Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Dr. Medard Matogolo Kalemani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chato

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nianze kwa kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuniamini na kuniteua kuwa Waziri kamili wa Nishati, Wizara ambayo ni mpya. Ninapenda kuchukua nafasi hii kuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote, hata mimi kuwa Waziri wa Nishati nadhani ni kwa sababu ya mikono ya Waheshimiwa Wabunge hawa, kwa jinsi ambavyo tumeshirikiana sana awamu iliyopita katika masuala yote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwa juhudi ambazo mlikuwa mnatupa na ushirikiano wenu, tunaamini sasa tutashirikiana zaidi katika safari inayofuata. Hongereni sana Waheshimiwa Wabunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kutekeleza Mpango wa Maendeleo wa miaka mitano, Wizara yetu mpya ya Nishati inayo vipaumbele ambavyo ni vya msingi sana katika kujenga uchumi wa viwanda. Tunatambua kama Serikali kwamba uchumi ni nishati, viwanda ni nishati na maendeleo ni nishati, bila nishati hakuna maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baadhi ya vipaumbele ambavyo kwa kweli vimezungumzwa vizuri sana na Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango ambavyo ninapenda kurejea kwenye michango ni pamoja na miradi mikubwa ya kuzalisha umeme. Hivi sasa tuna mkakati mkubwa wa kuzalisha umeme wa kujitosheleza kujenga uchumi wa viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa umeme tulionao unatosha kwa mazingira ya sasa, lakini hauwezi kutosheleza kwa mwendo kasi wa kujenga uchumi tunaokwenda nao. Kwa hiyo, juhudi kubwa tumezielekeza katika kuzalisha umeme ili sasa utumike vizuri kwenye kujenga uchumi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi mkubwa wa kuzalisha umeme tulionao kwa sasa ni Mradi wa Kinyerezi Namba Moja na Kinyerezi Namba Mbili. Mradi huu tuna matarajio utakamilika soon, mwezi Agosti, 2018 miradi miwili itakamilika na kutuingizia sasa jumla ya megawati 425. Huu ni umeme mkubwa, kama utaingia kwenye Gridi ya Taifa utachangia sana kwenye kujenga uchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kuishukuru sana Serikali kupitia kwa Mheshimiwa Rais na Serikali yetu kwa kupitisha uamuzi wa kujenga umeme wa maji kupitia Stiegler’s Gorge ya Mto Rufiji. Huu ni umeme mkubwa ambao utatuzalishia megawati 2100. Taratibu za kuanza kuujenga mrdai huu zimeshaanza, hivi sasa tumeshatangaza tender na waombaji zaidi ya 80 wamejitokeza, kesho tunaanza kufungua sasa kuanza kufanya evaluation.

Mheshimiwa Mwenyekiti, matayarisho ya ujenzi wa mradi huu yatakamilika mwezi Disemba mwaka huu na mwezi Januari tunaanza kuujenga. Kwa hiyo, kufikia mwaka 2020 tutaingiza kwenye Gridi ya Taifa megawati nyingine 2100. Tujipongeze sana kwa mradi huu mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi huu ulichelewa kidogo kwa sababu kubwa mbili; ya kwanza, kulikuwa na masuala ya mazingira, katika awamu hii sio kwamba tunapuuza mambo ya mazingira, tutaenda nayo lakini huku tukiharakisha ujenzi wake. Jambo la pili, mradi huu huko nyuma uliwekwa chini ya RUBADA, kazi ya RUBADA kimsingi haikuwa kuzalisha umeme, ilikuwa ni ku-reserve mambo ya mazingira na vyanzo vya maji lakini baada ya Serikali kuamua kwamba mradi huu upelekwe kwenye Wizara inayoshughulika na masuala ya nishati, Serikali tumeuchukua na ndiyo maana tutaharakisha ujenzi wake. Kwa hiyo, niwape uhakika wananchi na Waheshimiwa Wabunge kwamba mradi huu utajengwa kuanzia Januari, 2018.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipaumbele chetu cha pili, pamoja na mambo mengine, ni ukamilishaji wa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima, Uganda kuja Tanga, Tanzania. Kama mnavyokumbuka, niwapongeze sana Waheshimiwa Wabunge, mwezi Septemba 2017 mlipitisha mkataba wa nchi mbili ili uanze kutekelezwa. Tunawashukuru sana kwa sababu baada ya hapo ujenzi umeshaanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi huu kama ambavyo nimeeleza ni mradi mkubwa. Hapa nchini kwetu utahusisha Mikoa minane ambapo utapita katika Mikoa ya Geita, Tabora, Shinyanga, Singida, Dodoma, Manyara na hatimaye Tanga. Kama ambavyo nimekuwa nikieleza mara zote, mradi huu, nasema utakuwa na impact kubwa kwa sababu unapita katika Wilaya nyingi sana, unapita katika Wilaya 24 katika Mikoa niliyoitaja, kadhalika unapita katika vijiji 134 na unapita katika vitongoji 210. Sasa unaweza ukaona manufaa yake itakavyokuwa kwa Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kokote mradi utakapopita utakuwa na fursa kubwa sana za kiuchumi kwa Watanzania na wawekezaji wengine. Kwa hiyo, mradi huu ujenzi wake unaanza pia mwezi Januari utakapokamilika ndani ya miaka mitatu, fursa kubwa sana za kiuchumi zitakuwa zimeongezeka katika nchi yetu. Kwa hiyo, nilitaka kutoa taarifa kwamba haya ni maendeleo mazuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na juzi tuikuwa Uganda, tumekamilisha uwekaji wa bomba na kwa upande wetu tulishakamilisha, sasa kazi inayofanyika ni kukamilisha majadiliao kati ya Serikali na wawekezaji. Hatua inayofuata ni kuingia mkataba wa ubia na ujenzi kuanza mara moja; huo ulikuwa ni mradi wa pili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa tatu ni Mradi wa Uchakataji Gesi (LMG), huu ni mradi muhimu sana kama ambavyo mnausikia. Upo uvumi kwamba inawezekana mradi huu haupo, niseme kwa niaba ya Serikali; msimamo wa Serikali wa kujenga mradi huu uko palepale. Sasa kinachofanyika, pamoja na mambo mengine, tumeshapata eneo, tumeshafanya tathmini ya wale watakaoathirika na kutakiwa kufidiwa, lakini kazi inayofanyika sasa ni kukamilisha majadiliano ya uwekezaji, hatua inayofuata ni kuingia makubaliano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi nyingine iliyokamilika ni kupata eneo ambalo kinu kitajengwa kwa ajili ya kuchakata hiyo gesi. Kwa hiyo, hatua zinakwenda vizuri, na kesho nitakutana na wadau wote watakaojenga mradi ule kama Oil4All, Big Shell na makampuni mengine ili taratibu za kuanza kujenga zianze mara moja. Kwa hiyo, ule uvumi wa kwamba mradi huu umetelekezwa, Serikali iko makini sana na mradi huu na lazima utekelezwe kwa nguvu zote. Kama Waziri wa Wizara hii pamoja na Naibu wangu, tutausimamia mradi huu kwa makini sana mpaka utakapokamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, matumizi ya gesi viwandani. Kama mnavyojua imechukua muda mrefu sana, hasa viwanda vya mbolea na vingine vya mkakati kupewa gesi, ninapenda kutoa taarifa kwenye kikao chako kwamba wiki mbili zilizopita tumekamilisha makubaliano kati ya Serikali
na Ferrostaal, sasa wako tayari kuja kuwekeza wamekubaliana na bei ya Serikali. Walichoomba ni kupata unafuu wa masuala machache ya kodi. Sasa tumeshaanza kukamilisha makubaliano nao, tunachofanya ni kupitia maombi yao ili baada ya kukamilika waanze kuwekeza. Kwa hiyo, maeneo ya Kilwa Masoko kutajengwa kiwanda kikubwa cha mbolea chini ya ujenzi wa Ferrostaal kuanzia sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Mtwara bado tunaendelea kuzungumza na HELM na wenyewe wanaonesha nia ya kukubaliana na Serikali ili sasa nao waingie katika utaratibu wa kujenga. Kwa hiyo, viwanda vya kimkakati vitaanza kujengwa sasa kwa sababu tunakwenda kwa kukubaliana pamoja.

