Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Ritta Enespher Kabati

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. RITA E. KABATI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Kwanza kabisa nianze na dua la kukuombea, naomba Mwenyezi Mungu akujalie, akupe afya njema na wote wanaokutakia mabaya washindwe kwa Jina la Yesu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nianze na pongezi kubwa kabisa za kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kuwasilisha hotuba yake; na nimpongeze Mheshimiwa Jenista, Mheshimiwa Mavunde na Mheshimiwa Ikupa.

Mheshimiwa Spika, pia niwaambie wenzetu mwenye macho haambiwi ona, hivi kazi zote ambazo Mheshimiwa Rais, ambazo Serikali hii imezifanya, miradi mingi imefunguliwa, kila siku Mheshimiwa Waziri Mkuu anakwenda huku na huku, kweli hamuioni jamani? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niombe tu niseme kwamba, ukisoma ukurasa wa 10 unaonesha kabisa wananchi wameanza kuelewa sera za Chama cha Mapinduzi, wamehama wengi sana. Katika uchaguzi tu kati ya 59; 58 tumeshinda CCM na Wabunge wote majimbo yote tumeshinda na niwapongeze hata Wabunge ambao wamehama upande ule wakaja upande huu wa kwetu; hongereni sana kwa kuja huku wala hamjakosea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia, niwapongeze Mawaziri wote waliopo katika Serikali hii bila kuwasahau wanawake wenzetu; hamjatuangusha wanawake, mmefanya kazi vizuri sana tu. Kila siku tunawaona mnahangaika huko na huko kwa kweli mko vizuri, hongereni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nianze na kuchangia kuhusu uwezeshaji kwa vijana. Niendelee tu kuipongeza Serikali hii ya Chama cha Mapinduzi kwamba, walikuja Iringa wakafungua yale mafunzo ya vijana katika Chuo cha Don Bosco, Mheshimiwa Jenista nakushukuru sana. Vijana wengi sana wameitikia mwitikio mkubwa sana katika kile chuo mpaka kumetokea changamoto kubwa vijana wengi wanakosa sehemu za kusoma kwa sababu zile nafasi ni chache. Tungetamani hata kila wilaya yale mafunzo yaendeshwe ili vijana wengi waweze kupata yale mafunzo. Pia, kuna changamoto kwamba, vijana wale miezi sita sasa hawajapata posho, labda hilo liangaliwe ili waweze kupata wasisome kwa shida sana.

Mheshimiwa Spika, vile vile tulikuwa tunaomba pengine iwepo connection kati ya wakuu wa wilaya pamoja na chuo ili kuratibu maana imekuwa malalamiko yanatufuata sisi Wabunge tunashindwa sasa twende wapi. Tunaomba pia, hilo liangaliwe. Pia, uwepo utaratibu mzuri kuhakikisha kwamba, wale wanaohitimu yale mafunzo angalau pia halmashauri zao ziweze kuwapatia asilimia tano ile ya mikopo. Pia kama kuna kazi basi wapewe za kutengeneza madawati, chaki na kadhalika ili ile mikopo iwe rahisi kuweza kurejeshwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niendelee kumpongeza Mheshimiwa Jenista, niendelee kumpongeza sana Mheshimiwa Mavunde wamefanya kazi nzuri sana kufuatilia mikataba ya wafanyakazi katika viwanda, katika makampuni yale ya wawekezaji. Sasa niombe, sasa hivi waelekee kwenye hizi sekta ambazo si rasmi; kwa mfano wafanyakazi wa ndani wanafanya kazi kwenye mazingira ambayo bado ni magumu sana.

Mheshimiwa Spika, najua wengine waajiri wao mko humu ndani, lakini mtanisamehe lazima niwasemee, wengi wametoka kwenye Mkoa wetu wa Iringa, bado malalamiko yao ni makubwa sana hawatendewi haki. Vile vile kuna wafanyakazi ambao wanafanya kazi kwenye migahawa nao bado mikataba yao si mizuri. Hawa wenzetu wanaofanya kazi kwenye baa nao wanafanya kazi kwenye mazingira magumu ingawa ile bia yenyewe inatuletea faida kubwa sana katika nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vile vile nisisahau kabisa naomba niwasemee wenzetu waandishi wa habari, wamekuwa wakifanya kazi nzuri sana tunaonekana kwenye TV, wanatuandika kwenye magazeti, lakini nao pia mikataba yao si mizuri sana kwa sababu utakuta bado wengine hawana hata bima hizi za afya, hawana bima za maisha, wanahatarisha hata maisha yao. Vile vile tunatakiwa tuwasaidie ili wafanye kazi kwenye mazingira mazuri waendelee kujenga Taifa letu kwa kuandika vizuri. Mishahara yao pia, bado haieleweki, kila mwajiri anamwekea vyovyote anavyotaka; kwa hiyo, niombe kabisa pia, waangaliwe.

