Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Mungano na Mazingira kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Kangi Alphaxard Lugola

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mwibara

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Mungano na Mazingira kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS,MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kunipa nafasi niweze kuchangia na kutoa baadhi ya ufafanuzi kwenye hoja ambazo Kamati zote mbili pamoja na Wabunge wameweza kuziwasilisha. Kwanza kabisa nianze kuunga mkono hoja ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa namsikiliza Mheshimiwa Kigwangalla Dkt. na Mheshimiwa Sware Dkt. wanatunishiana misuli ya kiudokta kwenye suala la Stiegler’s Gorge, sasa nikasema mimi ambaye ni Naibu Waziri wa mambo haya ya mazingira nikiingia hapo nafikiri tutaelewana vizuri. Hata hivyo, namshukuru Dkt. Kigwangallla amemaliza masuala yote ya Stiegler’s Gorge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri wangu mtoto wa baba January namshukuru kwa sababu tangu alivyonipokea kwenye Ofisi ya Makamu wa Rais amekuwa msaada mkubwa sana na hivyo kunifanya niweze kukimbia haraka katika kumsaidia masuala haya ya mazingira katika nchi yetu. Kwa hiyo, Mheshimiwa mtoto wa Mzee Makamba, nakushukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwashukuru Katibu Mkuu wa Wizara yetu, Ofisi ya Makamu wa Rais, Jemedali Engineer Joseph Malongo na Naibu Waziri Mwanasheria Butamo wamenisaidia sana katika kuhakikisha kwamba nafanya shughuli hizi za mazingira kwa raha mustarehe kwa sababu kila nilichokuwa nikiwaelekeza wamekuwa wakitekeleza ninachokihitaji wamekuwa wakifanya hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niwashukuru wafanyakazi wote, Ofisi ya Makamu wa Rais namna ambavyo wamekuwa nami muda wote katika kunipa msaada na kuweza kupata uzoefu kwenye Ofisi ya Makamu wa Rais. Vile vile nimshukuru sana Dkt. Makotha ambaye ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NEMC pamoja na timu yake wamekuwa wakifanya kazi nzuri kazi ambayo imetukuka, wamekuwa watu wa msaada sana katika kunifanya mimi niweze kutekeleza majukumu yangu pasipo wasiwasi wala vikwazo vyovyote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ambazo zimeibuliwa na Kamati zipo nyingi, lakini wamejikita katika kutushauri. Naomba kupitia Bunge lako Tukufu kuwaondolea wasiwasi Wajumbe wote chini ya Mwenyekiti Saddiq na Makamu wake Bashungwa kwamba yale yote ambayo wametushauri juu ya mazingira tutayafanyia kazi na nitagusia machache juu ya mazingira na nitagusia machache ambayo wameyasisitiza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia wako Wabunge wengi ambao wamechangia kwa maandishi kwenye masuala ya mazingira na pia wamechangia kwa kusema hapa Bungeni kwa sababu ya muda nitakwenda kugusia masuala machache ambayo yamewasilishwa katika Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaanza kufafanua hizi hoja, kwa nafasi ya pekee nimshukuru Mheshimiwa Rais ambaye aliniteuwa na hii ni bajeti yangu ya kwanza na Mheshimiwa Rais ameendelea kuniamini nami namuahidi kwamba sitamwangusha, nitaendelea kuifanya kazi hii katika kasi yake ya hapa kazi tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa pia niendelee kumtia moyo Mheshimiwa Rais kwamba baadhi ya Watanzania wenzetu na baadhi ya Wabunge wenzetu humu ndani wamekuwa wakimkebehi na kumkejeli kwamba Rais huyu amekuja na mambo ambayo sasa Taifa hili linaenda kuangamia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo haya ni ya upotoshaji na siyo ya kweli. Kati ya Rais ambaye katika bara la Afrika na duniani kote ambaye amejibainisha kwamba sasa atakwenda kulinda kwa nguvu zote rasilimali za Watanzania ni Rais Dkt. John Pombe Magufuli, Rais Dkt. John Pombe Magufuli ni miongoni mwa Marais ambao hawazaliwi mara kwa mara na hawapatikani kila mahali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais anapokuwa anawaambia Watanzania kwamba katika shughuli zetu hizi tumtangulize Mungu mbele, wananchi wengi wanashindwa kuelewa maana yake ni nini. Maana yake ni kwamba Rais Dkt. Magufuli ni chaguo la Mungu na ndiyo maana anapotamka maneno hayo Mungu anamwambia kwamba hapo hapo uliposhikilia hapo usibadilishe gia endelea kulitetea Taifa la Watanzania na ndiyo maana.

T A A R I F A . . .

NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Gekul namheshimu sana, lakini napenda nimkumbushe kwamba hii kazi niyayofanya hapa nimeteuliwa na Rais na nafanya kazi ya Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama yeye hataki kusikia maneno ambayo nayasema juu ya aliyeniteua, basi avute subira pale ambapo vizazi vinavyokuja inawezekana na wenyewe wakawa Rais ambao watampatia majukumu ili aweze kuwazungumzia. Hata hivyo, nimhakikishie kwamba yeye na chama chake kuingia madarakani ni vigumu sana.

Na ni rahisi sana ngamia kupenya kwenye tundu la sitando. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze sasa kujibu hoja za Wabunge najua wana kiu ya kusikiliza. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wabunge wengi kwa kusema hapa na kuchangia kwa maandishi wamezungumzia kwa uchungu sana juu ya uchafuzi na uharibu mkubwa unaofanyika kwenye vyanzo vya maji. Vyanzo vya maji katika nchi yetu vina uhusiano mkubwa sana na maisha yetu na uhai wetu. Pia vyanzo hivi vya maji vina uhusiano mkubwa sana ndoto ya Mhesimiwa Rais ya Tanzania ya viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili tuweze kuwa na viwanda lazima tuwe na umeme wa uhakika; ili tuwe na umeme wa uhakika lazima tulinde vyanzo vya maji kwa gharama zote na kwa nguvu zote. Ndiyo maana katika nchi yetu vyanzo vya maji ambavyo vinazalisha umeme kwa kutumia maji tuna Kihansi, Kidatu, Mtera, Maporomoko ya Pangani, Hale, Nyumba ya Mungu, Uwemba, Tulila, Mwenga, Darakuta pamoja na Iyovi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi yote hii wanazalisha kwa ujumla megawatt 560.6, kwa kuwa sasa tunakwenda kuwa na mradi mkubwa huu wa Stiegler’s Gorge ambao utazalisha megawatt 2100. Maana yake ni nini kwenye vyanzo vya maji maana yake ni kwamba sisi Ofisi ya Makamu wa Rais tusiposaidiana na Watanzania katika kuhakikisha kwamba tunalinda vyanzo vya maji katika nchi nzima, uzalishaji wa umeme ambao unatumia maji hautaweza kufanikiwa kwa kiwango ambacho tunakihitaji. Ndiyo maana Ofisi ya Makamu wa Rais tunayo mikakati kuhakikisha kwamba tunalinda vyanzo vya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wabunge wengi walikuwa wanaulizia tuna mikakati gani? Tuna mkakati wa mwaka 2006 ambao unahusu uhifadhi wa mazingira na vyanzo vya maji na ndiyo maana katika mkakati huu Ofisi ya Makamu wa Rais iliwaandikia barua Wakurugenzi wote wa Halmashauri nchini kuhakikisha wanabaini vyanzo vyote vya maji pamoja na changamoto zake ili wawasilishe Ofisi ya Makamu wa Rais ili vyanzo vingine viwe protected viweze kuwekewa utaratibu wa kuvitangaza kwenye gazeti la Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kupitia Bunge lako Tukufu muda tuliowaongeza wa hadi tarehe 20 mwezi huu unakaribia kwisha na kama nilivyosema juzi kwenye Bunge hili. Wakurugenzi ambao watakaidi na kutotekeleza agizo hili hakika Ofisi ya Makamu wa Rais itaorodhesha majina yao na kumpelekea Mheshimiwa Rais ambaye ndiye amewateuwa ili aweze kutafakari na kuona vitumbua vyao ama vitiwe mchanga ama laa! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tuna mkakati mwingine wa mwaka 2008, mkakati huu ni wa kuhifadhi mazingira katika hatua za haraka kwenye bahari na kwenye ukanda wa Pwani pamoja na mito, maziwa na mabwawa makubwa. Tuna mkakati mwingine wa 2012, huu ni wa kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Kwa hiyo, mikakati yote hii pamoja na wananchi kuwataka watekeleze sheria ya mazingira tuna uhakikika tunakwenda kulinda vyanzo vya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana tuliweza kufanya mazoezi makubwa kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais kunusuru bonde la Mto Ruaha Mkuu, Task Force ambayo Mheshimiwa Makamu wa Rais aliiunda. Ndiyo maana maeneo yote ambayo yana mabonde, maeneo yote ambayo yana shughuli za binadamu lazima tutoe miongozo namna ya kufanya agriculture ambayo ni ya kihifadhi yaani conservation agriculture.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo limezungumziwa sana ni jambo hili la upandaji wa miti na hasa Kamati pamoja na Wabunge kwamba tumekuwa na kawaida ya kupanda miti ikiwa ni pamoja na uzinduzi wenye sherehe, lakini siku ya siku miti hiyo tukiihesabu haifiki idadi ile ambayo inakuwa inapandwa; Kamati ilitaka kujua tuna mpango gani Ofisi ya Makamu wa Rais. Kwenye ilani ya CCM ukurasa wa 212 hadi 213 halmashauri zote nchini wanatakiwa kupanda miti isiyopungua milioni moja na laki tano, lakini ni pamoja na kuweka sheria ndogo zitakazosimamia masuala hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba kuanzia mwakani Ofisi ya Makamu wa Rais inaandaa utaratibu wa kufanya sensa kubwa itakayokwenda kujua miti ambayo imepandwa imekuwa mingapi na mingapi imekufa. Ili tuweze kutoa miongozo ambayo itatusaidia kuwa na Tanzania ya kijani na hiyo imeenda sambamba, Mheshimiwa Makamu wa Rais alipohamia Dodoma alianza na mradi mkubwa wa kuijanikisha Dodoma na kwa utaratibu huo tunaendelea kujanikisha maeneo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mikakati mingine ni pamoja na siku ya mazingira duniani, tumekuwa tukihamasisha wananchi wapande miti ikiwa ni pamoja na kuomba shule, Taasisi za Dini pamoja Taasisi Zisizo za Kiserikali katika upandaji wa miti. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge niwatoe wasiwasi kwamba nchi yetu itakwenda kuwa na mkakati huo kuhakikisha kwamba miti tunayoipanda tunaitunza na kukua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni hili la UDART kwamba NEMC ilikuwa wapi; nataka niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge, mwaka 2009 UDART waliweza kupata cheti cha tathmini ya athari kwa mazingira na walipewa masharti ambayo watakuwa wanayazingatia katika kuhakikisha kwamba wana-mitigate na kuepuka athari ambazo zingeweza kutokea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba, kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi ambazo mara kwa mara tunawaambia mojawapo ya madhara ni mafuriko makubwa ndiyo maana katika eneo hilo mafuriko ambayo hayakutarajiwa yamechangia kwa kiasi kikubwa kuhakikisha kwamba UDART inakuwa kwenye mafuriko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na shughuli za binadamu ambazo zinafanyika kando kando ya Mto Msimbazi na zenyewe zimechangia kwa kiasi kikubwa na ndiyo maana tuna mpango wa kupitia mito yote na miji yote kuhakikisha kwamba hawa ambao wako ndani ya mita 60 na wengine wamejenga mpaka kwenye kingo tuweze kuotoa mwongozo wa namna gani wanaweza wakaepusha mambo haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.