Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Dr. Ashatu Kachwamba Kijaji

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Kondoa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyetuwezesha kufika siku hii ya tano ya mjadala huu muhimu sana kwa maendeleo ya Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, napenda na mimi nimshukuru Mheshimiwa Rais wetu kwa kuendelea kuniamini na kuniacha katika nafasi hii ya Naibu Waziri wa Fedha na Mipango ili niweze kuendelea kumsaidia Mheshimiwa Waziri pamoja na yeye Mheshimiwa Rais wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia nikushukuru wewe kaka yangu Job Ndugai kwa kazi nzuri ambayo unaendelea kuifanya ya kuendesha Bunge letu Tukufu. Kwa kweli hongera sana kaka yangu, Mwenyezi Mungu azidi kukubariki ili tuweze kuifanya kazi hii tuliyoaminiwa na Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia niwapongeze Waheshimiwa Wabunge wa Bunge lako Tukufu kwa michango yao mizuri ambayo wametupatia sisi kama Wizara ya Fedha ili kuboresha Mapendekezo ya Mpango na tunapokuja mwezi wa Machi/Aprili na Mpango kamili tuweze kuja na Mpango ambao upo imara. Ninaamini wote kwa pamoja wametimiza wajibu wao Kikatiba wa nini walitakiwa kufanya na niwapongeze sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Wizara tumeyachukua yote, mimi na Mheshimiwa Waziri hatuwezi kujibu michango yote ya Wabunge zaidi ya 100 waliochangia kwa siku 5. Tutazungumzia machache ili tuweze kuendelea mbele kwenda kuandaa Mpango wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa uniruhusu nianze kuchangia hoja hii iliyowekwa Mezani na Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango, kaka yangu, Mheshimiwa Philip Isdor Mpango. Nianze kwa kukupongeza Mheshimiwa Waziri wa Fedha, kazi yako ni njema sana, kazi yako ni nzuri na imeonekana ndiyo maana Mheshimiwa Rais ameendelea kukuamini, hongera sana kaka yangu, simama hivyo hivyo. (Makofi)

Sisi watumishi tulio chini yako wewe ndani ya Wizara ya Fedha na Mipango tunajivunia kufanya kazi na wewe. Kwa wale ambao walikuwa hawajui uchumi sasa wanaufahamu uchumi ndani ya Wizara ya Fedha, nikupongeze sana Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ya kwanza ambayo napenda kuitolea ufafanuzi ni hoja ambayo ilisema Serikali ione umuhimu wa kufanya malipo ya wakandarasi ambao wametekeleza miradi mbalimbali ndani ya Taifa letu. Serikali yetu ya Awamu ya Tano inatambua sana umuhimu wa kazi zinazofanywa na wakandarasi, lakini pia umuhimu wa kuwalipa malipo yao kwa muda mwafaka ili waweze kuendelea kufanya kazi zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha wa 2016/2017 Serikali imeweza kufanya malipo ya shilingi bilioni 3,358.89 kwa ajili ya wakandarasi, kati ya hizo, shilingi bilioni 1,321.47 zililipwa kama madeni ya wakandarasi waliojenga barabara zetu. Tunalipa lakini la muhimu kama ambavyo tumeendelea kusisitiza lazima uhakiki ufanywe ili tujiridhishe nini tunalipa kama Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kati ya kiasi hicho nilichotaja, shilingi bilioni 1,161.32 kililipwa kwa ajili ya Mfuko wa Reli. Kama ambavyo Serikali yetu imedhamiria kuboresha miundombinu ndani ya Taifa letu na tumeanza kulipa, shilingi bilioni 204.90 zililipwa kwa ajili ya Mfuko wa Maji kwa wakandarasi wetu ambao wamefanya kazi ndani ya Wizara ya Maji. Mwenyekiti hili ulilisema na Waheshimiwa Wabunge walilisema kwa wingi kwamba Mheshimiwa Waziri haangalii ni maswali yapi ambayo yakiulizwa wanasimama Waheshimiwa Wabunge wangapi. Sasa hili naomba kulidhihirishia Bunge lako Tukufu kwamba kama Serikali tumekuwa tukilipa na shilingi bilioni 204 zimelipwa kwa mwaka 2016/2017. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo pia limepigiwa kelele na kama Serikali tunaendelea kulipa na nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri wa Nishati, amesema vizuri na ametoa order nzuri sana na kwa mwaka 2016/2017 tulilipa shilingi bilioni 537.95 kwa ajili ya Mfuko wa Umeme Vijijini kuhakikisha vijiji vyetu vyote vinapatiwa umeme wa kutosha. Shilingi bilioni 133.24 tulilipa wakandarasi walioshughulika na miradi ya viwanja vya ndege. Tumesikia kelele nyingi zikipigwa kwa ajili ya shilingi bilioni 39 tu, hapana, tumelipa zaidi ya hizo kwa sababu zilikuwa ndani ya bajeti yetu ya mwaka husika. Kwa hiyo, nilidhihirishie Bunge lako Tukufu kwamba tumekuwa tukifanya malipo haya kwa ajili ya wakandarasi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika robo ya kwanza ya mwaka huu wa 2018/2019 tumelipa pia shilingi bilioni 562.29 kwa robo ya kwanza tu kwa wakandarasi wanaohusika na miradi mbalimbali ndani ya Serikali yetu. Kwa hiyo, nataka kusema kwamba dhamira ya Serikali yetu ni njema sana katika kuhakikisha kwamba watu wote wanaofanya kazi na Serikali yetu wanalipwa malipo yao yale wanayostahili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na jambo hili, liliongelewa pia suala la Serikali kuchukua kodi ya majengo na ni kiasi gani ambacho tumeweza kukusanya kwa Mamlaka ya Mapato na hili aliliongelea vizuri sana kaka yangu Mheshimiwa Lubeleje.

Napenda kusema kwamba katika ukusanyaji wa Kodi ya Mapato niliambie Bunge lako Tukufu kwamba hatukunyang’anya Halmashauri zetu chanzo chake cha mapato. Nasema hivyo kwa sababu moja kubwa, dhamira ya Serikali ya kuchukua chanzo hiki ilikuwa ni kuongeza ufanisi wake ili sasa tuone ni jinsi gani tutaweza kuzirejesha pesa hizi katika Halmshauri zetu. Kwa mwaka 2016/2017 kwa Halmashauri 30 tu tumeweza kukusanya shilingi bilioni 34.09 ukilinganisha na shilingi bilioni 28 ambazo zilikusanywa na Halmashauri husika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilisema dhamira ilikuwa ni kuongeza ufanisi na ufanisi tumeuongeza zaidi ya asilimia 20 lakini ukiangalia Mamlaka ya Mapato Tanzania ilianza kukusanya kodi hii mwezi Oktoba. Kwa hiyo, nilidhihirishie Bunge lako Tukufu kwamba kwa mwaka huu ambao tumeanza tangu mwezi Julai, mapato yetu kutoka Kodi ya Majengo yatakuwa ni mazuri sana. Mifumo yetu imekamilika, tumeanza kufanya kazi kwa umakini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ambalo lilikuwa linaulizwa kuhusu hili ni kwamba zimerejeshwa kiasi gani? Kama nilivyosema, dhamira kuu ilikuwa kuongeza ufanisi lakini kuhakikisha pesa hizi zinarejea kwa wananchi kwenda kufanya kazi. Baada ya kuzikusanya shilingi bilioni 34.09 pesa zote zilirejeshwa kulingana na bajeti za Halmashauri zetu kama Sheria yetu ya Fedha tuliyopitisha ilivyotuelekeza. Kwa hiyo, katika hili pia napenda kulieleza Bunge lako Tukufu kwamba hayo ndiyo mambo ambayo Serikali yetu ya Awamu ya Tano inayafanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine ambayo napenda kuitolea ufafanuzi ilikuwa ni kuhusu Serikali kutounga mkono sekta binafsi kwa kuwa Mapendekezo ya Mpango hayaongelei sekta hiyo wala kuainisha miradi ambayo Serikali itashirikiana na sekta binafsi katika kuitekeleza. Nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri wa Viwanda amelielezea suala hili lakini pia niwaombe Waheshimiwa Wabunge ni muhimu wanapokuja kuchangia wawe wamepitia Mpango kuanzia page ya kwanza mpaka ya mwisho kuliko kuja kutuhumu bila kuwa na facts wakizifahamu. Hilo ni jambo la msingi sana. Nilichoki-note, watu wanasoma hotuba ya Mheshimiwa Waziri halafu wanakuja kuchangia Bungeni, hapana, hotuba ya Mheshimiwa Waziri ni summary ya kitabu kizima cha Mapendekezo ya Mpango, kwa hiyo wakipitie kwa umakini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nasema hivi? Nasema hivi kwa sababu ndani ya Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2018/2019 tumeainisha sekta binafsi itahusika na miradi ipi na katika awamu ipi. Tumeonesha waziwazi kabisa ukurasa wa 26 hadi 28 wa Mapendekezo ya Mpango, tumeonesha sekta binafsi ilivyoshirikiana na Serikali kutekeleza bajeti yetu ya 2017/2018. Tukatoka