja baya linajitokeza katika nchi yetu, halifai kuigwa katika jamii na linaleta taswira mbaya katika nchi yetu. Jambo hilo ni ubakaji wa watoto wadogo wa miaka miwili. Watoto wadogo wanabakwa na baba zao, wajomba zao, pamoja na majirani kutokana na imani zao za kishirikina; inaumiza sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kipindi nilikuwa ziara nilienda wilaya fulani ambayo sitaitaja; kuna mtoto mdogo wa miaka mitatu alikuwa amebakwa akaharibiwa sana na ikabidi wampeleke rufaa Bugando. Naiomba Serikali ikemee hilo kwa nguvu zote ikiwezekana wanaofanya hivyo wanyongwe, hiyo itasaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni mimba za utotoni; sana sana zinatokea kwa maeneo ya wafugaji; naiomba Serikali iweze kudhibiti tatizo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru Serikali kwa kuanzisha Benki ya Wanawake, lengo ni kuwakomboa wanawake wote kiuchumi. Naiomba Serikali wakati Waziri anakuja kujibu hapa naomba aniambie benki hiyo ni lini itafika katika Mkoa wa Simiyu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa ya Mwenyekiti wa Bodi kupitia vyombo vya habari alisema kuna madeni hayalipiki, ni bilioni nane. Naomba Mheshimiwa Waziri akisimama aje atueleze hiyo bilioni nane imekwenda wapi na ni akina nani waliokopa ambao hawarudishi? Naiomba Serikali yangu ijitahidi sasa kukusanya yale madeni ya bilioni nane ili hizo pesa ziwafikie wananchi wa Mkoa wa Simiyu. Akinamama wa Mkoa wa Simiyu nao wana hamu ya kupata zile pesa za Benki ya Maendeleo ya Wanawake halafu na wanawake wa mikoa mingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi, niendelee kuipongeza Serikali yangu kwa kazi nzuri inazozifanya. Mwenyezi Mungu awabariki sana Mheshimiwa Rais na Waziri Mkuu kwa kazi nzuri wanayoifanya. Pia niwapongeze Mawaziri wote kwa ujumla wanajitahidi, wametembelea mikoa yetu pamoja na wilaya zetu wanafanya kazi nzuri, hongera sana, nawatia moyo, wachape kazi, wasonge mbele. Ahsanteni sana.