Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Daniel Nicodemus Nsanzugwako

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kasulu Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja hii, hata hivyo nitoe ushauri na maoni yangu katika maeneo yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ulinzi na usalama page 56. Idara ya Uhamiaji na matendo ya unyanyasaji wa raia hasa wanaoishi katika mipaka ya nchi yetu na hasa wananchi wanaoishi katika Mkoa wa Kigoma. Imekuwa ni desturi hasa kwa wenzetu wa Idara ya Uhamiaji kushika watu, kunyanyasa watu eti kwa sababu ni wahamiaji haramu au uraia wao unatia mashaka. Niombe sana Ofisi ya Waziri Mkuu itoe maelekezo ya kiutawala juu ya mwenendo wa Idara ya Uhamiaji na hasa katika Mkoa wetu wa Kigoma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo yafuatayo yazingatiwe; heshima kwa wanachi wa Kigoma na kamwe watu wasitambuliwe kwa sura zao, lugha zao na maumbile yao. Weledi utawale na ikibidi mafunzo zaidi ya utambuzi wa nani ni raia na nani si raia yafanyike kwa uharaka. Baadhi ya wananchi wa Kigoma wanaamriwa na Idara ya Uhamiaji wapeleke vyeti vya kuzaliwa vya wazazi wao na babu zao. Mambo ambayo ni vigumu sana kufanya hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mara kadhaa ni kuendeleza unyanyasaji na usumbufu kwa wananchi wa Kigoma, Kasulu, Kibondo Kakonko na Uvinza. Aidha, kwa nini shida hii iwe zaidi kwa Mkoa wa Kigoma ilhali mikoa mingi ya mpakani hatusikii. Viongozi wa kisiasa, dini wanaharakati na hata wasanii mashuhuri wanatoka katika Mkoa wa Kigoma kudhaniwa na kuhisiwa siyo raia, jambo hili linatia simanzi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo matukio ya hovyo ambayo viongozi mbalimbali watokao Mkoa wa Kigoma wameitwa uhamiaji kwa mahojiano na wengine hata kupelekwa kolokoloni kwa sababu tu ya kuwa wenyeji wa Kigoma. Tafadhali haki itendeke kwa wote na mtindo wa sasa wa kukomoana, vitisho na hata kuoneana ifike mwisho, watu wetu wa Kigoma wanajihisi ni raia daraja la pili. Jambo ambalo siyo sahihi, raia wetu wote wapo sawa katika nchi yetu, tusitengeneze matabaka bila sababu za msingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakimbizi na wahamiaji haramu watambuliwe, naomba sana Serikali na hiyo Ofisi ya Waziri Mkuu ifanye kazi ya kuwatambua wakimbizi, wahamiaji haramu na wahalifu ili watofautishwe na raia wema na wakazi wa Mkoa wa Kigoma. Wakimbizi wetu wa DRC na Burundi zipo tamaduni tunazofanana, tamaduni hizo zisiwe sababu ya watu wetu kudhaniwa ni wakimbizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafahamu vizuri juhudi za Serikali yetu, lakini Mkoa wa Kigoma kupokea wakimbizi isiwe laana, tunapokea wakimbizi kwa niaba ya Taifa lote, vitendea kazi kwa Idara ya Uhamiaji na Polisi changamoto ya vifaa vya kazi na wanafanya kazi katika Idara hizi mbili katika eneo lenye wakimbizi ni tatizo kubwa. Idadi ya Maofisa na Maaskari iongezwe, magari ya doria yaongezwe, malipo ya motisha kwa wafanyakazi wa Idara hizi yatazamwe upya na yaongezwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja hii.
Ahsante.