hapo, ukurasa wa 58 hadi 59 tukaainisha sasa kwa haya Mapendekezo ya Mpango tunayokwenda nayo, Mpango wetu unaokuja tunataka sekta binafsi ishiriki katika miradi ipi. Kwa hiyo, ndiyo maana nimesema wawe wanapitia kitabu kile tulichokileta Bungeni kwa ajili ya kujadili hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali yetu kwa kutambua umuhimu wa sekta binafsi katika kuleta maendeleo, hatukuishia tu kuainisha baadhi ya miradi lakini tumekwenda mbele na kuainisha na mikakati ni jinsi gani sekta binafsi na Serikali zitashirikiana ili tuweze kufanya kazi pamoja. Kwa hiyo, niombe sana hilo lifanyike.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini katika hoja hiyo liliongelewa pia suala zima la kwa nini Serikali inawekeza kwenye miradi mikubwa ya maendeleo ikatolewa mfano mradi wa reli yetu ya kati (Standard Gauge Railway), ukatolewa mfano pia mradi wa Stiegler’s Gorge kwa ajili ya kuzalisha nishati ya umeme. Katika hili, naomba niseme jambo moja, ipo katika dunia nzima katika uchumi kwa nchi ambazo zimeendelea na sisi tunaendelea kuendelea, miradi hii ya miundombinu huwa ina sifa zake kuu tatu au nne ambazo ndizo zinazotoa mwelekeo kwamba ni nani atawekeza katika miradi ya miundombinu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe Waheshimiwa Wabunge hasa waliosema katika jambo hili, waende wakasome The Economics of Infrastructure Projects ili waweze kuelewa. Katika economics of infrastructure projects, Maprofesa wabobezi wa uchumi wanasema miradi yote ya miundombinu ambayo ni ya kimkakati duniani kote huwa ina hatua zake tatu. Hatua ya kwanza, huwa ni planning phase, hatua ya pili huwa ni construction na hatua ya tatu huwa ni operation. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika planning phase wabobezi wa uchumi wanasema miradi hii, naomba ku- quote, sifa moja katika planning phase ni nini kilichopo. Wanasema; many strategic infrastructure projects generate cash flows after many years, and the initial phase of this project is subject to high risks. Hii ina maana kwamba miradi yetu hii ya miundombinu ya kimkakati katika initial phase huwa ina risk kubwa sana na risks hizi hakuna kampuni yoyote ya binafsi ambayo iko tayari kuchukua risk hii katika initial phase ya miradi hii. Ndicho ambacho Serikali yetu imeona nini cha kufanya, lazima uoneshe nia wewe kama Serikali. Tunaihitaji miradi hii, tunahitaji Standard Gauge Railway, nani wa kuwekeza kwa sifa hizi, hayupo, except the government itself. Katika hili, tumeanza vizuri na imeanza Serikali yetu at the initial phase, the planning phase, we planned, sasa hivi tuko kwenye construction phase, tunafanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sifa ya pili ya miradi hii ya kimkakati, hasa ya miundombinu, wachumi wabobezi wanasema; even though the direct payoffs to an owner of an infrastructure project may cover its costs, the indirect externalities include beneficial for the economy as a whole. Nini maana yake? Inamaanisha kwamba sawa gharama zake ni kubwa na risks zake ni kubwa lakini miradi hii ya miundombinu ina faida nje ya ile sekta husika. Sasa hivi tulikuwa tukilalamika mahindi yanayozalishwa Sumbawanga hayawezi kusafiri, Serikali ime-invest kwenye miundombinu ya barabara sasa mahindi yetu yanaweza kusafiri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kaka yangu Mheshimiwa Lubeleje, amelalamika asubuhi kwamba mahindi kule kwake Mpwapwa hayapo. Kwa infrastructure zilizowekezwa na Serikali ndugu zangu wa Mpwapwa watapata mahindi kwa bei nafuu. Ndiyo maana ya Serikali kuwekeza katika infrastructure projects kubwa kama standard gauge katika initial phase na construction phase lazima Serikali iweke mkono wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, faida hizi ni kubwa kama nilivyosema. Kwa hiyo, la msingi, tunapokwenda kwenye operational phase ambapo sasa tayari miradi hii itaanza ku- generate