Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Amb. Adadi Mohamed Rajabu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muheza

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nashukuru sana kwa kunipa fursa hii kuchangia hoja hii ambayo ni muhimu sana ya hotuba ya Waziri Mkuu. Hotuba ambayo ni hotuba mama, hotuba ambayo ina-cover shughuli zote zile za Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, napongeza sana juhudi ambazo anafanya Mheshimiwa Rais, tumeona maendeleo mbalimbali. Nampongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu, siyo siri tumemuona jinsi ambavyo anazunguka nchi nzima kwa ajili ya kuiletea maendeleo nchi yetu. Mheshimiwa Waziri Mkuu hongera sana na Mawaziri wote kwa shughuli ambazo wanazifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona miradi mikubwa, tumeona SGR ya reli ya kati ikianza, tumeona ufufuaji wa ATCL, tumeona flyovers, tumeona ujenzi wa vyanzo vipya vya umeme, tumeona miradi ya Mkulazi ambayo ni maendeleo makubwa sana kwa kilimo na pia tumeona bomba la mafuta la kutoka kule Hoima mpaka Mkoani Tanga. Juhudi ambazo nazipongeza kwa hii miradi mikubwa, hii inaongeza uchumi kupanda ndiyo maana kwenye hotuba ya Waziri Mkuu anaonesha kuna viashiria vikubwa vya kupanda uchumi wetu kwa asilimia 6.8. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la bomba la mafuta la Tanga tunaamini kabisa kwamba, shughuli hiyo imeshaanza na kwa kweli, itatusaidia sana Mkoa wa Tanga. Aidha, suala la ujenzi wa reli ya Tanga, mpaka sasa hivi ninafahamu kwamba upembuzi yakinifu umemalizika na juhudi zinafanyika za kuweza kuingia kwenye PPP, lakini tunaiomba Serikali Mheshimiwa Waziri Mkuu, suala hili ulipe kipaumbele. Najua upembuzi yakinifu wa Tanga – Arusha umemalizika, lakini upembuzi yakinifu wa Arusha – Musoma ndio unaendelea. Sasa ni vizuri tukaanza kutangaza hii tender ili ianze kushughulikiwa. Naamini kabisa wapo wawekezaji ambao watajitokeza kama alivyojitokeza juzi kwenye ujenzi wa viwanda vya madawa. Kwa hiyo, naomba suala hili lipewe umuhimu kwa sababu, wenzetu majirani pale Kenya SGR yao ambayo inakuja mpaka bandarini kwao Mombasa, wanatupa changamoto kubwa sana kwa hiyo, ningeshukuru na hii iende sambamba na SGR ya reli ya kati. (Makofi)

