Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Mary Pius Chatanda

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Korogwe Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii nami niweze kuchangia katika hotuba aliyoitoa Mheshimiwa Waziri wa Afya, ndugu yangu, mdogo wangu Ummy Mwalimu. Kwanza nianze kwa kuunga mkono hotuba hii ni nzuri, vilevile niunge mkono mapendekezo yaliyotolewa na Kamati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi ya kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama ambavyo wenzangu wamezungumza kwamba anafanya kazi kubwa ya kuhakikisha Watanzania wanakuwa na afya bora. Nimpongeze Waziri, nimpongeze Naibu Waziri, nimpongeze Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu Ndugu yangu mpendwa Dkt. Chaula na Watendaji wote wa Wizara hii ya Afya kwa kazi kubwa na nzuri ambayo inaonekana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii Mheshimiwa Ummy nimpe salamu za wanawake wa Mkoa wa Tanga wanasema kwamba wanashukuru kwelikweli kwamba Rais alimteua kuwa kwenye nafasi hii ameitendea haki, amewatoa aibu wanawake wa Mkoa wa Tanga. Kwa
hiyo, wanaendelea kumwombea kwa Mwenyezi Mungu aendelee kutimiza majukumu yake hayo vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakuwa mchoyo wa fadhila kama sitashukuru kwa sababu sikuchangia katika ile Wizara ya TAMISEMI. Wizara ya TAMISEMI wamenipatia hospitali ya Wilaya ya Korogwe ambayo ilikuwa ni Korogwe Vijijini, nawashukuru sana. Wananchi wa Korogwe Mjini wanawashukuru kweli, lakini vile vile nitakuwa sijamtendea haki kaka yangu Profesa Maji Marefu kwa sababu sisi ni mapacha, kwa kumtengea fedha bilioni 1.5 ili aweze kujenga hospitali katika Halmashauri yake ya Korogwe Vijijini, tunaishukuru sana Serikali kwa moyo huo wa upendo mliotuonesha katika Wilaya yetu hiyo ya Korogwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba nimepewa hiyo hospitali naomba hospitali ile ni kuu kuu, nitaomba sasa nisaidiwe kupewa fedha kwa ajili ya ukarabati wa hospitali ile. Lile jengo la mbele Mheshimiwa Waziri Ummy Mwalimu analijua linavuja. Kwa hiyo, naomba wanisaidie fedha kwa ajili ya ukarabati pale watakapokuwa wametukabidhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, matamshi ya humu ndani hayatoshi, niiombe TAMISEMI sasa ituandikie rasmi kutukabidhi ile hospitali ili kuanzia tarehe moja mwezi wa Saba tuweze kuanza kuisimamia Korogwe Mjini. Nitashukuru sana utekelezaji huo utakapokuwa umekamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niipongeze Serikali kwa kuweza kuipatia fedha hospitali ya Muhimbili ambapo sasa imeweza kuanza kufanya kazi ya kutoa huduma ya upandikizaji wa figo. Hii imesaidia sana kupunguza gharama za kwenda kutibiwa nje hasa ikizingatiwa hata kwenye taarifa ya CAG imeonesha kwamba tumepeleka wagonjwa wengi India kwenda kwenye matibabu na gharama imekuwa kubwa, lakini kwa utaratibu huu ambao sasa hospitali ya Muhimbili imeanza ya kupandikiza figo, itatupunguzia sana kupeleka wagonjwa nje na gharama zitapungua. (Makofi)

Mheshimishiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Dkt. Janabi kwa kazi kubwa anayoifanya na wenzake katika hospitali ile, kile kitengo cha Moyo cha Jakaya Kikwete. Niiombe Serikali, naungana na Kamati kwamba zile bilioni mbili walizokuwa wametengewa tunaomba wawape fedha hizo ili waweze kununua hivyo vifaa tiba, tusipofanya hivyo maana yake tunataka hawa watu sasa wasiendelee kufanya kazi nzuri ambayo tayari imeanza kufanyika. Shida iko wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hospitali ile inatusaidia kupunguza gharama za kwenda nje. Sasa kama waliomba bilioni mbili inashindikana kuwapa ni kwa nini? Naomba Serikali hebu iwatazameni katika hili, wapewe hizo bilioni mbili ili waweze kununua hivyo vifaa tiba waweze kufanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nizungumzie suala la Chuo cha Uuguzi pale Korogwe. Jambo hili limechukua muda mrefu sana. Chuo cha Uuguzi Korogwe jengo hili limejengwa lina miaka sasa 15 halijawahi kutengewa fedha za kumalizia jengo lile. Mheshimiwa Waziri naomba mniambie leo, kulikoni jengo lile limejengwa mpaka kufikia ile hatua ya kutaka kuanza kupauliwa halitengewi fedha. Fedha na kodi za wananchi zimepotea pale maana yake lile jengo lisipomaliziwa, likianza kuchakaa tutaingia gharama nyingine ya kuanza kutenga fedha kwa ajili ya jengo lile pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe mdogo wangu Mheshimiwa Ummy alifika aliliona lile jengo, kile chuo kiko pale, watoto wako pale wanasoma, lakini kwa bahati mbaya sana majengo ya utawala hayapo, wamechukua madarasa ya wanafunzi wameweka partition zimekuwa ndio ofisi za Walimu, halafu watoto wanaenda kusomea kwenye bwalo la chakula, haiwezekani. Napata mashaka kwa nini fedha haitengwi, inawezekana kwa kipindi hicho ulikuwa ni uchochoro wa kupitisha fedha zile kwenda kuliwa, kama siyo kwa nini fedha hazitengwi kwa ajili ya jengo lile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaomba majibu ya kunitosheleza hapa kwa sababu nimeona kwenye kitabu hapa wamezungumzia mipango yao, wamesema wataboresha vyuo vya afya ili kuendeleza uzalishaji wa wataalam, wakavitaja hapo. Sijaona kuzungumzia Chuo cha Uuguzi Korogwe, kuna nini? Mheshimiwa Ummy mdogo wangu nampenda kweli kweli na mimi ndiye mpiganaji wake kwa kura za maoni Mkoa wa Tanga. Katika hili hatutaelewana. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru na naunga mkono hoja.