revenue, cash flow inaingia, ndipo utakapoyaona makampuni binafsi yanaingia ili sasa kuweka mabehewa mazuri kwa ajili ya kusafirisha wananchi wetu na bidhaa zao. Hakuna kampuni au mfanyabiashara ambaye anakuja kuwekeza akijua ataishi yeye, atakufa, ataishi mtoto wake atakufa halafu awekeze mtaji, hilo halipo. Ni Serikali tu kwa sababu ya faida pana ya mradi husika kwenye uchumi, tunataka kujenga nini, uchumi wa viwanda, bila standard gauge hatuna uchumi wa viwanda. Ndiyo maana Serikali yetu imefanya hicho ambacho tumekifanya. Niwaombe Waheshimiwa Wabunge waendelee kutu-support ili tuweze kufanya kazi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala hilo, naungana kabisa asilimia 100 na kaka yangu, Mheshimiwa Bashe, aliposema economics is not a rocket science, we agree a hundred percent. Economics is not a rocket science but economics is a social science, you need to understand the agency you are dealing with, the behavioral economics, unafanya kazi na watu gani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wifi yangu anasema nirudie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema naungana na Mheshimiwa Bashe aliposema economics is not a rocket science, that’s quite right lakini economics is a social science, unahitaji nini, unahitaji kuelewa the social actors you are dealing with. Unakaa chini unaendelea kusubiri Stiegler’s Gorge tangu alivyouanzisha Mheshimiwa Baba wa Taifa letu, Mwalimu Nyerere mpaka leo hakuna mwekezaji aliyejitokeza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii Serikali imeanza kuwekeza Stiegler’s Gorge, tutakapoanza initial phase, the construction phase, operational phase, tutapata wawekezaji na uchumi wetu utaruka, that’s where now the rocket science will come, not at the initial phase. Niwaombe sana na mimi napenda kusema katika jambo hili sababu tunayo, nia tunayo, dhamira tunayo na uwezo tunao wa kuwekeza katika miradi mikubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema dhamira tunayo, sababu tunayo na uwezo tunao kwa sababu bado hatujafika asilimia zaidi ya 40 ya kukopa kwa ajili ya maendeleo ya Watanzania. Tukope, tuwekeze ili Watanzania wafikiwe na maendeleo kule walipo. Kama tungekuwa tunakopa na kulipana posho tungeweza kuogopa, lakini tunakopa tunawekeza kwenye standard gauge tusafirishe bidhaa zetu. Tunakopa tuwekeze kwenye Stiegler’s Gorge tuzalishe umeme wa kutosha viwanda vya shemeji yangu, Mheshimiwa Mwijage, vifanye kazi, hatuna sababu ya kuogopa. Mheshimiwa Waziri wa Fedha, niko na wewe nitafanya kazi pamoja na wewe katika jambo hili, naamini hilo limeeleweka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niende kwenye hoja nyingine ambayo ilisemwa na Kambi Rasmi ya Upinzani, wakasema kwamba Serikali inafanya matumizi ya fedha ambazo hazikuidhinishwa na Bunge kinyume na utaratibu wa Sheria ya Fedha ya Matumizi ya Umma ya 2011. Napenda kwanza kukanusha hiki kilichosemwa na Watanzania wafahamu Serikali yao ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Chama cha Mapinduzi iko makini katika kutekeleza sheria zake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatujafanya jambo hilo, hata siku moja. Kitu ambacho wanasahau ndugu zetu hawa na kuja kudanganya wananchi, Mheshimiwa Waziri wa Fedha kapewa mamlaka ya kufanya uhamisho kutoka kifungu kimoja kwenda kwenye kifungu kingine, amepewa hiyo dhamana. Mheshimiwa Silinde, sikiliza nikufundishe uchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri wa Fedha amepewa hayo mamlaka, anayo mamlaka, labda kama mnataka kumpoka lakini anayo hayo mamlaka. (Makofi)
