Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Hon. January Yusuf Makamba

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bumbuli

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kushukuru sana wote waliochangia hoja hii, wamefika wachangiaji 43 waliochangia kwa maandishi na kwa kuzungumza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunashukuru sana kwa waliotuunga mkono, tunashukuru waliotuongezea mawazo na vilevile tunawashukuru waliotukosoa. Tutajibu baadhi ya hoja hapa kwa sababu muda ni mdogo na nyingine tutazijibu kwa maandishi na kuwakabidhi Waheshimiwa Wabunge kabla ya mwisho wa Mkutano huu wa Bunge. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo kubwa ambalo limezungumzwa kwa hisia kubwa na Wabunge wa pande zote linahusu uchaguzi wa Zanzibar na ndilo nitakaloanza nalo na nitaanza kwa kunukuu Katiba ya Zanzibar ambayo inatambulika na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 72(1) inasema; “Mahakama Kuu ya Zanzibar ndiyo pekee yenye mamlaka na uwezo wa kusikiliza na kuamua mashauri yote yanayohusiana na uchaguzi wa Zanzibar.” (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hayo ndiyo majibu yetu kuhusu uchaguzi wa Zanzibar, sitazungumza lolote hapa kwa sababu hapa siyo mahali pake, mahali pake pameelezwa kwenye Katiba ya Zanzibar. Vilio vyovyote vinavyohusu uchaguzi wa Zanzibar vikiletwa hapa Bungeni kwa kweli hapana msaada wowote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja iliyoko mbele yetu ni ya Muungano na Mazingira. Nianze tu kwa kusema kwamba mimi sikuzaliwa wakati wa Tanganyika, nimezaliwa wakati wa Tanzania kama ilivyo asilimia 92 ya Watanzania, sijui nchi yoyote zaidi ya Tanzania. Asilimia 92 ya Watanzania hawajui nchi yoyote zaidi ya Tanzania. Leo Tanzania hii uhalali wake ukihojiwa naumia binafsi.
Nadhani kwa viongozi ambao tumepewa dhamana na tuko kwenye Bunge ambalo juu lina nembo ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni muhimu kabla hatujatoa maoni na kuzungumza kuhusu jambo kubwa kama hili tukajua shabaha yake, malengo yake, madhumuni yake na chimbuko la Muungano wenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutakumbuka kwamba kwenye miaka ya 1960 kulikuwa na hisia kubwa sana Barani Afrika za ukombozi, tulikuwa tunatafuta uhuru, tulikuwa tunataka kujikomboa na moja ya nyenzo kubwa za kujikomboa zilikuwa ni umoja wa watu wa Afrika. Hisia hizo za ukombozi zilihamasisha tuungane. Sisi bahati yetu Watanganyika na Wazanzibari Muungano wetu ulikuwa ni kurasimisha udugu ambao tayari upo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waasisi wa Muungano walikuwa na maarifa makubwa, walitafakari, walifikiria sana aina ya Muungano unaoendana na mazingira ya nchi yetu, aina ya Muungano unaoendana na ukubwa wa pande zote mbili, idadi ya pande zote mbili, tamaduni zetu na muingiliano ambao ulikuwa tayari umeshajitokeza kabla ya Muungano. Wale wazee walifikiria yote tunayoyazungumza sasa, Serikali hizi, zile na zile. Walipoamua, ndiyo maana Muungano huu umedumu, hawakuamua kwa pupa, hawakuamua kwa papara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi kama mwanafunzi wa umoja wa mwafrika, kama mwanafunzi wa historia ya Afrika, nimechukua muda mrefu kujifunza. Mmoja wa mwalimu wangu ambaye nimejifunza kwake yuko hapa, Balozi Job Lusinde. Nimetumia saa nyingi kuwa naye na moja ya swali nililomuuliza ni kwamba hebu niambie ilikuwaje, mliamuaje, chimbuko lake lilikuwa nini, nani alianzisha wazo! Nawasishi viongozi wenzangu Wabunge kwamba kama tunataka kuupa jina baya Muungano angalau tujue basi chimbuko lake. Naamini kwamba tukijua chimbuko lake, shabaha yake, malengo yake, kidogo tutapunguza ukali wa lugha tunayoitumia katika kuupa jina baya Muungano wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Muungano wetu ulikuwa ni sehemu ndogo ya mradi mkubwa wa ukombozi wa mwafrika. Baadhi wanadhani kwamba umoja wetu sisi hauhitajiki sasa hivi, lakini leo unahitajika zaidi kuliko ilivyokuwa mwaka 1964. Kuna nchi nyingine zimeungana miaka 200 iliyopita, Marekani kwa mfano, zile federal government wana miaka zaidi ya 200 na hawajamaliza changamoto za muungano wao lakini hawazungumzii kuuvunja kwa sababu ya changamoto zilizopo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuliaswa na waasisi wa nchi yetu kwamba sisi ambao tunatafuta kuwa nchi zinazoendelea tunahitaji umoja zaidi kuliko wengine. Inawezekana baadhi yetu hatuoni mantiki, hatuoni busara waliyoiona waasisi wa Muungano wetu, hiyo ni sawa kabisa kwa sababu watu tunatofautiana. Wito wangu tu ni kwamba hebu tu-moderate lugha zetu kidogo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesoma na nimesikiliza taarifa ya Kambi ya Upinzani kuhusu Muungano na mambo mengineyo na nimesikitishwa sana na baadhi ya lugha zilizotumika mle. Baadhi ya mambo yamejibiwa na Waziri Mheshimiwa Dkt. Mwinyi lakini kutumia maneno kwenye taarifa ile ya ukoloni na unyonyaji unaofanywa na Tanganyika dhidi ya Zanzibar, ni lugha ya kutugawa Watanzania. Inawezekana kuna mambo yanayoleta manung‟uniko kwenye Muungano, ni kweli inawezekana, lakini kwenda kwenye kiwango hiki cha kutumia maneno haya ya ukoloni na unyonyaji unaofanywa na Tanganyika dhidi ya Zanzibar ni lugha ambayo unapolaumiwa kwamba hupendi muungano huwezi kukataa kwa sababu umetumia lugha hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Jeshi la Tanganyika ameshajibu Mheshimiwa Mwinyi. Niendelee tu kwa kusema kwamba, ndugu yangu wa Konde pale rafiki yangu sana Mheshimiwa Khatib, anasema kwamba Muungano huu haufai kwa sababu tuko maskini, tuliungana ili tuwe matajiri. Mimi nataka kumuambia kwamba kwa sababu tuko maskini ndiyo tunauhitaji zaidi Muungano wetu huu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napata shida kuelewa kitu kimoja kwamba Muungano haufai lakini Ubunge wa Bunge la Muungano unafaa. Mimi mantiki siioni labda ni ile ya kusema nyama ya nguruwe haramu, mchuzi wake halali. Inabidi tuamue kitu kimoja, kama hatuamini katika Muungano hatuwezi kuamini katika taasisi za Muungano ikiwemo Bunge la Muungano na hatuwezi kuwa sehemu ya taasisi za nchi ambayo hatuikubali na hatuiamini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja imetolewa kwenye Taarifa ya Upinzani kwamba ni CUF na napenda kunukuu hivyo hivyo, ni CUF na kiongozi wake Maalim Seif ndiyo pekee wanaolinda Muungano hadi kufikia ulipofikia, ukurasa wa 13, haya ni matusi kwa viongozi wote waliowahi kuongoza nchi hii. Kwa sababu wamefanya kazi kubwa ya kuulinda muungano, kuimarisha na kuujenga. CUF imeanza kuingia kwenye harakati mwaka 1992 wakati Muungano upo na unaendelea. Unaposema kwamba ni yeye peke yake tu ndiyo anafanya Muungano uwepo na udumu maana yake Mwalimu Nyerere, Karume, Mwinyi, Mkapa, Salmin Amour, Karume wa pili wote hawakuwa na maana yoyote isipokuwa kiongozi mmoja kule Zanzibar. Ndiyo maana nasema hebu tuya-moderate kidogo haya maneno ili angalau tutoke tukiwa tunaonekana tuna busara katika Bunge hili. (Makofi)
Mheshimiwa mwenyekiti, baadhi ya mambo tutayajibu kwa maandishi kwa sababu hatuwezi kuyajibu yote hapa, niende kwenye michango ya baadhi ya Wabunge.
