Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017

Hon. Emmanuel Adamson Mwakasaka

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tabora Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

3

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017

MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia hii hoja. Mimi ni Mjumbe pia wa Kamati hii ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge. Kwanza naipongeza Kamati hii kwa kazi ambazo imekuwa ikizifanya pamoja na ugumu wake na changamoto zake, lakini imekuwa ikifanya kazi bila kumwonea mtu yeyote kama taarifa ambavyo imeweza kusomwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Bunge hili liweze kuelewa Kamati ile ya Maadili ina Vyama vyote, tuko mle ndani Vyama vyote na hatujawahi kupiga kura kutoa hukumu yoyote ile, tumetoa hukumu zote tukiwa tumekubaliana na hii inamaanisha kwamba hukumu zile hazikuwa na upendeleo wa aina yoyote. Kama ingekuwa siyo Kamati ile ya Maadili ambayo Mheshimiwa Naibu Spika unaielewa kazi mnayotuletea pamoja na Mheshimiwa Spika, kusingekuwa na Kamati ile sijui Bunge hili lingekuwaje.

Mheshimiwa Naibu Spika, mtakumbuka hasa sisi ambao ni Wabunge wageni, Bunge hili wakati tunaanza nidhamu ilikuwa siyo kabisa ambayo Mheshimiwa Mbunge anapaswa kuwa nayo kwa baadhi ya Wabunge wenzetu. Hata hivyo, baada ya mashauri mbalimbali leo hii hata ukiliangalia Bunge lina nidhamu kubwa. Nawashukuru sana Wabunge pia kwa kutuwezesha sisi kufanya kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hata unaona hata ukimwambia mtu anayevunja taratibu labda ukimwambia kaa chini, hurudii hata mara mbili, mara tatu, anakaa. Haikuwepo hiyo mwanzoni na nawashukuru pia Waheshimiwa Wabunge wenzangu kwamba mmeona umuhimu wa kuwa na nidhamu humu ndani.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni kwamba hakuna uhuru usiokuwa na mipaka hata uhuru wa kuzungumza kama ambavyo watu wamekuwa waki-quote Katiba kwamba wana uhuru wa kuzungumza. Uhuru wowote ule siyo absolute, kwa maana kwamba siyo timilifu kuna mipaka yake hata katika kuongea, sasa ukiwa umetumia vibaya uhuru huo basi unajikuta unafika mahali ambapo sipo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona hata wakati Mbunge mmoja anaongea hapa jana, Mheshimiwa Mbunge mmoja alikuwa anaongea suala ambalo limekatazwa hata kwenye vifungu hivi vya Kanuni zetu huruhusiwi kutumia lugha ambayo ni ya matusi au ya dhihaka hata kwa Mbunge mwenzio, siyo Mheshimiwa Rais tu kama ambavyo kila kitu Mheshimiwa Rais amekuwa over protected siyo kweli, hata kwa Mbunge mwenzio huruhusiwi kwa mujibu wa Kanuni zetu hizi na hasa hiyo ya 64(1)(f) na (g), inakataza kabisa hata kwa Mbunge mwenzio. Kwa hiyo siyo Rais tu hata sisi tunapaswa kuheshimiana. Pia kuzungumza uongo imekatazwa, kila jambo unalozungumza humu basi uwe una ushahidi nalo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, Mheshimiwa Mbunge mmoja hapa amezungumza suala la kwamba Mheshimiwa Rais alimwita Mheshimiwa Lowasa kumrudisha kwenye Chama cha Mapinduzi. Sijaiona hata kwenye clip yoyote kama ambavyo huwa mnatuma clip, je, mtu angekwambia uje Kamati ya Maadili uthibitishe unayo clip hiyo au mtu anaongea tu ili kufurahisha na kujaribu kutaka wananchi waamini hivyo. Kwa hiyo, naomba Waheshimiwa Wabunge tuwe tunaangalia tunachokizungumza ili msije mkajikuta mnaletwa kwenye Kamati hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama kusingekuwa hata na Code of Conduct unaweza ukaona humu ndani kwenyewe, hivi mavazi ya humu ndani yangekuwaje! Sasa kwa sababu kuna Code of Conduct Waheshimiwa Wabunge wanachagua mavazi ya kuvaa. Hata hizi sheria kama tunavyosema hatuhitaji kumwonea mtu yeyote, tunafanya kazi kwa ajili ya kuweka mambo sawa Bungeni kama ambavyo sasa tumeendelea kufanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna baadhi ya watu ni wachochezi wapo humu, lakini Waheshimiwa Wabunge wale ambao wanawachochea wenzao natoa rai tu kwamba jaribuni kuwaangalia wale mnaowachochea, wengine wanachochea anayepewa adhabu ni mwingine, sasa wewe unapata faida gani?