Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Esther Nicholus Matiko

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kutoa mchango wangu kwenye maeneo matatu muhimu. Nikianza na umuhimu wa kulinda amani, utulivu na mshikamano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri Mkuu ameeleza kuwa kuna amani nchini ilhali hakuna amani kwa sasa. Hakuna utulivu kwenye Taifa letu maana kila kukicha matukio ya maonevu yanayofanywa na vyombo vya dola ya kuvunja haki za msingi kwa raia wake. Tunashuhudia mauaji yakiendelea kwa kasi nchini, utekaji pamoja na watendaji wa Serikali kutishiwa hata kushindwa kufanya kazi kwa mujibu wa sheria za nchi na weledi wa kazi yake bali wanasubiria kauli kutoka juu. Jambo hili linalirudisha Taifa letu nyuma. Taifa linakuwa la woga, wanahifadhi chuki na mawazo mbadala moyoni badala ya kuyatoa ili yasaidie kuijenga nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshuhudia unyanyasaji wa dhahiri wa Vyama vya Upinzani huku Msajili wa Vyama vya Siasa anafumbia macho na zaidi anatumika kukandamiza Upinzani. Mfano kwenye Hotuba Mheshimiwa Waziri Mkuu amesema kabisa kuwa Vyama vya Siasa vimeruhusiwa kunadi sera zao na itikadi ili kupata wanachama, kitu ambacho ni uongo kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri Mkuu anajua fika kuwa watendaji, polisi na hata Ofisi ya Usajili wa Vyama vya Siasa anaifumbia macho kauli batili inayoenda kinyume na Sheria na Kanuni za Vyama Vingi na Katiba ya nchi yetu; huku tukishuhudia Rais ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi akiendelea na mikutano ya hadhara na kupokea wanachama huku mtendaji wa Chama cha Mapinduzi (Katibu Mwenezi), ndugu Humphrey Polepole, akiendelea kufanya mikutano ya hadhara na kuvinanga vyama vingine huku wakipandikiza chuki. Leo hii kusema kuwa wawakilishi tu ndio wafanye mikutano ilihali inafahamika fika kuwa tuna vyama ambavyo havina uwakilishi wa Wabunge, Madiwani, Wenyeviti wa Mitaa na Vijiji Sasa hivi vyama vitatangaza vipi hizo sera zake na itikadi zao?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshuhudia pia jinsi fedha za Watanzania maskini zikitumika vibaya, hasa kwa chaguzi ambazo zinarudiwa kupitia minada ya viongozi wa wananchi kununuliwa na kusababisha si tu upotevu wa fedha bali mauaji na ulemavu kwa raia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini Mheshimiwa Waziri Mkuu anasema bila aibu kuwa CCM wameshinda Majimbo yote na kata 58 huku CHADEMA wakishinda moja tu? Eti CCM wameshinda kwa kishindo ilhali anajua hujuma inayofanywa na vyombo vya dola, Tume ya Uchaguzi na Wakurugenzi ambao ni makada wa CCM.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshuhudia jinsi Jeshi la Polisi linavyojigeuza Tume ya Uchaguzi na kubandika matokeo ya uchaguzi kinyume na taratibu, wakishuhudia watendaji wakibadili ballot box na kuondoka nalo mbele ya RPC Kinondoni na pale Magomeni. Hapa hatuwezi kuwa na uchaguzi huru na hivyo hakuna amani wala mshikamano.