Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.

Hon. Allan Joseph Kiula

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Iramba Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.

MHE. ALLAN J. KIULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru nami kuweza kupata nafasi ya kuchangia katika mawasilisho ambayo yamewasilishwa na Wenyeviti wa Kamati. Ningependa kujikita kwenye wasilisho la Kamati ya PAC, yapo mambo ambayo yanabidi yatolewe uamuzi na Bunge ili yajadiliwe kwa kina ili kuweza kuweka mambo vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kuzungumzia suala la Mlimani City, Mlimani City limeelezwa kwenye taarifa ya PAC na tumeweza kuona ambavyo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam hakinufaiki Mkataba wa Mlimani City. Ukisoma kwa kituo, paragraph hiyo, utaona jinsi mwekezaji alipokuja na jinsi mtaji wake alivyoutoa na baadaye akatengeneza madeni, akaenda TIC akaweza kunufaika na msamaha wa uwekezaji.

Mheshimiwa mwenyekiti, pia tumeona uendelezaji, tulitembelea Mlimani City pale katika maeneo ambayo yanatakiwa yaendelezwe, kimkataba kama walivyokubaliana hayaendelezwi, kuna hoteli ya nyota tatu haijajengwa, lakini pia kuna botanic garden haijafanyiwa kazi na ukiangalia kwenye maelezo yao kuna mahali wale watu wanagawana dividend, kwa maana kuwa mradi huo una faida, lakini pia hawalipi kodi stahiki kama walivyokubaliana kwenye mkataba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulifanya mahojiano na wenzetu wa Chuo Kikuu, ikaonekana wanaendelea na mazungumzo, lakini mazungumzo hayo wanayofanya, eneo lolote lile ambalo, lina manufaa kwa Chuo Kikuu yule mwekezaji, halitaki, isipokuwa anataka maeneo ambayo wao wanaona kwamba wanaweza kunufaika nayo, ndipo hapo mabadiliko yafanyike, wa-review ule mkataba, ukiwemo muda wa mkataba ambao ni muda mrefu sana, lakini pia wameendeleza wamefanya extension pale, hiyo extension iliyofanyika, imefanyika haikuwemo kwenye mkataba na wameendeleza maeneo ambayo wanapata pesa. Kwa hiyo suala zima la Mlimani City, inabidi liangaliwe kwa macho mawili na Bunge hili lazima liazimie, mkataba huo upitiwe upya na TIC watoe maelezo ya kutosha ili tuweze kuona chuo kikuu kinanufaika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, liko jambo zima la ukopeshaji wa matrekta Suma JKT. Bunge lililopita tulizungumza kwamba bado yapo madeni makubwa watu hawajalipa matrekta, kwa hiyo, matrekta yanakuwa kama vile yalitolewa zawadi, Kamati imeshindwa kuona kwamba kwa nini madeni haya hayalipwi. Kama trekta ni rasilimali linafanya kazi, linalima na wengine wanakodisha ina maana watu wote waliokopa matrekta wanatakiwa wayalipe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana tulizungumza, mwaka mzima sasa umepita hapa, hatuoni juhudi zozote. Kwa hiyo tulishawishi bunge liazimie kwamba hawa Suma JKT na wenyewe ambao hawasimamii ukusanyaji wa madeni waweze kuchukuliwa hatua na pesa za Serikali zisipotee. Hilo ni jambo muhimu sana kwa sababu uzoefu unaonesha kwamba mali ya umma inapotea hivi hivi kienyeji, lakini hiyo ni pesa ya Serikali na ni pesa ambayo inatakiwa irudi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati pia iliweza kupitia, utendaji kazi katika mashirika mbalimbali na Wizara mbalimbali. Ukiangalia ukurasa wa 25 wa kitabu cha wasilisho la PAC kipengele 2.2.6 ambacho kinazungumza ununuzi wa magari ya polisi yenye thamani ya dola za Marekani milioni
