Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora

Hon. Ahmed Mabukhut Shabiby

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Gairo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora

MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii. Kwanza, nianze kumpongeza Mheshimiwa Mawaziri wote wawili pamoja na Naibu Mawaziri wao na Katibu Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nataka kujikita kwenye Jimbo langu na hasa kwenye Kituo cha Afya cha Gairo kwa sababu Gairo ni Wilaya lakini bado haina hospitali ya Wilaya. Namshukuru sana Mheshimiwa Waziri baada ya kufika Gairo na kuona kwamba kile kituo cha afya kina umuhimu sana na kiko katikati ya barabara ya Morogoro Dodoma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kituo kile kinapokea majeruhi wengi sana na wagonjwa wengi kutoka Wilaya ya Kongwa ambayo imepakana nayo, Wilaya ya Kilindi pamoja na Wilaya ya Kiteto. Kituo kile kimekuwa ndiyo sehemu yao ya hospitali yao ya rufaa pamoja na kuwa ni kituo cha afya. Namshukuru pia kwa kutupa pesa milioni 400 kwa ajili ya kujenga majengo ya operesheni na mambo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna tatizo moja cha ajabu sijui huku TAMISEMI kwa hawa Wakurugenzi wa hizi Idara nini wanafikiria, nini wanafanya na wanaangalia kwa vigezo gani kugawa watumishi kwenye wilaya, bado sipati jibu, leo nimeheshimu tu, lakini siku nyingine kwa kweli hatutoelewana hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, Mheshimiwa Waziri anajitahidi, lakini Wilaya ya Gairo kituo hicho cha afya na Wilaya nzima wametuletea mwezi wa Novemba mwaka jana Wauguzi Wasaidizi watatu, wakati upungufu ni zaidi ya Wauguzi 70. Wametuletea Matabibu wametuambia ni Matabibu baada ya kuwachunguza kumbe ni Matabibu Wasaidizi, tumewarudisha huko watubadilishie mpaka leo hakuna kibali cha kubadilisha ili waajiriwe. Kwa hiyo, ina maana hatukupata mtumishi yoyote kwenye kituo cha afya cha Gairo na Wilaya nzima ya Gairo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna mpango wa kufungua vituo vya afya vitano, lakini hatuna Matabibu wala hatuna Wauguzi. Ukija kwa wale Madaktari pale ni sehemu ya barabarani nimesema ile ndiyo ‘Tumbi’ ya Dodoma - Morogoro kwa sababu mtu yoyote akipata matatizo na ukiangalia hata idadi ukisoma ya accident nyingi zinazotokea katika maeneo yale, Madaktari wenyewe operesheni na Madaktari wengine tunahitaji zaidi ya wanne au watano lakini hatujapata hata mmoja. Sasa sielewi ni nini kinachofanyika hapa kwenye hizi Idara zenu za TAMISEMI. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukija hata watumishi katika Halmashauri ya Gairo; ukienda uhasibu hakuna watumishi wa daraja la pili, halafu leo tukipata hati chafu watatufungia hiyo Halmashauri kama alivyozungumza Waziri Mkuu? Haiwezekani kwa sababu watumishi Wahasibu hawapo! Utumishi kwenyewe hamna kitu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru dada yangu hapa Waziri wa Afya, Mheshimiwa Ummy Mwalimu ametupatia gari la wagonjwa, Wilaya ile haina kabisa magari ya wagonjwa. Bahati mbaya ina Tarafa nyingine kutoka Gairo ni kilometa 100 inaitwa Tarafa ya Nongwe, hii Tarafa milima yake ni kuliko milima ya Lushoto, nako wanahitaji gari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo gari lililoletwa na Wizara ya Afya nalo halina Madereva. Halmashauri imeomba kuajiri Madereva watano lakini kutoka Wizara ya Utumishi hakuna kibali mpaka leo. Kwa hiyo sasa mnataka hiyo gari aendeshe Mbunge? Matatizo tupu! Naomba sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Walimu shule za Msingi wale wengine