Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Stanslaus Shing'oma Mabula

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nyamagana

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami naomba nitumie fursa hii kukushukuru na kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kupata nafasi ya kuchangia Wizara hii muhimu kwa ajili ya maisha ya Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli kwamba kazi kubwa inayofanywa na sekta hii au Wizara hii ya Afya inasaidia sana katika kuhakikisha Watanzania wanaendelea kuwa na afya bora, lakini watoto ambao wanazaliwa na wenyewe pia wanazaliwa kwenye mazingira mazuri yanayowafanya na wao wawe watu ambao mwisho wa siku watakuwa sehemu ya watu wa kutegemewa kwenye Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumze mambo manne peke yake. Kwanza nizungumze juu ya upatikanaji wa madawa. Sote tunafahamu Serikali imefanya jitihada kubwa sana hasa katika suala zima la upatikanaji wa dawa. Taarifa iliyosomwa hapa na Mheshimiwa Waziri pia na Kamati inaonesha tumekwenda karibu asilimia 89 kwa mwaka 2017/2018, hii ni hatua moja kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Waziri, bado liko tatizo kule kwenye jamii. Watu wengi sana hawaelewi hizi dawa muhimu tunazozizungumza ni zipi, lakini dawa ambayo inapatikana kwenye zahanati, dawa ambayo inapatikana hospitali ya Wilaya unaweza usiipate kwenye kituo cha afya au kwenye zahanati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niiombe Wizara ichukue jambo hili kama sehemu ya utatuzi na elimu kwa jamii, itengeneze utaratibu kuanzia ngazi ya zahanati, ieleweke mtu anayekwenda kwenye zahanati ziko dawa za aina gani atakazozipata, akiwa kituo cha afya atapata dawa ya aina gani na hospitali ya Wilaya atapata dawa ya aina gani, kwa sababu hili linatukumba hata sisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwananchi anaweza kupiga simu yuko kwenye kituo cha afya anasema dawa hii hakuna, lakini ukweli ni kwamba dawa ile wakati ule pale alipo siyo sehemu yake. Sasa hii lazima tujitahidi sana kutoa elimu ya kutosha ili muweze kutusaidia tuepuke matatizo mengi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu juhudi kubwa zinazofanya na Serikali bila kuangalia motisha au haki za watumishi kule waliko na wanazozitegemea na zingine siyo kubwa sana Mheshimiwa Waziri. Kwa mfano, nimwombe sana, zile allowance za uniform zinazopatikana kwa mwaka pia allowance za likizo zao, lakini pia on call allowance, haya ni mambo ambayo yatatusaidia kuboresha zaidi huduma zetu za kiafya hasa kwa watumishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa watumishi ni wengi sana lakini pamoja na kazi kubwa wanayoifanya Mheshimiwa Waziri tunaamini kabisa kwamba tukiwatazama na wao kwa jicho jingine kwamba ni sehemu yetu na kazi hii ni kazi ya wito. Kazi ya wito ukipata stahiki zako ambazo ziko kwa mujibu wa sheria na wewe utaifanya kwa malengo yale yale uliyojiwekea na utakuwa umepiga hatua sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mheshimiwa Waziri, kwenye hotuba yake ameonesha moja ya kipaumbele ni kuhakikisha anaboresha miundombinu ya hospitali. Mheshimiwa Waziri hili ni jambo kubwa sana, miundombinu ya hospitali zetu nyingi kwa muda mrefu imekuwa siyo rafiki lakini kwa sasa amejitahidi sana kwa kufanya jambo hili. Hapa nazungumzia kuanzia kwenye ngazi ya zahanati, ngazi ya vituo vya afya lakini hospitali za Wilaya na hospitali za Rufaa za Mikoa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwanza Jimbo langu la Nyamagana ndipo