Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017, Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017

Hon. Riziki Saidi Lulida

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017, Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017

MHE. RIZIKI S. LULIDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kutoa shukrani za dhati. Nakushukuru kwa kunichagua na mimi kuwa mmoja wapo wa kuchangia siku ya leo. Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia afya njema na nitoe pole za dhati kwa Watanzania wenzangu na wananchi wa Mkoa wa Lindi hasa katika Wilaya ya Kilwa kwa kifo cha Mzee wetu Kingunge Ngombale Mwiru, Mwenyezi Mungu amlaze mahali pema peponi. Amina.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niangalie Tanzania kwa ubora wake na jinsi Mwenyezi Mungu alivyoipendelea. Ameipendelea Tanzania kwa kuturuzuku vitu mbalimbali ikiwemo mito mikubwa unaikuta Tanzania. Tanzania ni nchi ya kumi na moja kuwa na vyanzo vikubwa vya maji ikiwemo Maziwa ya Victoria, Tanganyika, Nyasa, mito mikubwa tumeipata Tanzania lakini Mwenyezi Mungu akatujaalia tukapata bahari Tanzania, hivyo hata tukisema mizigo inateremshwa Tanzania, nchi za wenzetu wanashindwa kupata vitu kama rasilimali ambazo tumepata Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania tumeruzukiwa mbuga kubwa za wanyamapori na urithi wa dunia tumeupata Tanzania ikiwemo Kilimanjaro, Serengeti, Selous Game Reserves na nyinginezo. Mwenyezi Mungu bado akaendelea kutusaidia sisi kutupa madini ya kutosha. Sasa hivi Tanzania nzima kila mkoa unaokwenda kuna madini. Kuna madini ambayo hata nchi zingine hawana kama Tanzanite, lakini tunajiuliza bado Tanzania wananchi ni maskini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajiuliza tumekwama wapi mpaka Watanzania tumekuwa maskini namna hii? Suala hili tujiulize Watanzania wote kwa uchungu wa nchi yetu kujiuliza kwa pamoja sio kumwacha mtu mmoja anakimbia peke yake, huku nyuma watu wamemwachia anachokifanya peke yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuziona resources kama hizo ambazo Tanzania zinachezewa chezewa nataka niongee katika zao ambalo liko katika Mkoa wangu wa Mtwara na Lindi. Hili ni zao la korosho. Zao la korosho sasa hivi limezagaa Tanzania nzima, lakini cha kushangaza baadhi ya wananchi wa Mikoa ya Lindi na Mtwara na baadhi ya mikoa wanayolima korosho kufaidika katika kipindi cha miaka miwili na nusu kutoka korosho Sh.600 mpaka kufikia Sh.4,000. Kinachoshangaza sasa hivi kumetokea sabotage kubwa sana katika hili zao za korosho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukimuachia nyani shamba utavuna mabua na usipoziba ufa, utajenga ukuta. Tunajua kabisa haya ni mambo yanafanyika na Serikali inasema ina mkono mpana, huu mkono mpana uko wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, korosho kama korosho Tanzania haionekani pamoja na kwamba sisi ndio tunaolima korosho. Inaonekana ya kwanza Vietnam; ya pili, India; ya tatu Nigeria; Ghana, Brazil, lakini Tanzania hatupo. Wafanyabiashara wakubwa wa korosho wanakuja kununua korosho Tanzania. Ametokea Vietnam kuja kununua korosho Tanzania amekutana na mazingira magumu sana ya kibiashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mara ya kwanza wali-hold makontena yote akajikuta ana korosho imekaa katika warehouses hawezi kuziondoa, hivyo anaanza kufanya biashara yake kwa hasara, mpo Watanzania? Sasa hivi tumeyaona, mimi nilirusha clip kwa Wabunge kuwaonesha jinsi korosho za Lindi zimetiwa mawe, kokoto, mchanga zimezunguka tayari ziko Vietnam korosho zetu ambazo zimewekwa mchanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mnasema mna mkono mpana, mkono mpana uko wapi hapo? Kama ni hivyo, hata mimi nina mkono mpana, kama kwa mkono wenyewe namna hii kujikuta mazao yetu yanapelekwa India, yanapelekwa Vietnam yakiwa na kokoto ni aibu kwa Taifa na uchumi huu utadorora kwa vile kuna kundi la watu hawataki kuona Watanzania wanafanikiwa, hawataki waone katika Tanzania hii wananchi wa Tandahimba, Naliendele, Mchinga ambao sasa hivi walikuwa wanaweza kupata milioni 50, hawataki, wanataka kuturudisha nyuma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu isilitazame suala hili kwa kawaida, ilitazame suala hili kwa mapana yake. Wewe ni shahidi, tupo humu ndani kwa muda mrefu, tulikuwa na viwanda vya korosho, viko wapi? Humu ndani tunasikia maneno, tutafufua, tutafufua! Viko wapi? Bado wamevishika, wamevifunga, hawajavifufua, viwanda hivyo wananchi hawana ajira na wao wanafanya kazi zao kwa sababu hawaoni thamani na viwanda vile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la viwanda 13 viko wapi? Masasi kulikuwa na viwanda, Newala kulikuwa na viwanda, Lindi kulikuwa na viwanda, Dar es Salaam kulikuwa na viwanda mpaka leo havijafufuliwa, viko wapi viwanda? Halafu mnasema mtakuja mtuletee viwanda tena, vile mlivifanya nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo wananchi wanatafuta ajira, kwa vile korosho mnapeleka India, ajira inakwenda India! Sisi hatuonekani kama producer wa korosho, Watanzania tuko katika aibu kubwa. Kahawa ya Tanzania inauzwa Uganda, sisi wenyewe tuko wapi? Mazao ya Tanzania yanauzwa Kenya, ina maana Kenya they are strong enough kusimamia mazao yao na maendeleo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na natural resources tulizokuwa nazo Tanzania tumepitwa na nchi zote tunazoziona, Kenya, Uganda, mpaka Rwanda imetupita, Tanzania ya mwisho. Tujiulize tumerogwa na nani? Mtanijibu mtasema tena wewe, basi tumejiroga sisi wenyewe kwa kuwakumbatia watu ambao wana-sabotage uchumi wetu lakini tunawaangalia kwa sababu ya maslahi binafsi na corruption. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya PIC. MSD wamekuja katika meza yetu na baadhi ya Taasisi nyingine, MSD wamebuni tenda ya ku-supply dawa nchi 15, sheria zilizokuwa mbovu za Tanzania, feasibility study tu inatakiwa ifanyike kwa muda wa mwaka mmoja, strategic plan one year, action plan one year... (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)