Anafanya reallocation kutoka kifungu kimoja kwenda kifungu kingine ndani ya bajeti ya Serikali iliyopitishwa na Bunge lako.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, naomba nim-quote kaka yangu Jafo alivyosema wanaanza kupata kiwewe kwamba hawezi kutukamata wapi tunakwenda. Hii speed siyo ya kawaida hakuna wa kutusogelea ndugu zangu. (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee kutoa darasa, Sheria ya Bajeti kifungu cha 48 kinampa mamlaka hiyo Waziri wa Fedha, kikisomwa pamoja na Kanuni zake, Kanuni ya 26(1) inamwelekeza Mheshimiwa Waziri wa Fedha nini cha kufanya. Kanuni ya 26(2) inamwelekeza aweze kufanya reallocation kwa kiwango gani, ndicho ambacho amekuwa akifanya Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Serikali yetu haijawahi kutumia fedha hizi nje ya bajeti iliyopitishwa na Bunge lako Tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja hiyo inaunganishwa na naona ndicho wanachokitafuta lakini wanashindwa kufika, kwamba Serikali sasa ilete Bungeni adjustment ya bajeti kwa sababu wamesahau mamlaka haya ya Waziri. Naomba niseme jambo moja, nini maana ya bajeti ya nyongeza?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhamisha kifungu hiki, kupeleka kifungu hiki siyo bajeti ya nyongeza ndugu zangu. Maana ya bajeti ya nyongeza ni kwamba Serikali ndani ya mwaka husika imekusanya mapato ya ziada ambayo hayakupitishwa na Bunge lako Tukufu na sasa inataka kuyafanyia matumizi. Hiyo ndiyo bajeti ya nyongeza ambayo Mheshimiwa Waziri wa Fedha kama anataka kutumia hayo mapato ya ziada tutalazimika kuja kwenye Bunge lako lakini kwa reallocation of funds between votes tunatakiwa tu tunapokuja hapa katika mid year review tu-report nini tumefanya, wala siyo kuleta bajeti ya ziada, hatuna bajeti ya ziada ndugu zangu. Tuko ndani ya bajeti iliyopitishwa na Bunge, ndani ya matumizi husika, tunatumia katika miradi yetu ya kipaumbele ndani ya Serikali yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri tukawa na uelewa wa pamoja wa Sheria tunazopitisha sisi wenyewe halafu tunaposimama tuseme kwa Watanzania nini Serikali inafanya kwa niaba yao. Hilo ni jambo la msingi sana nilitaka kuliomba Bunge lako Tukufu tukubaliane na hiki ambacho kiko ndani ya Sheria iliyopitishwa na Bunge lako Tukufu na siyo kuja hapa na kuwadanganya Watanzania kwamba Mheshimiwa Rais anatoa order, hawezi kutoa order bila kujua hiyo pesa ipo na ilipitishwa na Bunge lako Tukufu. Hilo ni jambo la msingi sana katika utekelezaji wa shughuli za Serikali yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine ambayo iliongelewa kwa uchungu na kwa sauti kali ilikuwa ni kwamba Mipango ya Maendeleo ya mwaka 2016/2017, 2017/ 2018 na 2018/2019 yote inafanana. Nianze kwa kukuomba kwamba tuwe tunapitia vitabu hivi ili tuweze kujua lakini tusisahau msingi wa mipango hii mitatu na sasa tumebakisha mipango mingine miwili ni Mpango wa Pili wa Maendeleo wa miaka mitano. Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano ndiyo unatupa sisi base ya miradi ipi itekelezwe, kwa kiwango kipi na imeelekezwa kabisa. Ukichukua Mpango ule wa Miaka Mitano mimi nausoma vizuri sana na baada ya kusikia hili nilienda nikarudia kusoma mara mbili, mara tatu kuna nini? Nikagundua miradi mingi iliyopo kwenye Mpango wa wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano inatekelezwa kwa kipindi cha kuanzia miaka mitatu mpaka mitano, nini maana yake? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2016/2017 tulileta mradi ule ukiwa katika initial phase, mwaka 2017/2018 tumeleta mradi ule katika hatua zake za mwanzo za utekelezaji, mwaka 2018/2019 tunaleta sasa wapi tumefika baada ya kufika nusu ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa miaka mitano, miradi ni ile ile. Tofauti ya miradi hii inayoripotiwa ni utekelezaji wake hatua moja kwenda hatua nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tukianza ku-crash miradi ambayo ipo kwenye Mipango yetu ya Maendeleo ya mwaka mmoja tunawambia nini Watanzania? Hatukuwa makini kupitisha Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano kwa sababu hakuna sehemu Waziri wangu wa Fedha anaweza kwenda kuchukua mradi ambao hauko kwenye Mpango wa Pili wa Maendeleo.

