Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Mary Deo Muro

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MH. MARY D. MURO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nipongeze uwasilishaji wa Kamati ya Bunge na Kambi ya Upinzani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Serikali kuwaangalia kwa jicho la huruma wajasiriamali wadogo kama wasindikaji ambao wanakutana na pingamizi kubwa na kukatishwa tamaa na Taasisi za Serikali za Udhibiti. Mfano, TFDA imekuwa chanzo cha wajasiriamali kukata tamaa kwani TFDA wanatoza fedha nyingi sana kwa kila product/ bidhaa inayotengenezwa. Pia suala la TFDA kutoza kwa dola imekuwa kikwazo kikubwa na inarudisha nyuma zoezi zima la wajasiriamali kukua. TFDA inatoza dola 2.5 mpaka 500 kwa bidhaa ambayo mtengenezaji anaiuza kwa shilingi za Kitanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali iangalie jinsi ya kupunguza urasimu kwenye usajili wa biashara kwani urasimu ni mkubwa unapelekea watu wengi kukata tamaa kwa mfano wawekezaji toka nje wanalalamikia sana kuhusu usajili hapa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niishauri Serikali juu ya kodi kwa wafanyabiashara wanaoanza biashara kutozwa kodi kabla ya biashara kuanza. Sheria ya mlipa kodi inatozwa kwa kuangalia pato la biashara na si mtaji hivyo inasababisha watu wengi kushindwa biashara kwani hawana grace period ya biashara kama wageni wanavyopewa fursa hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali kuwa na vipaumbele kwenye mipango yake kwani Serikali ikiwa na vipaumbele vichache vinavyotekelezeka itasaidia kuwezesha nchi kuondokana na utegemezi au kuongeza Pato la Taifa kuliko ilivyo sasa ambapo vipaumbele ni vingi kiasi kwamba utekelezaji unashindikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali katika Mpango wake wa viwanda iimarishe kilimo ambako malighafi zitatoka. Serikali iboreshe tafiti za kilimo na watoe elimu ya kilimo ili wananchi wajue kilimo cha kisasa chenye tija na si kilimo cha mlo tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali kuangalia hili suala la masoko kwa mazao, soko la ndani na la nje. Mpaka sasa wananchi wamekata tamaa ya kilimo baada ya Serikali kushindwa kununua mazao yao pia sheria ya kukataza wakulima kujitafutia masoko. Wakulima wengi wamekata mitaji baada ya kulima na kukosa masoko na mazao yao kuishia kuharibika. Pembejeo nazo ni tatizo, hazifiki kwa wakati hivyo kupishana na msimu wa kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niishauri Serikali kuweka viwanda vya kuchakata bidhaa zitokanazo na mifugo ikiwa ni pamoja na ngozi, maziwa, nyama kwani Tanzania ina mifugo mingi.