29. Jambo hili lina lenyewe lina utata mkubwa sana na utata wake ni kwamba pamoja na nia njema ya jeshi la polisi, lakini mkataba huo hauna maelezo yakinifu kuonesha kwamba uliingiwaje, ulifanyikaje na huo mkataba utamalizika lini, yaani hayo magari mengine, yatakuja lini. Kwa sababu ukisoma pale utaona idadi ya magari yaliyoletwa ni kidogo kulingana na yaliyohitajika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia mkataba huo wa Exim Bank ya India ambao uliingia ulifikia mahali ukawa ume- expire, hiyo credit facility ikawa ikawa ime-expire kabla ya utekelezaji wake kukamilika. Kwa hiyo sisi tunahoji tija ya mkataba huo na namna ulivyoingia na tunashauri kwamba lazima lifanyike jambo kubwa au maamuzi mazito kuhakikisha kwamba mkataba huo unakamilika na pesa za Serikali kuna mahali zilitolewa dola milioni 10 kama advance zijulikane ziko wapi. Kwa maana hiyo sisi tunaishauri Bunge tuweke azimio kuwe na reviw due deligency ya jambo hilo lote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, ukienda ukurasa 21, suala la TANESCO, TANESCO inawadai watu wengi madeni. Mashirika mengi yanadaiwa, tulizungumza tena hili jambo lishazungumzwa na linarudi tena kuzungumzwa na TANESCO hawa, wanaonekana wanahangaika sana lakini pesa ziko kwa wateja, sasa tunashindwa kuelewa kwamba tatizo ni nini na kwa nini hatua hazichukuliwi. Kamati ilipata mashaka sana, nami napata mashaka sana, kwa sababu mashirika mengi ofisi nyingi zinahamia Dodoma Makao Makuu na madeni yako Dar es Salaam, sasa wanahamia Makao Makuu huku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunaona ule msukumo wa kulipa madeni utakuwa ni mdogo, pamoja na kwamba, Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli alisema kama ni umeme kata sasa watakatiwa Dar es Salaam wanakuja kuanzia maisha huku upya, sasa jambo hilo na lenyewe inabidi liangaliwe ili liweze kuwa kuwa na tija. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua kwamba, jana tumepitisha hapa Sheria ya kuunganisha Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, lakini ukiangalia ukurasa wa 20 utaona madeni ambayo Serikali inadaiwa na mifuko ya jamii. Jambo hilo ni muhimu kwa afya ya Mifuko. Kwa hiyo, bado tunalishawishi Bunge liazimie kuona kwamba Serikali inalipa hayo madeni kikamilifu. Ukiona hilo jedwali linaonesha Mifuko na madeni na kiasi kinachodaiwa. Kwa hiyo, tunashawishi jambo hilo lifanyike kwa nguvu zote na Bunge liazimie kuona kwamba madeni haya yanalipwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba Mifuko hii wanasema ifanyiwe actuarial valuation, inakwisha sijui mwaka gani, yaani maisha yake bado inaonesha yana uhai, lakini Kamati inapata mashaka kama pesa hizi bado ziko Serikalini, sasa hata hiyo actuarial valuation inakuwa pia ina mashaka kidogo. Kwa hiyo, tunalishauri Bunge lione umuhimu lione umuhimu wa kuhakikisha kwamba madeni yanalipwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda ukurasa wa 37 umiliki wa taasisi ya ukuzaji maendeleo Pride Tanzania Limited, hapa Kamati kwa kauli moja inasema tu Pride Tanzania, irudi Serikalini kwa sababu ndiyo iliyotoa mtaji mkubwa, lakini baadaye ikahamishwa inaendeleshwa na utaratibu na watu wengine. Kwa hiyo, tunasema pride irudi kwa sababu mtaji ulitoka Serikalini. Kwa hiyo, tunaomba Bunge na Wabunge wenzetu tutakapofika kwenye maazimio, tuone umuhimu wa pride kurudi Serikalini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho katika kuchangia leo nataka nizungumze kidogo kuhusu bandari, na TRA uhusiano wake wa kutokurejeshwa kwa mapato ya wharfage. Jambo hilo ni muhimu sana kwa sababu bandari zetu zinaendelezwa kwa hizo pesa, ambazo pesa hizo kimsingi zinakusanywa na TRA, lakini tunatambua kwamba TRA ni wakala tu na pesa zinakwenda moja Benki Kuu, Hazina wanatakiwa warudishe hizo pesa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tungependa labda Waziri mhusika atakapojibu hoja aseme kwamba kwa nini pesa hizi hazirudishwi, kwa sababu tunatambua kwamba kuna pesa nyingi hazijarudishwa ambazo zingetumika kwa maendeleo ya bandari zetu.

Mhemishiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi na naomba Bunge likisoma maazimio tuyapokee maazimio yote kwa pamoja.