Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Suleiman Ahmed Saddiq

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mvomero

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. SULEIMAN A. SADDIQ: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi asubuhi ya leo. Niungane na Wabunge wenzangu kukukaribisha tena Bungeni karibu sana Bungeni tumefarijika sana kukuona ukiwa na afya njema na unang’ara kweli kwenye Kiti chako, Mwenyezi Mungu akufanyie wepesi zaidi, Inshallah. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi asubuhi ya leo na mimi niweze kuzungumza mawili matatu ya maendeleo kwa nchi yetu na Wilaya yetu ya Mvomero.

Naomba nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wetu kwa kazi kubwa anayofanya katika nchi yetu, kwa kazi ambayo italeta manufaa makubwa leo na kesho na kesho kutwa tunampongeza sana na tunasema wananchi wa Mvomero tuko naye bega kwa bega.

Mheshimiwa Spika, pia naomba nimpongeze Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi ambayo anafanya hususani kusimamia masuala mbalimbali ya pamba, kilimo na maendeleo kwa ujumla na naomba niwapongeze na wenzake wote na timu yao yote.

Mheshimiwa Spika, bila ya kupoteza muda naomba nizungumzie suala la Wilaya ya Mvomero, uvamizi wa ardhi katika Wilaya ya Mvomero uliofanywa na Manispaa ya Morogoro, naomba Mheshimiwa Waziri Mkuu, Waziri wa TAMISEMI, Waziri wa Maliasili na Waziri wa Ardhi kwa pamoja wanisikilize kwa makini sana.

Mheshimiwa Spika, Manispaa ya Morogoro imevamia eneo la Wilaya ya Mvomero na wameanzisha mitaa miwili ndani ya Wilaya ya Mvomero, mtaa wa kwanza unaitwa CCT Forest na mtaa wa pili unaitwa Maili Kumi na Nane.

Mheshimiwa Spika, Mitaa hii ipo ndani ya Wilaya ya Mvomero wapiga kura wa Mjini wanapiga kura katika Wilaya ya Mvomero na maeneo hayo yalianzishwa kwa mujibu wa utaratibu na sheria za nchi yetu. GN. No. 204 ya mwaka 1953 ilianzisha msitu wa kuni ambao uko ndani ya Wilaya ya Mvomero. GN No. 366 ya mwaka 2002 ilianzisha Wilaya ya Mvomero na GN Na. 242 ya mwaka 1991 ilianzisha Manispaa ya Morogoro hizi GN zote zipo kisheria na zipo pale kila mmoja inaeleza mipaka na maeneo jinsi yalivyo. Nimuombe Mheshimiwa Waziri Mkuu, nimuombe Waziri wa TAMISEMI mara watakapofanya majumuisho naomba tamko la Serikali eneo hili sasa litambulike kama eneo halali la Wilaya ya Mvomero na wavamizi wote waondoke wananchi waliopo maeneo yale tutawatambua kama wananchi wa Mvomero hatuna ugomvi nao. Kwa hiyo, naomba suala hili lifanyiwe kazi na Serikali na tupate majibu ya haraka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo la pili ni eneo la NARCO - National Ranch zile kubwa ambazo ziligawiwa kuna eneo ambalo walipewa wenzetu ambao hadi leo maeneo yale hawajaendeleza kuna kampuni mbili moja inaitwa Katenda group na moja inaitwa Elisa Mollel walipewa heka 5000. Eneo lile walipewa mwaka 2002 hadi leo maeneo yale hawajayaendeleza, leo kuna kaya zaidi ya 430 zinaishi eneo lile, naomba Waziri muhusika aunde timu yake waje wakague eneo lile watukabidhi Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero, tuweze kuliendeleza, tuweze kuwaleta wawekezaji eneo limekaa bure limekuwa pori yamebaki majoka, yamebaki mapori ambayo hayana faida yoyote kwa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kutokana na muda unavyoenda haraka naomba haya maeneo yote ya NARCO yaliyopo ndani ya Wilaya ya Mvomero Mheshimiwa Waziri alikuja akazungumza naomba sasa aje na timu yake tukae na timu ya Mvomero tuweze kuona ni namna gani maeneo yale yataendelezwa na yataleta faida.

