Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Magdalena Hamis Sakaya

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Kaliua

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kunipa nafasi ili niweze kuchangia Hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Niungane na Waheshimiwa wa Bungeni na Watanzania wote kumshukuru Mungu kwa kukupa afya njema, tunaomba aendelee kukutetea na kukupigania katika majukumu yako.

Mheshimiwa Spika, niishukuru sana hiyo kauli ya Serikali ambayo imetolewa leo hapa Bungeni asubuhi kwa ajili ya kuwarejesha watumishi wa umma ambao waliondolewa kinyama kwenye kazi zao, kwa kweli nashukuru sana, tumerudisha imani na matumaini kwa wale watendaji.

Mheshimiwa Spika, mwaka juzi Serikali ilikuja na mkakati kuhakikisha kwamba watoto wote wa Kitanzania wanakaa kwenye madawati na ikawezekana. Hata hivyo, hivi tunavyoongea watoto wengi wa Tanzania kutokana na idadi kuwa wengi, wengi wao wanakaa nje, jua linawapiga, mvua yao, jua lao.

Mheshimiwa Spika, tunaiomba Serikali, kwa mpango ule ule iliyokuja nao 2016/2017 watoto wakaweza kukaa kwenye madawati wote, tunaomba Serikali ije na mkakati maalum kuhakikisha watoto wote wanakaa kwenye madarasa. Katika wilaya zote hakuna sehemu ambapo madarasa yanatosha na kiukweli mtoto anayesoma nje hata ufaulu unakuwa ni mdogo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala lingine ni suala la vyakula mashuleni. Kutokana na tamko lililotolewa na Serikali kwamba elimu ni bure wazazi na walezi wameona kwamba hata jukumu la vyakula shuleni ni jukumu la Serikali, kwa hiyo watoto wengi sasa hivi hawali shuleni na mtoto ambaye ana njaa hafundishiki. Tunaiomba Serikali itoe ufafanuzi mzuri kwenye shule namna gani wazazi wahakikishe watoto wanakula shuleni.

Mheshimiwa Spika, ni ukweli kwamba tumepanda kielimu kwa maeneo mengi particularly kwenye Wilaya yangu ya Kaliua tumepanda vizuri sana na najua tumechangiwa na Walimu lakini pia watoto kula mashuleni na speed ya viongozi kufanya kazi; lakini sasa hivi wameacha kula tumeona trend yao imeanza kushuka.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tunaomba Serikali itoe ufafanuzi mzuri namna gani watoto waanze kula shuleni tukizingatia wengi wao wanatoka nyumbani hawajala mpaka jioni wana njaa, kwa hiyo hawawezi kufaulu vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala lingine ni suala la mifugo. Nchi yetu ni nchi ya pili kuwa na mifugo mingi Afrika, lakini ukiangalia pato la Taifa ambalo linaletwa na sekta ya mifugo bado ni dogo sana. Tatizo ni kwamba pamoja na kuwa tunaongoza kwa kuwa na mifugo mingi, lakini mifugo yetu haina tija kwa sababu hakuna maeneo yanayopangwa popote kwenye mikoa wala wilaya kwa ajili ya malisho ya mifugo.

Mheshimiwa Spika, katika maeneo mengine mifugo inaonekana kama ni changamoto, wanaonekana wanazurura na kila siku wanakamatwa na wanapigwa risasi huko kwenye hifadhi. Hatujaweza kama Watanzania kutumia rasilimali ya mifugo kama uchumi wa Taifa.

Mheshimiwa Spika, naiomba sana Serikali lazima kwenye bajeti hii tuje na mpango mkakati namna gani kila mkoa na wilaya ambao wanaendeleza mifugo watenge maeneo kwa ajili ya mifugo.

Mheshimiwa Spika, lingine ni kwamba, hakuna malisho, wakati wa mvua nyingi malisho yanajaa, ikiondoka mvua mifugo yote inateketea, kwa hiyo Mfugaji anafuga wakati wa mvua wakati wa ukame mifugo yote imepotea. Tunaiomba Serikali ije na mpango wakati wa mvua tuwe na utaratibu wa kuvuna majani tutengeneze hay, tutengeneze silage tutunze vyakula ili tufuge kwa tija.

Mheshimiwa Spika, lingine tuwe na viwanda. Tulikuwa na viwanda vya kuchakata mazao ya mifugo. Tulikuwa na Tanganyika Packers leo hamna. Ni kweli sasa hivi tunajitahidi kuwa na machinjio ya kisasa, lakini hatuna viwanda vya kuchakata mazao ya mifugo.

Mheshimiwa Spika, bahati nzuri kwenye mifugo kila kitu ni mali. Kwato, ngozi, nyama, mifupa, kila kitu ni mali. Tukiweza kutumia vizuri sekta ya mifugo tutaweza kuhakikisha kwamba inaingiza pato zuri kwa Taifa letu na tukaweza kufanya wafugaji wakawa ni watu ambao wana tija siyo huku wananyanyaswa kila siku kwa sababu Serikali haijaweza kuweka mfumo mzuri wa mifugo kwenye nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, suala lingine ni Mfuko wa Wanawake na uwezeshaji wa wanawake wa vijana. Tumeiona hapa Serikali imetenga fedha milioni mia saba themanini na tatu kwa ajili ya vijana ambapo vijana 840 kutoka halmashauri mbalimbali wamenufaika. Vijana 840 ni kijiji kimoja au viwili. Leo tuna vijana wangapi Tanzania, tuna wilaya ngapi, tuna kata ngapi, tuna vijiji vingapi? Kuja na vijana 840 mimi nashangaa.