wenye vyeti feki wameondoka wengi na mwaka huu wanastaafu Walimu 50 na sasa hivi pana upungufu wa Walimu zaidi ya 270. Kwa hiyo, shule za msingi utakuta kuna shule sasa hivi ina Walimu wawili ama Mwalimu mmoja. Sasa ndugu zangu wa TAMISEMI sielewi ni vigezo gani wanavyotumia kutafuta hawa watumishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala lingine, wakati tunatoka Wilaya ya Kilosa kugawanya kuwa Wilaya mbili tuliangalia ukubwa wa eneo Wilaya ya Kilosa ilikuwa na Tarafa saba, tukakubaliana kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa kwamba ianzishwe Wilaya ya Gairo kuwa na Tarafa tatu, Tarafa ya Nongwe, Tarafa ya Gairo na Tarafa ya Magole.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ikatokea baada ya ile Wilaya kuanzishwa uchaguzi wa 2010 ulishafanyika, kwa hiyo Mheshimiwa Rais aliyepita akasema sasa itabidi kwa sababu huku wamechagua Mbunge na huku nako wameshachagua Mbunge kwa hiyo NEC wametuambia baada ya zoezi hili likishapita wakati wa uchaguzi 2015, ile Tarafa ya Magole irudi Wilaya ya Gairo kama ilivyoamuliwa hapo mwanzo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, 2015 ile Tarafa haijarudishwa, kwa hiyo utashangaa wa pale Gairo ukitoka kilometa sita unakuta tena kijiji kipo Wilaya ya Kilosa, Berega yote, Kiegeya yote hata pale wanakouza viazi kwa mbele pako Wilaya ya Kilosa, kwa hiyo wanawatesa wananchi bila sababu. Wale Wapinzani sasa wameingia na majungu wanasema kwamba Mbunge wa Gairo hawapendi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna lingine liko kwenye Utumishi; hili lazima tulizungumze wazi mimi ni Mbunge wa CCM na nimepitia kwenye ngazi nyingi nimekuwa Kamanda, nimekuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa, nimekuwa Mbunge miaka mingi sana kwenye hiki Chama. Sasa hivi kuna watu kwenye ofisi za Serikali huku kwenye utumishi wanatafuta mbinu ya kujifanya watu wanafanya kazi zao lakini kuichafua Chama cha Mapinduzi na kuchafua Viongozi wa Chama cha Mapinduzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, Kijana yule Abdul Nondo ana umaarufu gani mpaka wamwite kwa kutumia vyombo vya habari, hawawezi kufanya investigation, wafanye investigation, wamwandikie barua anaitwa, lakini hapo ni kutaka kuichafua tu wanataka kuichafua Serikali ya CCM kwamba aambiwe yule kuna mbinu ya aina yoyote anatafutiwa, ana umaarufu gani mpaka yule mtu wa Immigration aende akakae anaanza anataka cheti cha bibi, cheti cha mjomba, cheti cha babu mpaka aandike kwenye vyombo vya habari? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunawapa watu umaarufu wakati kesi iko Mahakamani mtu anapatikana, kuna watu wengine watatumia ile kusema mmeona sasa, Serikali ya CCM ikimtaka mtu inaanza kumwambia siyo raia, wakati siyo kweli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba kwenye utumishi waambieni watu wenu, televisheni kila mtu anaipenda, lakini uwe na mambo ya maana ndiyo uende ukajiangalie kwenye televisheni. Sasa itakuwa basi kila mtu akitaka kitu anatoa taarifa kwenye televisheni au kwenye mitandao siyo sawa! Wanachafua Serikali yetu wakati hakuna mtu mwenye habari na mtu mdogo kama yule. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana kwenye utumishi tuangalie haya masuala, mnayaona ya kawaida lakini kuwapa watu maneno na mambo mengine ya kuongea au watu kufikiria au kuwasababisha watu wajue kwamba Serikali inamtafuta yule kijana, wakati Serikali nina uhakika kabisa haina mpango na mtu mdogo kama yule kwa sababu hana madhara yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hayo ndiyo yangu, ahsanteni sana.