Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Ignas Aloyce Malocha

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kwela

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Kwanza kabisa niungane na wenzangu kushukuru Serikali kwa kauli ambayo imetoa asubuhi ya kuwarejesha Watendaji wetu wa Vijiji wa darasa la saba. Ilikuwa ni huzuni kubwa sasa imekuwa furaha, tunashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie hotuba ya Waziri Mkuu katika kipengele kinachohusiana na kilimo. Ukiangalia ukurasa wa 27 katika hotuba ya Waziri Mkuu ameelezea kwa kifupi juu ya uzalishaji wa mazao ya kilimo na biashara. Katika maelezo yake ameelezea ufanisi mkubwa uliokuwa umetokea katika msimu wa 2016/2017 na 2017/2018 kwamba wananchi walizalisha chakula yapata tani milioni 15.9 na mahitaji ya chakula yalikuwa ni milioni 13.3, kwa maana ya ziada ilikuwa ni tani milioni 2.6 na ziada nyingine ambayo ilinunuliwa na NFRA ni tani 26. Ukifanya hesabu unakuta karibu tani milioni 5.5 haikununuliwa na kiwango hicho ndiyo kilibaki kwa wananchi wamehangaika nacho na hawakujua wauze wapi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili linahuzunisha sana katika nchi yetu. Wakulima wa mahindi wamepata shida sana katika jambo hili, wanazalisha kwa jitihada zao na kwa nguvu kubwa lakini wanakosa wapi wauze mazao hayo. Hadi sasa kilio hicho bado kinaendelea, wananchi wana hali mbaya sana hasa Mkoa wangu wa Rukwa ukienda karibu Wilaya zote, ukienda kwenye magulio yale utafikiri watu wana msiba kwa sababu mazao yao wamekosa kwa kuuza na maendeleo yamesimama. Kama mtu alianza nyumba 2015 imesimama vilevile haiendelei. Sasa tunajiuliza hii hali itaendelea mpaka lini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika maelezo ya kitabu hiki cha Waziri Mkuu hakuna mahali ambapo wameeleza ni namna gani watatatua tatizo hili. Kwa hiyo, wameacha wakulima kwenye dilemma, sasa sijui wakulima wa mahindi waache kulima au ni kitu gani kinatokea. Hali hii ni mbaya sana, uchumi umesimama na wananchi wamefilisika, je, Serikali inakubali hali hii iendelee na hata huu uchumi wa viwanda tunaouzungumzia, vitakuwa na faida gani kama mwananchi hana uchumi wa kununua bidhaa ndani ya kiwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nataka nizungumzie jambo labda Waziri wa Kilimo atakuja kutuelezea ni namna gani mwaka huu amepanga mipango mizuri ya kuwezesha wananchi kuuza mahindi yao ikiwa ni pamoja na kufungua mipaka. Kwa sababu kuacha hali hii kuendelea sioni sababu ya wananchi kuendelea kulima mahindi, watasimama na ndiyo maana hata unaona hata mwaka huu uzalishaji umepungua wameshindwa kununua mbolea kwa sababu hawana pesa, wamelima kienyeji, wamepanda mbegu ambayo sio bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukizunguka katika Wilaya zetu zote za Mkoa wa Rukwa mazao yapo chini sana hayajastawi, hii ni kutokana na wananchi kukosa fedha za kununulia pembejeo kwa sababu mahindi waliyozalisha hayajanunuliwa na mengine yameoza. Kwa hiyo, jambo hili ni la kuangaliwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nataka nizungumzie suala la TARURA. Kwanza tunapoingeza Serikali, tuna imani chombo hiki kimeanza kufanya kazi nzuri. Tunachoomba chombo hiki kinapaswa kipewe fedha za kutosha, kisipopewa fedha za kutosha itakuwa ni sawa na Halmashauri zetu zilivyokuwa zinahangaika na barabara hizi zinashindwa kutengenezwa kwa sababu zilikuwa zilikuwa zinapewa fedha kidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kutoa pesa hizi angalieni Halmashauri ambazo barabara zake zina changamoto. Kwa mfano ukichukulia Halmashauri yangu ya Wilaya ya Sumbawanga jiografia yake ni mbaya na barabara ni mbaya, hazipitiki muda mwingi kwa sababu jiografia yake imekaa utata, barabara zinaunganishwa na milima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, ukiangalia barabara ya Mawezunzi – Msia, Miangalua - Chombe – Kipeta, ukija huku Miangalua kuelekea Laela ukizunguka kule Kwakifuti barabara ni mbaya, daraja la Kaengesa limeshabomoka ambalo lilijengwa na Wamishionari sasa hivi halipo, linahitaji pesa nyingi. Barabara ya Kaengesa – Myunga inahitaji pesa nyingi, kivuko cha pale Laela kwenda kwenye hospitali kinahitaji pesa nyingi. Kwa hiyo, tunaomba TARURA waweze kuwezeshwa kupata pesa nyingi ili waweze kumudu kutengeneza barabara hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tumeona Serikali inafanya jitihada ya kutengeneza standard gauge, tunashukuru…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)