Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Eng. Atashasta Justus Nditiye

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muhambwe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, kwa jitihada zake mbalimbali za kuisogeza nchi yetu katika uchumi wa kati. Nampongeza vilevile Waziri wa Fedha na Mipango, Mheshimiwa Dkt. Mpango, kwa mpango mzuri sana aliouleta, ambao ni mpango endelevu kwa ajili ya Serikali, unaolenga Mpango wa Serikali wa miaka mitano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii vilevile kuwashukuru wachangiaji mbalimbali Waheshimiwa Wabunge waliochangia Mpango huu kwa nia njema kabisa, lakini niwashukuru kipekee wale waliochangia kwenye sekta ya ujenzi, uchukuzi na mawasiliano.

Mheshimwa Mwenyekiti, kipekee kabisa napenda niongelee masuala makuu manne, nitaongelea masuala ya reli, nitaongelea masuala ya barabara, nitaongelea masuala ya bandari na mwisho nitagusia kidogo masuala ya viwanja vya ndege. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ina mpango mkubwa sana wa ujenzi wa reli mpya kwa kiwango cha standard gauge, kila Mbunge anajua na kila mwananchi anafahamu. Serikali ya Awamu ya Tano inatarajia kujenga jumla ya kilometa 4,886 ambazo kiujumla kabisa zitajumuisha kanda kuu tatu, tutakuwa na Ukanda wa Kati ambao utajumuisha mikoa ya Dar es Salaam, Isaka, Mwanza ambayo ni kilometa 1,219 lakini vilevile tutakuwa na Ukanda wa Kaskazini ambao tutakuwa na reli ya kutoka Tanga, itapita Arusha mpaka Musoma, hizo ni kilometa 1,233 na vilevile tutakuwa na Ukanda wa Kusini ambao ni wa kilometa 1,092 ambao utatoka Mtwara – Mbamba Bay na matawi yake ambayo ni ya Liganga na Mchuchuma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuanzia na reli ya kati, tumeshaanza ujenzi wa kiwango cha standard gauge kutoka Dar es Salaam mpaka Morogoro, kilometa 300 ambazo zitajumlisha njia ya reli ya kawaida pamoja na trunks zake na sliding, mkandarasi mpaka sasahivi yuko site anaendelea na kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekwishapata mkandarasi vilevile kwa ajili ya kipande cha Morogoro mpaka Makutupora kilometa 422 sasa hivi yuko kwenye mobilization, wakati wowote ule ataanza kazi, sehemu nyingine zote zinaendelea na utaratibu wa upembuzi yakinifu na taratibu nyingine kwa ajili ya ujenzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jumla ya gharama itakayotumika kwa ajili ya mradi huu wa standard gauge kwa nchi yetu itakuwa ni dola za Kimarekani bilioni 3.17. Tunategemea itakapokwisha itakuwa na uwezo wa kwenda speed ya kilometa 160 kwa saa, vilevile itabeba tani milioni 17 kwa mwaka. Hiyo ni miradi kwa upande wa reli ambayo inaendelea na tumeona jitihada za Serikali katika kuhakikisha kwamba hiyo reli inajengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa bandari tulikuwa na wachangiaji kadhaa ambao walizungumzia sana masuala ya bandari. Serikali imekuwa na mpango mzuri sana wa kuboresha bandari yetu kwanza ya Dar es Salaam kwa geti namba moja mpaka geti namba saba, ambapo moja ya shughuli zitakazofanyika itakuwa ni kuongeza kina cha bandari kwa mita 15 deep sea, halafu kuna sehemu ya meli kugeuzia na yenyewe inapanuliwa kwa kiwango kizuri kabisa cha kimataifa, vilevile tunaongeza sehemu ya dragging and channel.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Bandari ya Dar es Salaam itaenda kuboreshwa kwa kipindi kifupi kinachokuja kuhakikisha kwamba inaweza kuhudumia meli nyingi kwa wakati mmoja kwa kiwango cha kimataifa na gharama zitakazohusika katika mradi huo ni shilingi za Kitanzania bilioni 335.