Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Oliver Daniel Semuguruka

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi hii ili niweze kuchangia katika Wizara ya Afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniweza kusimama katika Bunge lako Tukufu, siyo kwa uwezo wangu bali ni kwa uwezo wake. Nampongeza Rais wetu mpendwa wa Jamhuri ya Muungano Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri anazofanya za kujenga Taifa letu, binafsi namuombea kwa Mwenyezi Mungu azidi kumtia nguvu ili aendelee kulijenga Taifa letu na sisi tuko nyuma yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nampongeza Makamu wa Rais Mama Samia Hassan Suluhu na Waziri Mkuu Kasim Majaliwa na Mawaziri wote, Naibu Mawaziri kwa kazi nzuri wanazozifanya kwa moyo wa dhati wa kujenga Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nimpongeze dada yangu mpenzi Mheshimiwa Ummy Mwalimu na Mheshimiwa Dkt. Ndungulile kwa kazi nzuri wanazozifanya katika kitengo cha afya. Sasa naomba nijielekeze moja kwa moja katika mchango wangu katika Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa, naishukuru Serikali kwa mwaka wa fedha 2017/2018 kwa kutenga bilioni 3.5 kwa ajili ya ukarabati wa vituo vya afya vya Mkoa wa

Kagera. Pamoja na kazi nzuri zinazofanywa kwa upande wa afya, napenda kusemea wafanyakazi wa Murugwanza Wilaya ya Ngara, wafanyakazi 17 ambao hawajaingizwa kwenye payroll licha ya kuombewa kibali Wizarani na hupelekea kupata mishahara yao kwa shida. Naomba sana Wizara ya Afya pamoja na Serikali iweze kuwaona hawa watu ambao wanafanya kazi kwa moyo wao wote lakini hawajaingiziwa majina yao kwenye payroll mpaka muda huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanapata shida sana na ikumbuke kwamba wanazo familia, wana watoto wanaowasomesha na mambo yao binafsi kwa ajili ya kupata fedha ili waweze kujikimu, lakini mpaka muda huu hawajaweza kupata mishahara wanadai zaidi ya muda mrefu sana hata wakipata mshahara wanaweza kupata mshahara wa mwezi mmoja miezi miwili, ambayo haikidhi mahitaji yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna wafanyakazi 49 walitolewa kwenye payroll na baadaye wakarudishwa wako chini ya Dayosisi ambao wanalipwa na Wizara, walivyorudishwa kwenye payroll hadi leo kuna arrears zao wanadai, ambapo kuna mtumishi anadai miezi kumi miezi sita, miezi mitano, hiyo pia inaleta shida sana katika kufanya kazi. Watu hawa wako kwenye kitengo ambacho ni mahsusi lakini mtu unakuta ameshindwa hajapata mshahara zaidi ya miezi kumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli naomba Wizara iweze kuwaangalia hasa dada yangu mpenzi Mheshimiwa Ummy Mwalimu, najua ana moyo sana wa upendo hebu naomba aangalie Wilaya yangu ya Ngara jamani, hawa watu waweze kusaidiwa. Mheshimiwa Dkt. Ndungulile nilishamlilia sana nilishamwona uso kwa uso nikamwelezea kuhusu hawa watu lakini bado hawajapata mishahara yao, naomba sana waangalie kwa jicho la huruma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vituo vya afya katika Wilaya ya Ngara tuna upungufu wa watumishi kwa asilimia 67, jambo linalotatiza huduma za afya. Hebu imagine asilimia 67 vituo vya afya hamna watumishi. Unaweza ukaenda kituoni ukakuta kuna Mganga mmoja huyu ndiyo receptionist, huyo ndiyo aangalie wazazi, huyo ndiyo angalie watoto na kila kitu. Jamani Wizara ya afya naomba watuangalie sana Wilaya ya Ngara, tuko mpakani mwa Rwanda na Burundi lakini tuko Tanzania, tunaomba watuangalie inawezekana wameshatusahau lakini tunaomba watuangalie kwa jicho la huruma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba kuongelea Watumishi wa Afya kutolipwa stahiki zao kwa muda mrefu kama vile on call allowance na malimbikizo ya mishahara, likizo na matibabu. Unakuta wafanyakazi wanafanya kazi kwa muda mrefu bado hawajapata stahiki zao, dada yangu Mheshimiwa Ummy Mwalimu Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee na Watoto yaani mimi nakufa na yeye kwa sababu najua ni dada wa upendo nina imani ataweza kunisaidia huko ili tuweze kuwasaidia hawa ndugu zetu waweze kupata mishahara yao kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hospitali ya Nyamiaga inayomilikiwa na Serikali kwa asilimia 100, hiyo hospitali wodi ya wajawazito kuna vitanda vichache, unakuta wajawazito wanalala watatu hadi watano katika kitanda kimoja. Imagine, dada yangu Ummy ni mzazi kama mimi, wakati mwingine uchungu unakushika, unaenda kushika tumbo kumbe unashika la mwenzako, unaenda kushika mgongo unashika wa mwenzako, mmelala kitanda watu mko watatu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri aangalie hili, tupate angalau vitanda vya kutosheleza katika hospitali yetu ya Nyamiaga ambayo iko chini ya Serikali asilimia 100. Tunaweza tukasemea Murugwanza lakini Murugwanza iko chini ya Dayosisi na tuna watumishi wetu wa Serikali lakini Nyamiaga ni ya Serikali asilimia 100, lakini wagonjwa wanapata shida sana hasa akinamama wajawazito.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni mama nawawakilisha akinamama inaniuma sana, ninapokwenda nakuta akinamama wamelala watatu, watano kitanda kimoja na ile habari dada Ummy unaifahamu jinsi inavyouma, yaani sijui nisemeje, Mheshimiwa Dkt. Faustine Ndungulile naweza nikamwacha pembeni kwa sababu hajui uchungu wa akinamama tunaoupata wakati wa kujifungua. Kwa hiyo, naomba kwa kweli watuangalie kwa jicho la huruma sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo zahanati ya Kijiji cha Ishozi, Wilaya ya Misenyi iliangushwa wakati wa tetemeko la ardhi mpaka leo ukarabati wa zahanati hiyo haujaweza kufanyika ipasavyo. Naomba Serikali iweze kufanya ukarabati wa kutosha ili wale wananchi wa Ishozi kule Misenyi waweze kupata matibabu ya kutosha especially wazee, kuna watoto kuna akinamama, lakini hawapati huduma ile kutokana na kutokukarabatiwa kwa yale majengo yaliyoanguka kwa tetemeko. Sisi wa Mkoa wa Kagera hatukuliita tetemeko, lilikuja tu kwa bahati mbaya. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri na Wizara husika iweze kutusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa haina hospitali ya Wilaya. Ile hospitali ina watu wengi sana pale Kyerwa kuna zaidi ya wananchi laki tatu, wote tunatuma kituo cha Kyerwa, naomba Serikali ituangalie kwa jicho la huruma tuweze kupata hospitali ya Wilaya katika Wilaya ya Kyerwa ili wananchi waweze kupata matibabu pasipo shida. Mheshimiwa dada yangu Ummy Mwalimu naomba anisikilize kwa makini sana na Mheshimiwa Dkt. Ndungulile nisije nikashika shilingi. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hospitali zote za Wilaya za Mkoa wa Kagera zina upungufu wa watumishi, kwa kweli tuna shida sana, kila Wilaya, kila zahanati kuna shida ya upungufu wa watumishi. Kipindi wanafanya uhakiki wa vyeti watu waliondoka wengi. Mheshimiwa baba yangu Mzee Mkuchika alishasema uhakiki ulishapita, sasa kwa nini wasiajiri watu wa kutosha katika hospitali zetu ili wazee, mama zangu, watoto, baba zangu waweze kupata huduma. Naomba sana watuangalie sana kwa jicho la huruma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri za Manispaa za ya Bukoba na Muleba tayari zimeanza kujenga vituo vya afya. Je, ni lini Serikali au ina mpango gani wa kutenga pesa ili kuweza kusaidia hizi Halmashauri zikamilishe ujenzi wa vituo vile vya afya? Kwa sababu wananchi walishajitolea kwa moyo wao, tumejitolea kama wananchi kujenga vituo vya afya lakini havijakamilika, wanatusaidiaje ili tuweze kukamilisha vituo vile?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wetu wa Kagera tuna visiwa 25 ambavyo vinakaliwa na wananchi, lakini visiwa vyote hivyo vina zahanati tano tu, katika zile zahanati...

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE.OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.