Mheshimiwa Spika, naiomba Serikali, fedha zinazotengwa kwenye halmashauri ni kidogo sana. Leo Kaliua tumetenga zaidi ya milioni mia mbili hamsini, vijana wenyewe wamekuja na vikundi hamsini, hatukuweza kuwapa wote tumewapa vikundi 15. Wanawake wamekuja na vikundi 56 tumewapa vikundi 30 na wanaomba milioni kumi unawapa milioni mbili, haitoshi.

Mheshimiwa Spika, ni kweli tunatenga lakini kwa kweli kama hatujajizatiti vizuri Serikali hatuwezi kusaidia vijana wakaweza kujiajiri, hatuwezi kusaidia wanawake wakaweza kujiajiri kwa sababu fedha tunayotenga ni kidogo. Halmashauri zetu tunafahamu uwezo wake, hawana uwezo wa kuweza kusaidia vikundi vyote vinavyoundwa. Kwa hiyo naiomba Serikali, lazima itenge fedha ya kutosha ili wanawake wawezeshwe, vijana wawezeshwe ili nchi yetu iondokane na kundi kubwa ambalo linakosa ajira na waweze kuendeleza familia zao.

Mheshimiwa Spika, suala lingine ni suala la kilimo; nazungumzia kidogo kwa sababu nitazungumzia kwenye sekta ijayo. Tuna shida kubwa Taifa letu, hatujaweza kuwa na mizani ya kisasa kwenye manunuzi ya mazao, tumelia Bungeni na mimi binafsi nimeongea sana hapa. Leo bado wakulima wanakwenda kulaliwa kule vijijini, wakulima wanakwenda kununuliwa mazao yao bila mizani ya uhakika.

Mheshimiwa Spika, vile vile leo lumbesa inaendelea, pia kuna ndoo za Mozambique, mkulima analima kwa shida, anavuna kwa shida hata kwenda kuuza anaibiwa. Naiomba Serikali kwa nini tunashindwa kusimamia mizani ya kisasa kwa ajili ya kununua mazao? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa nini Serikali inaruhusu lumbesa mpaka hivi leo dunia ya leo, kwa nini Serikali inaruhusu Mozambique ndoo moja inachukua mpaka galoni saba, kwa nini inaruhusu? Hatuwezi kuwa na nchi ya viwanda bila kuwa na kilimo chenye tija. Pia tunahitaji wakulima wanufaike na wanachokilima, tunaiomba Serikali ije na mpango, ituambie kwa nini tumekubali wakulima waendelee kuibiwa wakati wakulima hao hao tunawategemea waendeleze Taifa hili.

Mheshimiwa Spika, suala lingine ni maji; katika Wilaya ya Kaliua bado hatuna mpango mkakati wa kupata maji. Mpango wa Ziwa Victoria kutoa maji kutoka Mto Malagarasi ni mpango wa muda mrefu. Leo ni mwaka wa tano bado mpango huu uko kwenye upembuzi yakinifu. Naiomba Serikali kwenye mpango wa mwaka huu ituletee mpango wa muda mfupi kuwatua wanawake wa Kaliua ndoo kichwani.

Mheshimiwa Spika, leo mvua zinanyesha ukienda Kaliua akinamama angalau wanatulia, watoto wanaenda shule, njoo mwezi Agosti ni hatari. Kwa hiyo naiomba sana Serikali ije na mpango huu mwaka huu tuhakikishe kwamba tunapata maji wanawake wa Kaliua, watoto waende shule kwa wakati na tuondokane na shida.

Mheshimiwa Spika, mpango wa Maji Victoria haufiki Kaliua wala Urambo, kwa hiyo mpango pekee wa kuwapatia wana Kaliua maji ni kutoka Mto Malagarasi lakini mpango huu unaenda taratibu sana na fedha inayopangwa pale ni ndogo haitoshelezi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala lingine ni afya; Kaliua tunaishukuru Serikali imetutengea fedha kwa ajili ya hospitali yetu ambayo tunategemea kujenga Kaliua, lakini pia Kaliua mpango wetu wa mwaka huu ni kuwa na vituo vya afya, tumeongeza vituo vya afya vinne, viwili Ulyankulu, viwili Kaliua, Jimbo langu.

Mheshimiwa Spika, naiomba Serikali, wananchi sasa hivi wanacheka kwa speed kubwa Mheshimiwa Rais alivyofika Kaliua alitoa milioni kumi kwa ajili ya kituo cha Kaliua Usinge ambapo wengi wao wanatibiwa kule Nguruka.

Mheshimiwa Spika, naiomba Serikali iongeze nguvu kwenye kituo cha Usinge ili wananchi ambao wanatibiwa Nguruka waweze kutibiwa pale kwenye kituo cha Usinge iongeze nguvu ya Rais. Mfuko wa Jimbo tumeongeza, wananchi wanachanga sana kila siku, Rais ameweka nguvu tunaomba na Serikali pia itusaidie mwaka huu tuhakikishe kwamba kituo kile kinakamilika ili wananchi wa Kaliua waweze kupata huduma za afya kwa karibu.

Mheshimiwa Spika, nizungumzie hata hapa Dodoma. Benjamin Mkapa wanafanya kazi nzuri sana ya kuokoa wananchi na pia Wabunge wenyewe, lakini Madaktari hakuna. Hivi sasa ninavyoongea kuna Mbunge amelazwa paleā€¦

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)