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tuna uboreshaji wa Bandari ya Mtwara ambapo zimetengwa jumla ya shilingi za Kitanzania bilioni 186. Tunatengeneza gati mpya pale kwa ajili ya kufungua lango la Kusini kusafirisha na kupokea mizigo. Tunajua jinsi ambavyo kuna mabadiliko makubwa sana katika Ukanda wetu wa Kusini, kuna viwanda vinaanzishwa vikubwa, tunategemea tuweze kupata mizigo ya kutosha kwa ajili ya kuhudumia bandari ile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Mamlaka ya Bandari Tanzania inaendelea kulipa fidia kwa wananchi kwa ajili ya ujenzi wa bandari mpya ya Bagamoyo baada ya malipo kukamilika tunategemea kwamba ardhi itakayokuwa imepatikana sasa atapewa mwekezaji ambaye tunaendelea na mawasiliano naye kwa ajili ya kujenga bandari hiyo ambayo itasaidia sana katika kufungua lango upande wa Mashariki wa nchi yetu. Ni matumaini yetu kwamba, wananchi ambao wako maeneo ya Bagamoyo ambayo yako karibu na sehemu tutakakojenga bandari watatoa ushirikiano wa hali ya juu kwa Serikali kuhakikisha kwamba tunapata eneo hilo kwa ajili ya kujenga bandari mpya pale Bagamoyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tuna suala la viwanja vya ndege. Ni kweli kwamba Serikali imenunua jumla ya ndege sita, tunazo Bombadier Q400 ziko tatu ambazo zina uwezo wa kubeba abiria 76 na ndege mbili tayari ziko hapa nchini na moja itakuja hivi karibuni. Tunayo ndege ya Q Series au Q300 ambayo inabeba abiria 150 mpaka 176 na yenyewe iko kwenye hatua za mwisho kabla haijaja nchini na tumekwishafanya malipo ya mwanzo kwa ajili ya kupata Boeing 787 ambayo itakuwa na uwezo wa kubeba abiria 262. Ndege hizo zote ni kwa ajili ya kurahisisha huduma ya usafiri kwa njia ya anga ili nchi yetu iweze kupata maendeleo yanayotarajiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Serikali imeendelea kufanya upembuzi yakinifu kwa ajili ya upanuzi wa viwanja mbalimbali hapa nchini. Tuna viwanja 11 ambavyo tayari matengenezo yameshaanza kwa ajili ya kuvipanua, kupanua run ways, kuna sehemu kwa ajili ya apron, kwa ajili ya sehemu za kugeuzia ndege na ku-park, lakini vilevile tumeendelea kujenga majengo ya abiria kwa ajili ya kuhudumia abiria wanaofika kwenye viwanja hivyo husika vya ndege. Kwa kutaja tu, kuna uwanja wa ndege wa Kigoma tumeshatangaza tender kwa ajili ya kutafuta mkandarasi wa kupanua uwanja huo, kuna uwanja wa ndege wa Sumbawanga tumeshatangaza tender vilevile, kuna viwanja vingine mbalimbali kama Mbeya, Tabora na uwanja wa ndege wa Geita. Kwa hiyo, kuna maendeleo makubwa ambayo Serikali inayafanya kwa ajili ya kuhakikisha kwamba viwanja vyetu vinakuwa vya ubora wa kisasa kabisa kwa ajili ya kuhudumia abiria mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaongelea kwa haraka tu upande wa barabara. Waheshimiwa Wabunge wote wanaelewa wazi kwamba kuna miradi mikubwa tunaendelea nayo ya ujenzi wa barabara. Kuna barabara ya TAZARA flyovers inaendelea, mkandarasi yuko pale na tunategemea muda sio mrefu barabara itakuwa iko tayari kwa ajili ya matumizi, vilevile kuna Ubungo Interchange ambayo tayari maandalizi ya ujenzi yameshaanza, mkandarasi yuko kwenye site kwa ajili ya kufanya mobilization na shughuli mbalimbali za kuhakikisha kwamba ujenzi unaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Serikali imeendelea na mpango wa kuhakikisha kwamba kila Mkoa katika nchi yetu ya Tanzania unaunganishwa kwa kiwango cha lami. Sehemu zile chache zilizobakia ambazo bado hazijapata mkandarasi tunaendelea kutangaza tenda ili mkandarasi apatikane kwa ajili ya kuweza kuunganisha Mikoa yetu kwa kiwango cha lami, lakini vilevile tunaunganisha Wilaya zetu ndani ya Mikoa mbalimbali kwa kiwango cha lami na hatua kadhaa mbalimbali zimeshaendelea kutekelezwa. Tunashukuru sana kwa michango ya Waheshimiwa Wabunge na tunawaahidi tutaendelea kuhakikisha kwamba tunayachukua mawazo yao na kuyafanyia kazi kwa kadri itakavyowezekana, ili nchi yetu iweze kuwa na mtandao wa barabara nchi nzima ambao unapitika mwaka mzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kuwapongeza vilevile Waheshimiwa Wabunge ambao wametuletea michango kwa njia mbalimbali na kwa sekta yetu ya uchukuzi, mawasiliano na ujenzi tunawaahidi kwamba, tutafanya nao kazi kwa karibu sana, lakini tukiwakumbusha kwamba ujenzi au uinuaji wa kiwango cha barabara unategemea kwanza vikao ndani ya Halmashauri husika, baada ya hapo inekwenda kwenye RCC, baada ya hapo ndiyo inakuja kwenye bajeti kuu na kutengewa pesa kwa ajli ya ujenzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuzungumza hayo naomba kuunga mkono hoja. Ahsante.