ilipo hospitali ya Rufaa ya Mkoa hospitali ya Sekou Toure, lakini ndipo ambapo nina hospitali ya Wilaya ya Nyamagana ambayo iko Butimba. Nikianza na hospitali yetu ya Sekou Toure, hospitali hii imekuwa ni hospitali tegemeo lakini imekuwa ni hospitali kubwa ya muda mrefu na nimshukuru sana ameiangalia kwa muda mfupi aliokuwepo hospitali yetu kwa sasa imekuwa bora sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hospitali hizi haziwezi zikaboreka bila kuangalia umuhimu wa watu ambao wamefanya kazi kwenye maeneo haya. Nitumie nafasi hii nimpongeze sana ndugu yangu na rafiki yangu Dkt. Leonard Subi ambaye amekuwa RMO pale, lakini nimpongeze Katibu wake Ndugu Temba. Niwapongeze na Waganga wafawidhi mama yangu Onesmo ambaye leo ni mstaafu lakini dada yangu Bahati Msaki ambaye sasa anashikilia nafasi ile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bila kuficha ni kwamba hospitali hizi pamoja na wataalam tulionao bila kutumia weledi wao na ubora na moyo wao wa dhati wa kujitoa mazingira ya hospitali haya hayawezi kubadilika. Leo ukienda hospitali ya Sekou Toure ni sawa unazungumza hospitali tofauti kabisa na ilivyokuwa miaka mitatu huko nyuma iliyopita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni pongezi kubwa kwa watumishi wote, lakini jitihada zinazofanywa na Serikali na utashi wa watu wenyewe waliopewa jukumu hili na nimeambia Dkt. Subi amepanda daraja kidogo. Nimpongeze sana kwa sababu jitihada alizozifanya Sekou Toure anastahili na sifa hiyo anastahili kwenda hapo alipo leo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na maboresho makubwa haya ya hospitali ya Sekou Toure ambayo kwa kweli ni hospitali ya Kanda ya Kimkoa, tunaitegema kwa nguvu nyingi, nimwombe sana liko jambo moja pamoja na ubora huu hospitali hii haina CT Scan. Sote tunafahamu tukiongeza CT Scan kwa sasa, mapato yaliyoongezeka kutoka shilingi milioni 30 kwa mwezi mpaka milioni 120, leo ukiongeza CT Scan utakuwa umeiongezea uwezo mkubwa lakini kingine tuongeze Madaktari bingwa kushughulika matatizo ya kibingwa ili wawepo kwa wingi waweze kusaidia umma wa watu zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni sambamba na jengo tunalolijenga sasa hivi kwenye hospitali ye Sekou Toure, nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri tumepata bilioni moja kwa mwaka huu, imefanya kazi kubwa na Mkoa wa Mwanza ni moja kati ya mikoa nane ambayo kwa kweli imetajwa katika matatizo ya vifo vya mama na mtoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kukamilika kwa jengo hili kwa wakati itakuwa imetusaidia sana kuhakikisha kwamba vifo vya mama na mtoto ambao ni sehemu ya kipaumbele cha Mheshimiwa Waziri, atakuwa ametusaidia lakini atakuwa amesaidia akinamama wa Mkoa wa Mwanza na wale wa mikoa ya jirani kuja kupata huduma hizi kwa kiwango cha hali ya juu, tukiamini mpango huu wa malipo kwa ufanisi utakuwa na tija na utatoa matunda ambayo ni stahiki sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumze juu ya habari ya uboreshaji wa huduma za afya kwenye hospitali zetu za Wilaya. Tunayo hospitali yetu ya Wilaya ya Nyamagana. Hospitali hii ilianza miaka mingi ikiwa kama zahanati ikapandishwa daraja kuwa kituo cha afya na sasa ni hospitali ya Wilaya. Ukweli usiofichika nirudie tena kusema Watumishi hawa Madaktari, Wauguzi na Wakunga wanafanya kazi kubwa sana. Hospitali hii miaka miwili iliyopita kabla hatujawa na dawa za uhakika, kabla hatujawa na uhakika wa kukabiliana na kushughulika na matatizo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)