Kwa hiyo, lazima tulifahamu hilo, twende tusome content of the document not what the Minister has presented in the Parliament, tutapata content na tutaelewa sasa wapi tupo na miaka mwili inayobaki nini tutafanya, je, tutaweza kutimiza kile tulichodhamiria? Hicho ndicho kilichopo, ukisoma tu bila kubeba jicho la planning ndani ya mipango hii utagundua hatuna utofauti ndani ya mipango yetu lakini ukiweka jicho la planning (the planners) utaona nini kilichopo ndani ya mipango yetu na wapi tunaelekea sasa katika kuhakikisha Tanzania ya viwanda tunaifikia kabla ya mwaka 2020. Dhamira yetu ni moja tu, kabla ya mwaka 2025 tunahitaji kuona Watanzania wenye kipato cha kati, kabla ya mwaka 2020 tunadhamiria kuona Watanzania wa Tanzania ya viwanda, hilo ndiyo jambo la msingi na ndiyo kazi tunayoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya niseme jambo lingine ndogo ambalo liliongelewa katika ile ile hoja ya kupotosha Watanzania na nini Serikali yetu inafanya. Ilikuwa ni hoja kwamba Serikali imeendelea kudharau mamlaka ya Bunge lako Tukufu kwa kuacha kuleta sheria ya kusimamia mipango tunayopitisha ndani ya Bunge lako. Naomba kusema Serikali yetu ni sikivu sana hasa Serikali ya Chama cha Mapinduzi inayoongozwa na Mheshimiwa John Pombe Magufuli. Ni Serikali sikivu sana na hatuna ujanja huo wa kulidharau Bunge lako. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kusema kwamba, katika hili turejee kwenye Sheria ya Bajeti Na.11 ya mwaka 2015, kwa nini ilitungwa Sheria ya Bajeti, ni kusimamia mipango na bajeti tunayopitisha humu ndani. Tunahitaji sheria nyingine ipi na kufanya lipi? Pia kwa kila mwaka tuna Appropriation Act kwa ajili ya kusimamia matumizi ya Mpango tunaojadili leo, sasa tunahitaji sheria nyingine kufanya nini? Hatuhitaji sheria nyingine. Tunayo Sheria ya Bajeti na tunayo Appropriation Act ya kila siku. Sheria ya Bajeti inatuwezesha kubainisha kisheria majukumu na mipaka ya kiutendaji ya wahusika wakuu katika mchakato mzima wa kibajeti na kimpango. Sheria ya Bajeti inaweka uwiano kati ya mipango yetu, mapato yetu na matumizi yetu, tunahitaji sheria nyingine ya kufanya nini? Sheria ya Bajeti pia inaweza kutueleza na sisi tukatambua mzunguko wa kisheria wa kibajeti nini kilichopo, tungekaa tukaisoma vizuri wala tusingefika sehemu ya kuja na personal issues za kumtuhumu Waziri wa Fedha hata siku moja, turejee tu kwenye sheria tunazozipitisha sisi wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, naomba nikushukuru kwa kupata nafasi hii. Kama nilivyosema mwanzo yako mengi tutayafanyia kazi kwa umakini yote kwa pamoja na tutakuja na Mpango unaoakisi mapendekezo mazuri yaliyotolewa na Wabunge hasa wa Chama changu, Chama cha Mapinduzi walioongea mengi kwa ajili ya kuboresha Mpango wetu. Yale machache ya upande wa pili tutayachukua yale mazuri, yale mabaya naomba tuyaache humu humu tunapotoka tutoke na ushirikiano wetu na udugu wetu ili tuweze kutekeleza azma ya Serikali yetu na Hapa Kazi Tu itafanikiwa. Ahsante sana.