Miradi mikubwa imeshughulikiwa kwa kiwango kikubwa sana, lakini sasa naona kwamba msisitizo mkubwa twende vijijini. Naamini kabisa tutakapokwenda vijijini tutapunguza umaskini ambao uko mwingi kwenye vijiji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kilimo; tumeona kabisa juhudi ambazo zimefanyika kwenye suala la korosho, lakini hatujaona juhudi ambazo zinafanyika kuinua zao la katani. Sasa hivi zao la katani liko bei kubwa sana kwenye soko la dunia. Ni hivi majuzi tu Waziri wa Kilimo amekuja Tanga kuanza kufufua, lakini ningeshukuru kama Waziri Mkuu utaingilia kati na kujaribu kuona tutalifanya vipi soko la katani liweze kukua. Katani ndiyo imetukuza Tanga, miradi mingi sana imetokana na katani, sasa katani inadharaulika, haijapewa ule umuhimu ambao unatakiwa. Waziri Mkuu na Waziri wa Kilimo naamini kabisa suala hili mtalipa umuhimu wa kipekee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la maji; maji ni muhimu sana, sasa hivi tunashindwa kupata Wawekezaji Muheza pale kwa sababu ya maji, tuna tatizo kubwa sana la maji. Ninamshukuru sana Waziri wa Maji, tumepata mradi wa kutoa maji Pongwe, mradi wa kutoa maji Pongwe unakwenda vizuri sana Mheshimiwa Waziri Mkuu, lakini mradi huo ambao tuliutegemea umalizike mwezi ujao mwishoni umechelewa kwa mwezi mmoja na umechelewa kwa sababu ya ujenzi wa tenki ambao utaanza baada ya wiki mbili zijazo, lakini inanipa wasiwasi kwenye mifumo ya kufumua Mji wa Muheza ambao tulitengewa bilioni tano, sasa bado hatujaruhusiwa kutangaza hili suala. Ningemuomba Waziri wa Maji aliangalie ili utakapofika wakati basi mradi huu usiweze kuchelewa kwa sabau, maji yatakapotoka kule ni lazima tufumue hii mifumo ya Mjini Muheza. Hata hivyo namshukuru sana kwa juhudi zake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la miradi mikubwa 17 ambalo tumeambiwa kila siku linakwama shauri ya financial agreement haijasainiwa. Miradi hii 17 itakapoanza itasaidia sana tatizo la maji kwenye nchi hii, lakini kila siku tunaambiwa financial agreement. Najua kuna technical ground iliyoko pale, naamini kabisa kwamba, Waziri wa Fedha yuko hapa na Waziri wa Maji yuko hapa, suala hilo mtaweza kulitatua kabla ya bajeti ya Wizara ya Maji haijasomwa. Nitashukuru sana na pia kwenye bajeti ya maji itakaposomwa basi ile shilingi 50 ambayo tuliipigia kelele sana wakati uliopita nategemea itakuwepo kwenye bajeti ya Waziri wa Maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la afya, tunajenga Hospitali ya Wilaya ya Muheza na hapa nimeona kwamba, kuna hospitali zitajengwa 67 nchi nzima. Namtegemea Waziri wa Afya na au TAMISEMI, Waziri wa TAMISEMI naamini kama tumeonesha juhudi basi naamini hizo bilioni 1.5 na Muheza tutapewa ili tuweze kukamilisha hii hospitali yetu ya Wilaya. Lakini pamoja na hayo tunawashukuru sana TAMISEMI na Waziri wa Afya kwa kutupa milioni 400 kwa ajili ya kujenga kituo cha afya ambacho tumekianza kule Mkuzi. Tunategemea pia kujenga vituo vingine vitano vya afya ambavyo ambapo juhudi za wananchi wameanza kule Muhamba, wameanza kule Ngomeni, wameanza kule Tongwe, wamenza Potwe na wamenza Ubwari ambacho tunaendelea kukiboresha na wameanza kule maeneo ya Amani - Msarai, zote hizo wameshaanza kuweka misingi, naamini kwamba, tutakapofika juu basi Serikali itakuja iweke mkono wake pale.

Suala REA Muheza ina Kata nyingi sana, kata 37 kwa hiyo, nina vijiji karibu 135 ambavyo vingi bado havijapata umeme. REA imeanza kuingia, survey imefanyika kwa vijiji vingi, lakini kazi ilikuwa haijaanza ni wiki iliyopita tu Waziri alipopita pale, ambapo ningependa kumshukuru sana Mheshimiwa Waziri Dkt. Kalemani kwamba baada ya kufika basi kazi zimeanza, nguzo zimeanza kuletwa, lakini ninachoomba ni suala hili lifanyike kwa haraka kwa sababu vijiji vyangu vingi havijapata umeme. Survey ilipofanyika tu kwenye vile vijiji wananchi wenyewe wameanza kufurahi, wameanza kushukuru. Mimi nimekula mbuzi na kuku wengi tu wananipa, lakini bado hawajapata umeme, lakini mbuzi hao wenu nimewala pamoja na kuku wengi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la barabara, barabara yangu ya Amani na Muheza kilometa 36 ipo kwenye bajeti shilingi bilioni tatu, lakini mpaka sasa hivi bado sijaona dalili zozote za TANROADS kuja kuanza kuishughulikia. Ningeomba Mheshimiwa Waziri Mkuu na Waziri wa Ujenzi basi suala hili muliangalie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho ni suala la Watendaji wa Vijiji na madereva ambao walimaliza darasa la saba, kwa kweli inasikitisha. Sisi tumeendeshwa na madereva wa darasa la saba kwa miaka yote, miaka mingi na wamefanya kazi kwa bidii. Juzi wakati hilo zoezi linafanyika tulikuwa tuna ziara ya kwenda wapi, naambiwa magari yako pale Halmashauri madereva hawapo wamesimamishwa, nini? darasa la saba. Mheshimiwa Waziri Mkuu tuwe na imani, wamefanya wameendesha gari bila ajali zozote zile miaka yote, wanakuja mwisho wanakaribia kustaafu tunawafukuza. Tuwe na ubinadamu tuangalie na hawa watu ningeshauri kabisa Mheshimiwa Waziri Mkuu basi warudishwe waendelee kufanya kazi kwa miaka yao ambayo imebaki. Wakati wanaajiriwa watu hawa wakati huo darasa la saba lilikuwa lina umuhimu wake, lakini sasa hivi wasomi wengi! Lakini hatuwezi kuwa tumewapata wasomi basi tuwaache wale. Naomba kabisa Serikali iangalie na ione namna ya kurekebisha. (Makofi)

Baada ya kusema hayo, naunga hoja mkono na ninakushukuru sana kunipa nafasi hii.