Mchango wa Mheshimiwa Shamsi Vuai Nahodha kuhusu mapendekezo ya mgawanyo wa mapato jambo ambalo ni la msingi sana na jambo ambalo ndilo litapelekea kwenye ile dhana ya msingi ya kwamba kila upande uchangie na upate kulingana na mchango wake na ukubwa wake. Mheshimiwa Vuai amesema kwamba katika miaka kumi ya yeye kuwa Waziri Kiongozi na miaka mitatu ya kuwa Waziri kwenye Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hawakufanikiwa kulimaliza suala hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimueleze ndugu yangu kwamba Serikali hii imeingia madarakani miezi sita iliyopita, sisi hatutatumia miaka kumi kama aliyoitumia yeye katika Serikali iliyopita. Naomba niseme tu kwamba atupe nafasi na tumeanza, barua yangu ya kwanza kabisa kama Waziri katika Serikali hii na ilichelewa kwa sababu Waziri wa Fedha alichelewa kuteuliwa, ilikwenda kwa Waziri wa Fedha kuhusu kushirikiana kuandaa Waraka wa Baraza la Mawaziri wa kupitisha mapendekezo ya Tume ya Pamoja kuhusu mgawanyo wa mapato. Wizara ya Fedha imelifanyia kazi jambo hilo, Waraka upo tayari na wakati wowote utapelekwa kwenye Baraza la Mawaziri na kufanyiwa maamuzi ikiwemo uanzishwaji wa Akaunti ya Pamoja. Jambo hili litahusu pia mgawanyo wa zile asilimia 4.5 na kadhalika litafanyiwa kazi mara mapendekezo haya yatakapopitishwa kwa hiyo kazi inafanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Menyekiti, lakini kabla ya hapo kuna arrangement za muda ambazo zinaendelea ikiwemo hiyo 4.5 kwa GBS na gawio la BOT. Pia VAT inayokusanywa Zanzibar kwa wafanyakazi wa Bara wanaofanya kazi Zanzibar inabaki Zanzibar na PAYE kwa maana hiyo na VAT inayokusanywa na TRA kwa upande wa Zanzibar inabaki Zanzibar na PAYE kwa wafanyakazi wa Bara wanaofanya kazi Zanzibar inabaki Zanzibar vilevile. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Fakharia amezungumzia kuhusu Sekretarieti ya Ajira. Waziri wa Utumishi alitoa taarifa hapa kwamba tutafungua ofisi Zanzibar katika mwaka wa fedha unaokuja. Kwa hiyo, ofisi hiyo itafunguliwa na mimi niliwaunganisha Waziri wa Utumishi, dada yangu Mheshimiwa Angellah Kairuki na Waziri wa Utumishi, Mwalimu Haroun kule Zanzibar na Mheshimiwa Kairuki amepanga tarehe ya kwenda kutazama jengo na mahali ambapo ofisi itakuwepo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wiki nne zilizopita niliandika barua kwa Mawaziri kama saba hivi ambao wanasimamia taasisi za Muungano na kuwaomba kwamba watuletee mgawanyo wa ajira kati ya watumishi wa Zanzibar na watumishi wa Tanzania Bara kwenye taasisi za Muungano. Makubaliano yaliyokuwepo ni ya asilimia 79 kwa 21, makubaliano ya muda na Waheshimiwa Mawaziri hawa wameanza kunitumia. Nimeona kwa mfano Wizara ya Mambo ya Nje ambayo ndiyo inalalamikiwa sana kwa mwaka 2014/2015, katika nafasi 27 zilizotoka nafasi saba asilimia 26 zilikuwa Zanzibar na nafasi 20 asilimia 74 zilikuwa upande wa Tanzania Bara. Kwa hiyo, tumeanza na tutaendelea kwa sababu tunayo dhamira ya kuimarisha Muungano wetu, hatutachoka wala hatutachukizwa na maneneo ya kuudhi yanayozungumzwa dhidi ya muungano. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kaka yangu Mheshimiwa Daniel Nsanzugwanko amezungumza na napenda nikiri kwamba tulipitiwa. Tulipitiwa kwa msingi kwamba sisi tulichukua human activities zote zinazoathiri mazingira ikiwemo wingi wa watu katika eneo dogo kwa wakati mmoja. Nakubali kwamba tungetaja wakimbizi kama ni changamoto mahsusi ya mazingira. Bahati nzuri maeneo aliyoyataja mimi nimefanya kazi miaka 20 iliyopita, nilikuwa Meneja wa Kambi ya Wakimbizi kule Mtabila, nafahamu Mtabila, Muyovosi, Lugufu, Nyarugusu, Kanembwa na kwingineko, kwa hiyo, Heru Juu, Heru Shingo na Mabanda kote ni kwetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nithibitishe kwamba kweli uharibu wa mazingira ni mkubwa sana unaotokana na uingiaji wa wakimbizi. Kwa hiyo, sisi kama Wizara tutawasiliana na Mashirika ya Kimataifa yanayohudumia wakimbizi kwamba kazi yao isiwe ni kulisha wakimbizi tu bali kutoa mchango kwenye kurudisha mazingira ya eneo lile kwenye hali nzuri. Mimi naahidi kutembelea mwenyewe kujionea mambo yalivyo huku. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, badhi ya Wabunge wamezungumzia masuala ya NEMC. Kwenye hotuba yetu tumezungumza jinsi ambavyo tutabadilisha na kupitia mfumo mzima wa kupitia vyeti vya tathmini ya athari kwa mazingira ili visiwe vinatumika kuchelewesha miradi ya uwekezaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baadhi ya Wabunge wamesema kwamba ofisi yetu ina bajeti ndogo na ina uwezo mdogo wa kitaasisi wa kudhibiti changamoto kubwa za mazingira. Mkitazama kwenye hotuba yetu ya bajeti katika maelezo ya Mfuko wa Mazingira, moja ya maelezo ya kazi ni kujenga uwezo wa kitaasisi wa Serikali ikiwemo NEMC kukabiliana na athari za mazingira. Kwa hiyo, Mfuko ule utakapoanza ofisi yetu itakuwa na uwezo mkubwa wa kifedha na rasilimali watu wa kuweza kudhibiti mazingira ikiwemo kuajiri Maafisa Wakaguzi wa Mazingira nchi nzima ili kila Halmashauri iwe na watumishi na hizi kamati kwenye kila kata na kijiji ili ziweze kufanya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesoma Taarifa ya Kambi Rasmi ya Upinzani ya dada yangu Mheshimiwa Pauline na napenda kumshuru sana kwamba kwa dhana na falsafa tunakubaliana bila shaka yoyote. Tunakubaliana kwamba mazingira ni jambo kubwa na pana na kule tunapoenda kwenye uchumi wa viwanda lazima tuzingatie hifadhi ya mazingira. Hilo tunakubaliana na tunashukuru kwa sehemu kubwa ushauri mlioutoa tutauzingatia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie mambo machache tu kwenye taarifa ile ambayo yanahitaji kurekebishwa. Kwenye ukurasa wa 19 ripoti imesema kwamba kwenye mradi wa DART tathmini ya mazingira haikufanyika. Nilitaka tu nisahihishe kwamba tathmini ilifanyika na cheti Na. EC/EIS/146 cha tarehe 30/6/2009 kilitolewa na masharti yalitolewa kwa waendesha mradi ule wa mambo ya kuzingatia katika hifadhi ya mazingira kwenye mkondo ule. Kwa hiyo, nilitaka niseme hilo la uelewa kwamba kwenye mradi ule tathmini ilifanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ripoti ya Mheshimiwa Pauline ilizungumzia kuhusu ripoti ya CAG ambayo ilitambua udhaifu kwenye utayari wa NEMC kwenye tasnia hii ya gesi na mafuta. Tumepokea sisi taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu na tutafanyia kazi mapendekezo yale. Mapendekezo yale utekelezaji wake unahitaji uwezo mkubwa na hakuna shaka yoyote kwamba tunaujenga. Niseme tu kwamba Sheria ya Gesi na Mafuta ambayo ndiyo ingetupa nguvu na uhalali sisi wana mazingira kuhusu ufuatiliaji imepitishwa mwaka jana tu na bahati nzuri sheria ile inatambua Sheria ya Mazingira na inatoa nafasi kwa NEMC kufanya kazi hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia taarifa ya Kambi Rasmi ya Upinzani imezungumzia miradi yenye shaka, miradi ambayo anasema inanukanuka ufisadi kidogo.
