Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Mohamed Omary Mchengerwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Rufiji

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba yake nzuri. Lakini niipongeze Serikali ya Awamu ya Tano kwa juhudi zake kubwa za kufanikisha utawala bora wa kujenga ustawi wa maendeleo ya uchumi jamii wa Taifa letu hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yako mambo mengi mazuri yamezungumzwa na mimi kwa niaba ya Warufiji na Wandengereko wote duniani niseme tu kwamba tunaipongeza sana Serikali kwa kazi nzuri iliyoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Rais wetu kwa kuchagua Mawaziri wa Nishati wazuri wachapa kazi ambao leo hii kuliwaka umeme eneo nusu la Rufiji, lakini hivi tunavyozungumza maeneo mengi ya Rufiji sasa yanakwenda kuwaka umeme, ikiwa ni pamoja na ahadi ya Waziri wa Nishati kwamba sasa kule Kata ya Ngarambe watapata umeme na nimeambiwa leo na kesho Kata ya Mwasenyi watawashiwa umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yako mambo mengi mazuri ya kuzungumza kuhusiana na sifa za Serikali ya Awamu ya Tano, lakini kwa uchache wa muda naomba nijielekeze katika hoja ambazo nimwombe Mheshimiwa Waziri Mkuu akisimama hapa awaeleze Watanzania. Kamati ya Katiba na Sheria ilimtaka Msajili wa Vyama vya Siasa kutatua migogoro iliyopo katika vyama vya siasa. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri Mkuu akisimama kwenye Bunge lako hili Tukufu awaeleze Watanzania je, Serikali ina juhudi gani za kutatua migogoro ya vyama vya siasa hapa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua kabisa kwamba, migogoro ya vyama vya siasa inakwenda kujenga taswira potofu kuhusu kuminywa uhuru wa siasa na demokrasia. Waziri Mkuu atueleze je, migogoro hii inasababishwa na mazalia ya mambo gani yanayohitaji kupatiwa ufumbuzi? Je, ni historia ya nchi yetu? Je, ni uhuru wa Tanganyika? Je, ni Mapinduzi ya kule Zanzibar? Au ni sintofahamu ya elimu ya uraia? Je, Serikali ina mpango gani wa kuimarisha masomo ya uzalendo na masomo ya umoja wa kitaifa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua kabisa kwamba, uzalendo na utaifa unajengwa kama ambavyo ilivyo kwa Masheikh, Mapadri na Maaskofu wanajengwa na kuandaliwa. Je, Serikali ina mpango gani wa kuleta mapinduzi ya kifikra unaodhamiria kuzalisha elimu ya vyama vya siasa inayotokana na mawazo duni ya udumavu yasiyoendana sambamba na mageuzi ya dira ya Serikali ya Awamu ya Tano?