Mradi mwingine ni wa usambazaji umeme vijijini wa REA. Tunaposema ujenzi wa viwanda, havijengwi mjini peke yake. Serikali imedhamiria viwanda vianze kujengwa kuanzia vijijini na hakuna njia ya kujenga viwanda vijijini kama hujawapelekea wananchi umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati wetu uko palepale, kama ambavyo tumeeleza, majibu mengi yametolewa na Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini mimi nifafanue kwa urefu zaidi. Kwamba mradi huu kama ambavyo tumekuwa tukisema tumeanza kuutekeleza. Na nitoe rai na tamko kwa wakandarasi wote, tunataka ifikapo tarehe 20 mwezi huu, wakandarasi wote wa REA wawe wamesharipoti katika maeneo yao na mkandarasi yeyote abaye atakuwa hajafika kwenye eneo lake na kuanza kazi ifikapo tarehe 20 mwezi huu atakumbwa na kimbunga kikali kweli kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kusema kwamba Mpango wa Maendeleo wa miaka mitano kuwapelekea umeme wananchi kwa ajili ya kujenga uchumi tunakwenda nao vizuri. Vijiji vyote 7,873 vitapatiwa umeme katika awamu hii ya kwanza tunaanza na vijiji 3,359 lakini baadaye tunamalizia na vijiji 4,320, vyote vitapelekewa umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo maeneo ya mitambo ya maji ambayo tumedhamiria kuyapelekea umeme ili kurahisisha shughuli zao. Kule Karatu tayari vile visima walivyokuwa wameomba tumewapelekea umeme na tunataka kupeleka visima vya maji maeneo ya Mara na mikoa mingine. Lakini maeneo yote ambayo kutakuwa na mitambo ya maji niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge mtupatie orodha ya maeneo hayo ili tuanze kuyapelekea umeme mapema iwezekanavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie tu na mradi wa kusambaza gesi majumbani. Huu mradi ulikuwa unafanyiwa tathmini, tathmini imekamilika, hivi karibuni tutatoa tenda kwa ajili ya kuanza ujenzi. Kadhalika tumezungumza na wadau mbalimbali wanaounga mkono juhudi kwa ajili ya kujenga viwanda hivi. Tutaanza na Mkoa wa Dar es Salaam ili kupunguza matumizi ya mkaa. Tutaanza kusambaza Dar es Salaam kwa kaya 3,000 na baadaye tutahamia Mtwara na Lindi na baadaye tutakwenda katika Mikoa ya Dodoma, Morogoro, Singida na hatimaye katika mikoa yote ya Tanzania Bara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, itoshe tu kusema naunga mkono hoja, Wizara ya Nishati itapambana kwa niaba ya Serikali kuhakikisha kwamba uchumi wa viwanda unajengwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.