Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.

Hon. Munde Abdallah Tambwe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.

MHE. MUNDE A. TAMBWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa fursa hii niweze kuchangia hotuba ya CAG na PAC na hotuba ya LAAC.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kuipongeza ofisi ya CAG kazi nzuri walioifanya, lakini niipongeze Kamati yangu ya PAC kwa kazi kubwa walioifanya katika kupitia vitu hivi. Nianze moja kwa moja na mambo ya TANESCO, kwa sababu nchi yetu iko kwenye Sera ya Viwanda, hatuwezi kuwa na viwanda bila kuwa na umeme wa uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, taasisi za Serikali zinadaiwa pesa nyingi, ukiangalia ukurasa wa 21 mwaka 2016 tulikuwa tunadaiwa shilingi bilioni mia moja ishirini na tisa. Kufikia sasa ukiangalia ukurasa wa 22 tunadaiwa shilingi bilioni mia moja themanini na tisa. Niiombe sasa Ofisi ya ya Waziri wa Fedha, Hazina, ifanye mkakati wa makusudi mazima, kuzikata fedha taasisi hizi zinazodaiwa, kutokana na bajeti zao za umeme kila wanapoleta bajeti zao, huwa kuna bajeti za umeme, tunaomba bajeti hizi za umeme zikatwe moja kwa moja na zipelekwe TANESCO ili tuweze kuwa na umeme wa uhakika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili linawezekana, Local Government walikuwa wanakatwa hela za LAPF, hazipelekwi kwenye mifuko yao, lakini Serikali ikaamua kukata moja kwa moja kupitia Hazina na kupeleka kwenye mifuko yao na sasa hivi pesa zinakwenda. Tunaomba sasa kwa umuhimu wa TANESCO, ili tuweze kuenda na sera ya viwanda, Serikali ikate pesa hizo za Taasisi moja kwa moja na kuzipeleka kwenye sehemu husika ambayo ni TANESCO. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumuunge mkono mkono Rais katika suala hili la umeme, Rais amehangaika sana, kwanza kabisa, ameanza kuvunja mikataba mibovu ya umeme, amevunja mikataba ya Symbion, lakini, amevunja mkataba mkubwa wa kifisadi wa IPTL ambao ulikuwa unachukua karibu milioni thelathini, kila mwezi, kuwapa kununua mafuta mazito ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Rais anafanya kazi sana, anastahili pongezi na anastahili kuungwa mkono kwa vitendo. Niwaombe sana Hazina wahakikishe fedha hizi zinarudi TANESCO kupitia Taasisi zinazohusika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais, ameweka nguvu kubwa Kinyerezi one (I), lakini ameweka nguvu kubwa Kinyerezi II. Yote hiyo ni kuhakikisha umeme unapatikana. Kuna watu waliokuwa na wasiwasi sana na Stieglers Gorge, kwamba haiwezi kufanikiwa, lakini kwa jambo la kushangaza Mheshimiwa Rais na Serikali yake wameshatangaza tenda, kwa ajili ya kujenga huo mgodi wa umeme na umeme huo nadhani muda sio mrefu mwaka 2021 tutaanza kupata megawatts 2000 kutoka huko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli Mheshimiwa Rais anapojituma niwaombe Mawaziri wanaohusika nao wajitume, tuone tunamuunga mkono kiasi gani, ili kupata umeme wa kutosha na viwanda vyetu tunavyovijenga kwa kasi viweze kufanya kazi kutokana na umeme huo tutakaoupata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli nampongeza sana Mheshimiwa Rais na nimwambie tu kwamba hizi ni legacy anazoziacha, hatutakaa tumsahau kwa kazi kubwa anazozifanya na ataweza tu, ameweza standard gauge, barabara, Flyovers, ameweza elimu bure, naamini ataweza na Stieglers Gorge itajengwa na itatoa umeme na watu tutafaidika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende sasa nikachangie kuhusu NSSF, kwanza nianze kupongeza, miradi mizuri ya majengo ya NSSF, mradi mzuri wa Twangoma tumeenda kukagua zile nyumba ni nzuri, tumekagua nyumba za Kijichi ni nzuri, lakini naamini na nyumba za Dege zitakapokwisha zitakuwa nzuri. (Makofi)

TAARIFA. . .

MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti kwanza naomba unitunzie muda, lakini nisimlaumu sana Mheshimiwa Sophia ni njuka, haelewi chochote, sijawahi kuwa Mjumbe wa Bodi ya TANESCO. Kama ana uhakika alete uthibitisho Bungeni kwamba niliwahi kuwa Mjumbe wa Bodi ya TANESCO, mwambie atulie, huo unjuka usimsumbue sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti naomba kuendelea. NSSF, ina mradi wa Dege ambao tumeenda kuutembelea mradi ule umechukua pesa nyingi za umma karibu bilioni mia mbili na point. Tunaiomba sana Serikali aidha iongeze mbia mwingine mradi ule uishe au itumie mbinu mbadala yoyote kuhakikisha mradi ule unakwisha ili mradi ule ufanye kazi pesa za umma zirejee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuiombe pia Serikali, miundombinu ya barabara ya kwenda Kijichi na Tuangoma, kwa kweli hairidhishi hata mtu anakwenda kupanga akianza kupelekwa anaweza kuona huko anapokwenda hapafai. Kwa hiyo, tunaomba sana mradi wa miundo ya barabara itengenezwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii Watanzania hizi nyumba za NSSF, zinakopesheka, kwa sababu ukienda leo kununua nyumba ya milioni themanini, unaambiwa ulipe asilimia 10. Ukilipa asilimia 10 zinazobaki zinagawiwa kwa miaka 15. Unaingia ndani na unalipa polepole, tofauti na mashirika mengine unatakiwa ulipe hela cash ndiyo uingie ndani. Aidha, ukakope Benki na Benki tunajua kwamba watu wengi hawakopesheki hasa sisi wanawake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nawapongeza sana NSSF kwa kazi nzuri wanaifanya. Napongeza pia uongozi mpya kwa Mkurugenzi wa NSSF, naye ni Mkurugenzi mzuri sana anajitahidi tunamwombea kila la kheri aweze kupata mwekezaji mwingine amalizane na huu mradi uliopo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongee sasa kuhusu Mlimani City, ulipata bahati ya kwenda kutembelea mradi wa Mlimani City, kwa kweli tunaomba Serikali ifuatilie mradi huu kwa makini zaidi. Inasikitisha sana mkataba huu ni mbovu kupita kiasi, watu hawa kwenye mkataba walikubaliana walipe 10 percent ya gross ya mapato ya Milimani City, lakini mpaka leo hii, watu wao wanalipa net ya ten percent sio gross.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulipouliza Mlimani City Uongozi wa Chuo cha UDSM kwa nini watu wao hawalipwi gross wanalipwa net, wanasema mgogoro unaendelea. Sasa hivi wana miaka 13, ni jambo la kushangaza kusikia bado mgogoro unaendelea, haujatatuka kwa maiaka 13, tunamnufaisha mwekezaji ambaye alikuja bila mtaji na dola 75 kama shilingi laki moja na nusu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huwezi kuamini, sasa hivi pale Dar es Salaam wameanzisha Milimani City mradi wa parking za magari, hakuna mfumo wowote, unawaonyesha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwamba parking zile zinaingiza shilingi ngapi kwa siku, kwa wiki, wala kwa mwezi. Ni mwekezaji anakuja ku-declare kwamba kwa mwezi huu, nimeingiza milioni tatu wanakubali bila kujua chochote, ni vitu vinasikitisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti kuna ukumbi pale Mlimani City, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, hawajui ukiwauliza ukumbi ule unaingiza shilingi ngapi kwa mwezi au kwa wiki, ni mwekezaji anakuja ku-declare. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkaguzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, haruhusiwi kwenda kukagua Mlimani City, anakatiliwa na mwekezaji, hivi ni vitu ambayo nimwombe sana Waziri wa Fedha, aunde Tume ya haraka iwezekanavyo na Waziri Mkuu, wakakague upya ule mradi ufanyiwe uchunguzi wa kina. Mtu huyu amepewa mkataba wa miaka 85, inatia shaka. Niiombe sana Serikali yangu ifanye pale kazi mpya iende ikaague, tukae tena mezani Mkataba ufumuliwe na uwekwe mkataba vizuri. Kuna vitu vinasikitisha sana huwezi kuona majengo yote haya yale hatuingizi pesa yoyote kwenye Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee kidogo kuhusu Pride, kwa sababu ni mama, sisi akinamama ndiyo tunaokopa Pride ni jambo linalosikitisha sana kuona kwamba kuna watu wamezihodhi pesa za Pride, niiombe Serikali sasa ichukue hatua za makusudi mazima kuhakikisha wale wote waliohusika kwenye masuala mazima ya Pride, wanachukuliwa hatua za kisheria. Tunaamini Serikali ya Awamu ya Tano ina uwezo huo mkubwa na tunaamini watajulikana na pesa zetu zitapatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.