Mimi niseme tu kwamba tumepokea angalizo na mtu yeyote ambaye ananyoosha kidole kwamba mahali fulani inawezekana pana harufu anakusaidia. Sisi tunachukua taarifa hizo kama msaada kwa sababu Serikali hii imeamua kupambana na maovu ikiwemo rushwa na ufisadi. Kwa hiyo, haiwezekani nikasimama hapa nikakulaumu kwamba kwa nini umesema, nasimama hapa kukushukuru kwamba ni jambo ambalo tutalifanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ila niseme tu kwamba miradi ile ina fedha za ndani kwa maana ya fedha zetu na za wafadhili, fedha za ndani zinaitwa counterpart fund. Kwa hiyo, siyo ajabu ukitazama makaratasi yetu ukakuta mradi wa ukuta, ukatazama karatasi la mfadhili ukakuta mradi wa ukuta kwa sababu fedha hizi zinakaa pamoja. Vilevile miradi hii inakaguliwa na CAG na katika miaka miwili iliyopita imepata hati safi lakini angalizo tumelipokea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu jana wakati nakutana na wataalam Wizarani nilielekeza kwamba wasiondoke kesho ili tupitie miradi yote. Kwa sababu kuna miradi mingi vya mazingira ambayo wakati mwingine hatuna taarifa za kina ili tuijue kila mradi ni upi, gharama zake ni zipi, umefikia wapi, unanufaisha watu wangapi, uliamuliwaje upelekwe huko ulikopelekwa na tunaweza kufanya maamuzi ya kuhakikisha kwamba miradi hii inawanufaisha watu wengi zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepokea mchango wa Mheshimiwa Rehani Mwinyi anazungumzia kuhusu Mfuko wa Mazingira kwamba ndiyo mkombozi wa mazingira yetu na mimi nakubaliana naye asilimia 100. Katika mwaka huu wa fedha tunafanya mazungumzo ndani ya Serikali kuhusu vyanzo mbalimbali vya Mfuko huu na tunategemea support ya Bunge tutakapokuwa tumemaliza Serikalini. Mfuko huu kama tulivyosema kwenye hotuba yetu tunataka kwa kuanzia uwe na shilingi bilioni 100 lakini fedha hizi hazitoshi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, gharama ya kuhifadhi mazingira na kukabiliana na athari za mazingira na kurudisha mazingira katika hali yake ya kawaida kwa mwaka ni karibu shilingi bilioni 350. Ili turudi katika hali ambayo tunataka tuwe lazima fedha hizi zipatikane kwa miaka 17 mfululizo lakini sisi tunaomba shilingi bilioni 100. Nina imani kwamba ndani ya Serikali tutakubaliana kuhusu maeneo gani tunaweza kupata vyanzo hivyo ili Mfuko huu uanze ili tuwe na uwezo wa kuja katika maeneo yote kama aliyosema dada yangu Mheshimiwa Maufi kule Rukwa na kusaidia kurekebisha mazingira yaliyoharibika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatupaswi kutegemea wahisani kwa kuhifadhi mazingira ya nchi yetu kwa sababu huo ndiyo umekuwa mwelekeo mkubwa. Kuna dhana kwamba kwenye mazingira kuna hela nyingi za misaada lakini nchi hii ni ya kwetu, itarithiwa na watoto na wajukuu wetu, wahisani hapa siyo kwao. Kwa hiyo, sisi tuna wajibu mkubwa zaidi wa kuchanga ili kuhifadhi nchi yetu iendelee kuwepo siku nyingi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie tena kwa kushukuru kwa kupata fursa hii, nawashukuru Wabunge wote waliochangia, nashukuru kwamba mmetusaidia na naomba muendelee kutuunga mkono.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawashukuru wageni wetu walikokuja hapa siku ya leo ambao nimewataja, wale vijana wa mwaka 1964 waliochanganya udongo, Mzee Job Lusinde, wamekaa mpaka jioni hii na nina hakika matumbo yalikuwa yanawazunguka wakati Muungano ambao waliushuhudia unaundwa ulikuwa unadhalilishwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwaambie kwamba Serikali yao ipo imara katika kuulinda na kuhakikisha unaimarika ili kazi waliyoifanya iwe na matunda na iendelee kuwa sehemu ya urithi wa nchi yetu. (Makofi/Vigelegele)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naomba kutoa hoja.