Mheshimiwa Waziri Mkuu akisimama hapa basi atuelezee je, Serikali wakati tukiwa tunajielekeza katika suala zima la kuwaangalia Watanzania na kuangalia uzalendo uliopo pamoja na fikra za Watanzania, je, Serikali na ofisi yake inajipanga vipi kutoa elimu ya utaifa na kuondokana na msongo wa Taifa ili kuondokana na maporomoko ya miiko na maadili ya Watanzania?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri Mkuu akisimama hapa pia awaeleze Watanzania yalikuwa ni mawazo yapi ya Baba wa Taifa wakati wa kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi? Lakini pia Mheshimiwa Waziri Mkuu awaeleze Watanzania atakaposimama hapa makutano ya mawazo ya vyama vya siasa na ni kwenye ndoto gani ya Taifa letu? Na je, Serikali ina mpango mkakati gani wa kuondoa kusigana na huku kusigana kunasababishwa na ombwe la kitu gani linalosababisha kutofautiana kati ya wanasiasa, ili kuweza kujenga jamii nzuri ya Watanzania ambao kwa kweli wanailinda amani ya nchi yao na kuwa na umoja wa kitaifa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri Mkuu akisimama hapa basi awaeleze Watanzania Ibara ya 8 ya Katiba inatambua kwamba, ustawi wa wananchi unajengwa na Serikali yao, lakini pia Ibara ya 26 ya Katiba inatambua na inakataza kuondoa mgawanyo au kufanya makosa ambayo ameainishwa katika Katiba au makosa yaliyoainishwa katika sheria tulizonazo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri Mkuu akisimama hapa basi aelezee kuhusiana na mgawanyo wa pato la Taifa, yako manung’uniko mengi. Tunatambua wananchi wa Rufiji, wananchi wa Pwani, wananchi wa Kusini tunatambua kwamba, kipo kiasi cha fedha kilichotengwa kwa ajili ya kuendeleza Hifadhi ya Selous, lakini tunapata taarifa kwamba, kiasi kile cha fedha kimepelekwa kuendeleza Ruaha. Haya ni miongoni mwa mambo ambayo wananchi wengi wa Rufiji, Kusini na maeneo mengine wanayalalamikia, basi Mheshimiwa Waziri Mkuu ukisimama hapa ni vyema ukawaeleza wananchi wakatambua ni namna gani na ni kwa nini mgawanyo wa pato la Taifa umekuwa ni kikwazo kwa wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe Mheshimiwa Waziri Mkuu atakaposimama hapa atambue kwamba, wananchi wa Rufiji wana imani na Serikali yao ya Awamu ya Tano, lakini pia, wamenituma nimkumbushe Mheshimiwa Waziri Mkuu kwamba, tarehe 02/03/2017 Rais Dkt. John Pombe Magufuli alifika Ikwiriri na akaahidi ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami kutoka Nyamwage kuelekea Utete. Mheshimiwa Waziri Mkuu tukuombe wananchi wa Rufiji sasa jambo hili mpelekee Rais wetu na atambue kwamba wananchi wa Rufiji wana imani kubwa na Serikali yao na atambue kwamba tumebakiza miaka miwili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa ahadi hii ya ujenzi wa barabara kiwango cha lami ilianza mwaka 2017 na Mheshimiwa Rais alisema itajengwa kabla ya mwaka 2020 basi, atambue kwamba ni kilometa 33 na kwamba tumebakiza miaka miwili tu. Na Serikali ina mpango gani sasa kuhakikisha kwamba barabara hii inajengwa kwa kiwango cha lami?

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo kwa kweli, ni msingi wa wananchi wetu wa Rufiji na Pwani na maeneo mengine sisi tunampa hongera sana Rais wetu wa Awamu ya Tano kwa jitihada zake za dhati kabisa za ujenzi wa bwawa la Stiegler’s Gorge kama ambavyo nimetanguliza kusema. Na niseme tu mwenzangu amesema kwamba Stiegler’s Gorge ilianza miaka ya 1960, lakini mimi nataka kukataa niseme kwamba Stiegler’s Gorge kama sisi wa Rufiji tunauita STIGo, ilianza miaka ya 1956 wakati wa harakati za TANU, harakati za uhuru wa nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na Mwalimu Nyerere alidhamiria kujenga umeme huu kuweza kuikomboa nchi yetu. Na sisi tunaunga mkono na wananchi wa Rufiji tunaunga mkono sana, tunachoomba Serikali yetu ya Awamu ya Tano kama ilivyo madini katika maeneo mengine na wananchi wa Rufiji wanaomba kunufaika na Stiegler’s Gorge. Tuiombe Serikali kuhakikisha kwamba mradi huu wa Stiegler’s unakwenda kujenga barabara yetu ya kutoka Mwasenyi - Mloka kuelekea Ikwiriri, lakini pia, kutoka Mwasenyi - Mloka kuelekea Kibiti na maeneo mengine ya Morogoro yanayopakana na Stiegler’s Gorge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi ni ndoto za Mwalimu Nyerere hatuna haja wala hakuna sababu ya kuzibeza. Na kwa kweli, Rais Magufuli amefanya maamuzi magumu na ni miongoni mwa Marais ambao tuliwasubiri kwa muda mrefu sana. Na sisi tunampa pongezi sana kwa jitihada hizi. Na Warufiji tuko tayari kutambua mradi huu utakwenda kuinufaisha nchi, lakini utakwenda kuinufaisha Rufiji kwa mambo mengi mazuri yanayokuja; ujenzi wa barabara, ujenzi wa madaraja, Daraja la Utete litajengwa kuiunganisha Rufiji na maeneo mengine ya Kusini. Tunampongeza sana Rais wetu, lakini pia tunamtakia kila la heri katika kutekeleza mambo haya yote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya naomba kuwasilisha, naunga mkono hoja. Ahsante sana.