Mheshimiwa Spika, niendelee katika sekta ya afya. Niendelee kuipongeza Serikali kwa sababu, wamepunguza changamoto ya upatikanaji wa dawa kwenye hospitali na vituo vya afya, lakini kuna changamoto kwenye Hospitali yetu ya Mkoa wa Iringa. Kwamba eneo lile ni dogo sana na lina mwingiliano na magereza. Tulishawahi kusema na Waziri wa Mambo ya Ndani analijua na Naibu Waziri wa Afya naye si muda mrefu alikuwa kule ameona.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo inasababisha Madaktari wetu Bingwa wanakaa nje ya hospitali, kwa hiyo inakuwa shida sana kuwahudumia wagonjwa wanapopata shida usiku. Vile vile tuna changamoto ya Daktari Bingwa wa Watoto, hakuna kabisa kwenye hospitali yetu ya mkoa.

Mheshimiwa Spika, vile vile upungufu mkubwa sana wa wafanyakazi sekta ya afya, karibu asilimia 60 ni tatizo katika mkoa mzima; na Hospitali ya Wilaya ya Mufindi yenyewe inaongoza kwa sababu asilmia 40 hakuna wafanyakazi. Kwa hiyo, niiombe Serikali iangalie kuziba zile nyufa za wafanyakazi ambao waliondolewa ili wagonjwa waweze kutendewa haki.

Mheshimiwa Spika, niipongeze pia Serikali kwa mgawo wa 4.5 billion katika wilaya zetu kujenga hospitali za wilaya katika mkoa wetu; Wilaya ya Kilolo, Wilaya ya Mufindi, Iringa DC. Japokuwa katika hospitali ya manispaa hatujatengewa kitu chochote na kuna changamoto kubwa ya jengo la vipimo hakuna kabisa na kuna mashine za X-Ray, CT-Scan, Ultrasound, hakuna kabisa. Vilevile wodi za kulaza wagonjwa wengine pia, hakuna na tulikuwa tunategemea kwamba, ile hospitali ingepunguza msongamano wa wagonjwa wa hospitali ya mkoa.

Mheshimiwa Spika, najua kwamba, Mheshimiwa jafo alishapita na kuona hizi changamoto, kwa hiyo niombe kwa kweli zifanyiwe kazi. Mashine hizi zitakazopatikana zitasaidia hata gharama ndogondogo za kuiendesha ile hospitali. Vile vile huduma ya wazee dawa ni ghali sana, zipo nje ya mfumo, kwa hiyo huduma zile ambazo ziko nje ya mfumo wa bima yao wanapata shida kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile niendelee kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kukaa na wafanyabiashara na kusikiliza changamoto zao. Ni kweli tozo katika viwanda zimekuwa nyingi sana, ningeomba kwa kweli waziangalie ili tuendelee kuhamasika na huu uchumi wa viwanda, ili viwanda vingi viweze kufunguliwa.

Mheshimiwa Spika, nichukulie tu mfano mdogo kwenye sekta ya maziwa. Unaona TFDA ile yogurt wana- charge flavor dola 3,000, lakini hii ingechajiwa tu labda kwa zao lenyewe la maziwa bila kuangalia kila flavour kwa sababu mtu akiwa na flavour 10 anachajiwa (charge) dola 3,000. Kwa hiyo, naona hii pia, Waziri wa Mifugo aliangalie.

Mheshimiwa Spika, vilevile OSHA. Hii OSHA wanapima afya za wafanyakazi unalipia Sh.80,000, Manispaa nao wanapima afya za wafanyakazi wanalipia tena; sasa hii ingewekwa kwenye sekta moja, ili zote zichajiwe (charge) kwa pamoja. Hii inawakatisha sana watu wanaofanya kazi katika sekta hii ya maziwa.

Mheshimiwa Spika, mbaya zaidi kuna watendaji wengine hawaitakii mema hii nchi yetu, kwa sababu kwa mfano tarehe tatu mwezi wa nne walikamata gari la maziwa la ASAS pale Iringa. Lile gari lilivyokamatwa limekamatwa kuanzia saa 12.00 limekuja kuachiwa saa 6.00 wamechajiwa (charge) 1,000,000/= kwa kosa ambalo kwa kweli, ukilisikiliza wala si kosa.

Mheshimiwa Spika, sasa hapohapo ukatokea uharibifu wa packets 3,000 takriban 3,500,000/=. Sasa hii inaleta matatizo sana kwa wenzetu ambao tunatagemea kwamba, wangetusaidia hata uajiriā€¦

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. RITA E. KABATI: Mheshimiwa Spika, naomba kuunga mkono hoja hii, kwa yale ambayo sijachangia nitachangia kwenye Wizara husika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana.