Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Silafu Jumbe Maufi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mungu kwa kunipa nguvu ya kuweza kuchangia kwa maandishi angalau kutimiza azma yangu kwenye hotuba ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kutoa pongezi za dhati kwa kazi njema ifanyikayo ndani ya Serikali ya Awamu ya Tano kwa miaka hii miwili na nusu chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan wakishirikiana na mtendaji wao mkuu, Waziri Mkuu Mheshimiwa Kassim M. Majaliwa, katika lengo la kuwainua wananchi wetu kiuchumi, kuondoa umaskini na kwa jitihada ya kuanzisha na kuimarisha miundombinu yote ya kufanikisha uchumi wa viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia kuhusu suala la ajira. Katika ukurasa wa 20, aya ya 37 ya hotuba amesema Serikali itaendelea kuimarisha ufuatiliaji wa tathmini ikiwa ni pamoja na kufanya kaguzi, kusajili, kusuluhisha na kuamua migogoro katika maeneo ya kazi. Sasa huu utaratibu uliopitishwa wa kuwaondoa watumishi wa darasa la saba ambao wamefanya kazi nzuri kuanzia Awamu ya Kwanza na jitihada zao ndio zimetufikisha hapa ndani ya Awamu ya Tano siyo mzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali tusizue mgogoro ambao tunalazimika wenyewe kuushughulikia kuupatia ufumbuzi. Kwanza miongoni mwao wanastaafu sasa na wataendelea kustaafu, ni bora kwa busara kuanzia sasa tuendelee na utaratibu huo unaohitajika kwa wakati huu. Hata wakati ule walikuwepo kwa uchache wao, lakini hawakuwa na wito wa kazi hizo na darasa la saba walizichukua. Narudia tena tuwaache wamalizie muda wao wa utumishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ni kuhusu barabara, ukurasa wa 44-45. Naipongeza Serikali yangu kwa jitihada ya kujenga miundombinu ya barabara hapa nchini kwa jitihada ya kuunganisha wilaya na mikoa hata na nchi jirani. Napenda kukumbushia kwa Serikali hii sikivu kwamba mikoa ya pembezoni ilisahaulika na msukumo wa maendeleo ya barabara ulichelewa kuwafikia ndio maana maendeleo yao bado yanasuasua katika nyanja zote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunashukuru Daraja la Momba kujengwa na kuunganisha Chunya (Kamsamba) na Rukwa (Kilyamatundu) lakini barabara zake kuelekea Chunya na kuelekea barabara kuu ya Tunduma – Sumbawanga ni za udongo, hivi Serikali inaonaje na barabara hizo kuwa za kiwango cha lami?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeweza kupita Mlima Kitonga na Mlima Nyang’oro ambayo awali ilitupatia wananchi shida sana ya kupita na kuchukua muda mrefu, lakini sasa naishukuru Serikali yangu imetatua tatizo na milima hiyo inapitika na usafiri wake kwa wananchi umewarahisishia na kutekeleza majukumu yao kwa urahisi na wepesi kwa maendeleo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuiomba Serikali kuangalia na barabara za milima inayoteremka mabonde ya Ziwa Rukwa na Ziwa Tanganyika kwa kuanza na hatua za awali kuelekea kiwango cha Kitonga na Nyang’oro ili wananchi wa maeneo hayo wafaidike na matunda ya Serikali yao na ikumbukwe tunapakana na nchi ya DRC – Congo na Zambia. Pia tunaomba jitihada kubwa kuongezeka kwa sasa kwani zinasuasua za Mkoa wa Rukwa kuunganishwa na Mikoa ya Katavi, Kigoma na Tabora na nchi za Zambia na DRC – Congo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Serikali kutoa tamko au mwongozo wa TARURA kushirikiana na Mabaraza ya Halmashauri kwani kule wanawashirikisha wananchi wa maeneo husika kufanya kazi. Pasipo kufanya hivyo kazi yao itakuwa ngumu au itawagharimu sana wakikosa ushirikiano wa awali kabla ya utekelezaji wao kwenye maeneo husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu ni kuhusu maji, ukurasa wa 52 – 53. Maji ni uhai wa viumbe wote duniani na ndiyo eneo nyeti linalohitajika kufanikisha mengine yote. Tunajitahidi kuanzisha miradi ya maji ambayo bado haijakidhi mahitaji kwa kutoa matokeo mazuri, imekuwa ni miradi ya kunufaisha hao wanaoifanya siyo walengwa (wananchi). Mradi haujatoa matokeo mhusika keshalipwa mabilioni ya pesa, siyo sahihi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano, taasisi zetu za majeshi hawana maji na ndiyo tunawategemea kwa ulinzi na usalama, mchana na usiku ndani ya nchi na nje. Pia shule na vyuo kukosa maji ni janga la kipekee. Matatizo ya taasisi za majeshi na shule kukosa maji yamekithiri Lindi, Mtwara, Rukwa, Ruvuma kwa ujumla mikoa ya pembezoni mwa nchi yetu, tuangalieni kwa huruma, tusijutie kuwa pembezoni ni tatizo kwa maendeleo yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri wakandarasi ambao hawana uwezo wa kuchimba visima na kupatikana maji kwa lengo la eneo husika wasipewe kazi na apewe muda wa kipindi maalum cha maji kupatikana na ndipo akubalike kupewa mradi mwingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la nne ni afya, ukurasa wa 54. Tunashukuru jitihada ya Serikali na kujituma kwa Waziri mwenye dhamana kuhakikisha huduma ya afya inasonga mbele. Hata hivyo, jitihada hii ya kuongeza idadi ya vituo vya afya nchini tunaomba iende sambamba na ujenzi wa Hospitali za Wilaya kwani Mkoa wa Rukwa hakuna hata wilaya yenye hospitali pamoja na kuanzishwa mwaka 1974.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri Mkuu aweze kushirikiana na wataalam wake kuona umuhimu wa Wabunge wa Viti Maalum kupatiwa angalau nusu ya Mfuko wa Jimbo kwa wastani wa idadi ya majimbo yaliyomo ndani ya mkoa anaoishi. Kwani Mbunge wa Viti Maalum na Mbunge wa Jimbo hawatofautiani kwenye majukumu ingawa wa Viti Maalum anazunguka mkoa mzima na kuwajibika ndani ya majimbo yote ya Mkoa. Sio ndani ya chama changu, wananchi na Serikali hawatutenganishi wanatuhesabu Wabunge tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.