Mheshimiwa Spika, Mvomero tumepata wawekezaji wengi maeneo ya barabarani yote ni mapori hayaendelezwi, namuomba Waziri wa Maliasili akumbuke ombi la Wilaya ya Mvomero tuliloandika barua na kupeleka ofisini kwake tunahitaji heka 10,000 za barabarani tuwape wawekezaji waweze kujenga viwanda, waweze kuleta mashamba bora ya kisasa tuweze, kusonga mbele. Kwa hiyo, naomba Waziri wa Maliasili aweze kukumbuka barua yetu ya Mvomero.

Mheshimiwa Spika, pia tuna mgogoro wa hifadhi na Mikumi National Park na kijiji cha Doma na Kata ya Doma, namuomba Waziri wa TAMISEMI, Waziri wa Maliasili, Waziri wa Ardhi watuletee timu tuweze kukaa nao chini Mikumi National Park wameingia kwenye eneo la Mvomero, wameingia kwenye mashamba ya wakulima na sasa hivi wameweka na beacon, suala hili naomba tamko litolewe na ikiwezekana timu ya Mawaziri tukutane tuweze kuona tunafanyaje.

Mheshimiwa Spika, lakini naomba Mheshimiwa Waziri Mkuu atoe tamko kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero, mapato ya ndani asilimia 40 na ile 20 asilimia 60 mapato ya ndani yale yaende kwenye miradi ya wananchi, fedha za mapato ya ndani zinatumika kulipa madeni ya Halmashauri, fedha za mapato ya ndani zinatumika katika mipango ya Wilaya ambayo sio maendeleo na miradi ya wananchi.

Mheshimiwa Spika, wananchi wamejenga zahanati wanahitaji bati, wananchi wanahitaji pampu ya kisima fedha hizi zinakwenda kwenye sherehe za Nane Nane, fedha hizi zinakwenda kwenye mambo mengine, naomba tamko la Waziri Mkuu fedha za mapato ya ndani kwa mujibu wa kanuni na sheria zirudi kwenye miradi ya wananchi na bahati nzuri Waziri Mkuu nimeonana nae na baadaye tutaonana nitamkabidhi na baadhi ya documents ili tamko litolewe wananchi wa Mvomero wapate maendeleo kutokana na mapato ya ndani.

Mheshimiwa Spika, lipo tatizo moja kubwa katika Wilaya ya Mvomero, Wilaya ya Mvomero kijiografia unatoka mpakani na Handeni unarudi mpaka Morogoro Mjini unaanza safari unaacha Manispaa unakwenda Mzumbe, unakwenda mpaka Mgeta, unakwenda mpaka Kikeo, unasafiri masaa zaidi ya 10 kutoka kwenye Kata moja kwenda kwenye Kata nyingine tulipeleka ombi tunaomba Jimbo la Mvomero ligawanywe ili tuwe na Majimbo mawili ya uchaguzi. Suala hili tumelifikisha kwenye vikao mbalimbali bado tutaleta na documents zetu tunaomba Serikali inapofanya marekebisho ya Majimbo ya Uchaguzi watuangalie Mvomero namna gani jiografia yetu ilivyokuwa ngumu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la mwisho naomba kuipongeza Serikali, ninampongeze Waziri wa Utumishi kwa kauli yake ya leo Bungeni kuhusu ajira za watumishi hii ndiyo Serikali sikivu ya CCM, Waziri wa Utumishi nakupongeza, naipongeza Serikali kwa maamuzi haya mazuri ambayo yana tija kwa Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, bila ya kupoteza muda nasema naunga mkono hoja. Ahsante sana.