Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Hasna Sudi Katunda Mwilima

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Kigoma Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. HASNA S.K. MWILIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya. Binafsi sina shaka kabisa kwamba 2020 Serikali ya Chama cha Mapinduzi itaendelea kuongoza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kama Kiongozi Mkuu wa shughuli zote za Serikali. Nianze sasa kuzungumzia changamoto mbalimbali zinazoikabili Halmashauri yangu ya Uvinza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la umeme, ukurasa wa 21 tunao mradi wa REA awamu ya pili kwenye Vijiji vya Kabeba, Mwakizega, Ilagala, Mkandarasi aliyekuwa akitekeleza mradi huu kasimamishwa kuendeleza mradi, wakati mradi huu ulitakiwa uwe umezinduliwa tangu Machi, 2017. Leo hii wananchi wamebaki kuziangalia nguzo na transfoma badala ya kuwasha umeme kwenye nyumba zao. Niombe Serikali ituletee Mkandarasi mwingine atakayemalizia mradi huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hili, hadi tarehe ya leo hatma ya mradi wa REA awamu ya tatu wananchi wa Jimbo la Kigoma Kusini hawajui lini mradi huu utaanza rasmi, niombe Serikali kutangaza tender mara moja ili na mradi huu wa REA awamu ya tatu uanze mara moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Uvinza inayo miradi sita (6) mikubwa ya maji. Mradi wa maji wa Nguruka, mradi wa maji wa Uvinza, mradi wa maji wa Kandaga, mradi huu wa Kandaga hadi leo Halmashauri ya Uvinza hawajui utekelezaji, kwa kuwa mradi huu unatekelezwa na Halmashauri ya Kigoma Vijijini pamoja na mradi wa maji wa Rukoma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na tabia ya kupeleka Viongozi wa Kitaifa upande mmoja wa Wilaya au upande mmoja wa Jimbo la Kigoma Kusini, mfano. Jimbo hili la Kigoma Kusini lina Kata 16 na Vijiji 61 ndani ya square meter za mraba 10,178 na Kanda mbili (2). Ukanda wa Reli una kata nane, Kata ya Kandaga inayopakana na Kidahwe Mbili, Kata ya Kazuramimba, Kata ya Basanza inapakana na Kasulu, Kata ya Uvinza, Kata ya Mganza, Kata ya Itabula inapakana na Urambo, Kata ya Nguruka, Kata ya Mtego wa Noti inapakana na Kibondo na Upande wa Kaliua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukanda wa Ziwa Tanganyika, Kata ya Mwakizega inapakana na Simbo. Kata ya Ilagala kwenye Gereza la Ilagala, Kata ya Sunuka, Kata ya Sigunga, Kata ya Herembe, Kata ya Igalula inayopakana na Mwesa Mkoa wa Katavi, Kata ya Bohingu kwenye Hifadhi ya Mahale, Kata ya Kalya inapakana na Mpanda. Naelezea haya yote ili Mheshimiwa Waziri Mkuu aone umuhimu wa Viongozi wa Kitaifa wanapokuja kufanya ziara wajue kuwa ukanda huu pia una kata nane (8) na vijiji 34 na una miradi mikubwa ya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mradi wa maji mkubwa wa Kalya na wananchi wameishaanza kunywa maji na Mkandarasi anajipanga kuukabidhi mradi huu Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza. Tunao mradi wa maji Ilagala tayari maji yanatoka, tunaomba mradi wa Mwalo wa Samaki na Dagaa Muyobaozi, Kata ya Mwakizega, lakini cha kusikitisha kila kiongozi anayekuja wanaishia kumpeleka ukanda huu wa Lake Tanganyika na badala yake wote wanaishia kuwapeleka ukanda wa Reli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Waziri Mkuu atakapokuja kufanya ziara ya Wilaya ya Uvinza aje kuzindua kati ya miradi ifuatayo: Mradi wa maji Kalya, mradi wa maji Ilagala au mradi wa Mwalo wa samaki Mwakizega sambamba na mradi wa shule ya sekondari ya Mwakizega.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho Mheshimiwa Waziri Mkuu atakapofanya ziara ukanda huu wa maji ndiyo ataona umuhimu wa kuligawa Jimbo, tayari utaratibu wote ulishafanyika kugawa Majimbo mawili (2) Jimbo la Uvinza na Jimbo la Kigoma Kusini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho niendelee kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi kubwa na nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.