Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Stanslaus Shing'oma Mabula

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nyamagana

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami naomba nitumie nafasi hii kukushukuru kwa kunipa nafasi ili angalau niweze kusema kidogo juu ya Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa ili haya ambayo tunakwenda kuyachangia utakapokuja Mpango kamili tuweze kuona mabadiliko lakini tuweze kuona hiki tunachokizungumza kinakwenda kufanyika kwa vitendo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sote tunafahamu tuko hapa ndani kwa sababu ya kuzungumza lakini kwa sababu ya kuleta hoja ambazo zitawasaidia Watanzania. Naomba nianze tofauti kidogo na kuanza kwangu nataka kuzungumza juu ya suala zima la uboreshaji wa miji, majiji lakini namna ambavyo tunaweza kushughulika na mambo ambayo yanaweza yakatusaidia sana kwenye sekta ya ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimefurahi moja ya kati ya mapendekezo yaliyoko kwenye Mpango huu katika sekta ya ardhi inatambua na wajibu wake mkubwa ni kupanga, kupima na kumilikisha lakini tukifanikiwa kupanga, kupima na kumilikisha sisi wenyewe tunasema itakuwa ni sehemu nyingine ya mfumo wa uboreshaji na upatikanaji wa mapato mengi zaidi. Kwa nini nasema haya? Natambua Serikali inao mpango thabiti wa kuhakikisha maeneo ya Miji, Majiji, Manispaa na Miji inapimwa kwa kiwango ambacho kinastahili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa upo mpango ambao unaendelea, mpango wa upimaji shirikishi ambao unamfanya mwananchi achange mwenyewe ili kuweza kupimiwa kwa sababu tu ya msingi kwamba maeneo mengi sana Serikali inatambua hayajapimwa. Liko tatizo moja hapa ambalo nilitamani sana kuliona kwenye Mpango humu ndani linawekewa mkakati thabiti.

Mheshimiwa Spika, la kwanza ni kuhakikisha hii premier ambayo inatokana na ada zinazoongezeka katika kulipia hati inaondolewa ili mwananchi huyu aweze kupata nafuu anapokwenda sasa kuchukua hati yake kimsingi.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine kubwa sote tunafahamu mpango huu ukifanyika vizuri miji yetu mingi ambayo kiukweli ziko squatters za kutosha ikapimwa ikapangika na watu wote hawa wenye squatters wakishamaliza kupimiwa hizi ni fedha zingine ambazo Serikali inaweza kuzipata na zikatusaidia sana kwenye mapato. Kwa sababu ni ukweli usiofichika sasa hivi ziko fedha nyingi sana zinapotea kwenye kodi ya majengo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa wale ambao wanasafiri na ndege ukipita kwenye Miji ya Dar es Salaam, Mwanza, Dodoma, Arusha na miji mingine yote mikubwa unaweza kuona ni namna gani nyumba zilivyo nyingi lakini 70% ya nyumba hizi unaweza kukuta miji haijapangwa, nyumba hazitambuliki na badala yake hazilipi kodi.

Mheshimiwa Spika, sasa zoezi hili likifanyika vizuri sina shaka mwananchi mwenyewe atakuwa na uhakika na kile ambacho anakifanya lakini atakuwa na uhakika na makazi yake, lakini kubwa zaidi muda ambao kwa sasa Serikali imetoa na ndiyo mpango, kwenye Mpango ije ituambie huu muda utakuwa unakwenda kwa ukomo wa muda gani ili kuweza kusaidia wananchi hao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu sote tunafahamu hata Mpango tunaokwenda nao upatikanaji wa fedha wenyewe haukidhi mahitaji na muda uliowekwa na Serikali. Sasa kule tunakokwenda lazima tuseme kwenye Mpango tunatazamia tuwe na muda mrefu.

Mheshimiwa Spika, yako maeneo ambayo yana milima, mimi natoka Mwanza, Jimbo la Nyamagana, watu wengi sana wamejenga kwenye milima na hawa hatuwezi kuwaondoa kwa namna yoyote ile lakini tukijitahidi tukawapimia, tukarasimisha maeneo yao waliyopo yana uwezo wa kutengenezwa vizuri na eneo hilo tukawa tumesaidia Serikali ikakusanya kodi wananchi wakaishi kwa amani na wakaendelea kushughulika na maisha yao ya kawaida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili, nilikuwa najaribu kupitia mpango huu sijaona popote, tulizungumza hapa juu ya urasimishaji wa biashara na wafanyabisahara ndogo- ndogo, tunawazungumzia machinga, mama lishe, baba lishe na wengine wauza mbogamboga na matunda. Sasa kwenye mpango huu tunaoupendekeza sasa hivi hatuoni umuhimu wa kuweka wafanyabiashara hawa watengenezewe mkakati endelevu kuliko hivi walivyo sasa tutawaacha tu, tumesema wapewe vitambulisho, halafu miaka mingine inakuwaje? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni lazima tuhakikishe kwenye Mpango huu tunaoutafakari tuwatambue watu hawa vizuri, wawekewe misingi ambayo itawasaidia maisha ya mbele zaidi watoke hatua moja na kwenda hatua nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu kwenye miji yote mikubwa hii, kama ambavyo kwenye kitabu chenu mmesema, ukitoka miaka ya 1967 mpaka leo kuna zaidi ya ongezeko la watu zaidi ya milioni 13 tafsiri yake ni nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ongezeko hili linapatikana kubwa sana kwenye miji. Kama hatutalitengenezea mkakati endelevu wa kudumu tutakuwa tunacheza mark time na hatuwezi kuwasaidia wananchi hawa. Kwa hiyo, ningependa sana tuone mkakati wa wafanyabiashara ndogondogo kwenye nchi hii inakuwa ni endelevu na mazingira yao tunatafakari namna ya kuwasaidia ili waweze kuendelea kufanya biashara zao vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu ni mpango wa kuzifanya Halmashauri ziwe na uwezo wa kukusanya mapato. Sote tunafahamu kwenye mpango hapa tumeshaanzisha sheria ambazo zipo, zilikuwepo na nyingine tumezihuisha sasa hivi, namna ya ukusanyaji wa mapato mengi na makubwa yaende kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali. Hili sio jambo jipya toka mwaka 2005/2006 lilifikiriwa, lakini halikufanyiwa kazi, mkakati wa upangaji wa matumizi asilimia 30 na 40 tunayoizungumza sasa hivi tunafahamu, ziko kodi zinaondoka kwenye Halmashauri zinakwenda kwenye Mfuko wa Serikali Kuu ikiwemo kodi ya majengo, ikiwemo kodi ya mabango na kodi nyingine kama tunavyoendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ni lazima tutengeneze mkakati kwenye mpango tunaoutazamia kuziwezesha Halmashauri zote nchini ziwe na uwezo wa kuanzisha vyanzo vingine vipya vya mapato. Kwa mfano, watu wanafikiria kujenga stand za mabasi, watu wanafikiria kuwa na miradi ya masoko ambayo inaweza ikaleta fedha nyingi kama kodi, lakini wapi wanapewa fursa ya kufanya hivyo? Hii PPP tunayoizungumza inaanza kufanya kufanya kazi kwa wakati gani na msingi wake ni upi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima tujenge msingi ambao utasaidia kuhakikisha kwamba, suala hili Halmashauri zinakuwa na uwezo. Mbali ya fedha hizi zilizoondoka, lakini nzina uwezo wa kujiendesha, zitapata fedha ambazo Madiwani watafanya vikao, Wenyeviti watalipwa na mambo mengine kadha wa kadha yataendelea, lakini Mheshimiwa Waziri wa Mipango hujalizungumza humu ndani. Ninaomba ulichukue na utakapoleta mpango kamili tuone namna ambavyo Halmashauri zimewekewa mkakati, ili ziweze kusimama na kujitegemea zenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la nne naomba niizungumzie sekta ya afya. Sote tunafahamu kwenye sekta ya afya mipango tuliyopita nayo, kwenye mwaka 2015/2016, 2016/2017 na 2017/2018 tuliweka mkakati wa kuhakikisha kila Wilaya kwenye kila Kata na Kijiji tunakuwa na zahanati na vituo vya afya. Kwenye Mpango huu nimejaribu kuangalia naona tumejikita kwenye Hospitali za Rufaa za Mikoa,Hospitali za Rufaa za Kanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sina tatizo na hili, lakini lazima tufahamu kama tunashindwa kujenga vituo vya afya na zahanati za kutosha, kesi tunayoizungumza ya kuokoa maisha ya mama na mtoto hatutafanikikiwa kama tuta-base kwenye hospitali za Kanda peke yake. Sasa ni lazima tukubaliane tunapozungumza namna ya kumsaidia mama na mtoto wasiendelee kupoteza maisha, tumeongeza dawa kwa kiwango kikubwa lakini lazima iendane na ujenzi wa zahanati na vituo vya afya kwenye kata na vijiji vyetu, ili tuweze kuwa na msingi imara. Tunapozungumza kumuokoa mama na mtoto tuwe tunamaanisha kutokana na haya ambayo tunayafanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumezungumzia hospitali za rufaa. Hospitali za Rufaa tumeona ujenzi unaendelea, lakini mikakati ya kuboresha, humu imetajwa Benjamin Mkapa, imetajwa Hospitali ya Ocean Road, zimetajwa hospitali nyingine ikiwemo na Muhimbili. Pia, nishukuru kwamba mmesema jengo la wodi ya mionzi kwa ajili ya ugonjwa wa kansa pale Hospitali ya Bugando limeshakamilika na ni kweli, lina mashine kubwa za kisasa zinafanya kazi na gharama yake ni kubwa. Mpango mkakati wa kujenga jengo la wodi ya wagonjwa ni upi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, imekuwepo bajeti miaka mitano iliyopita. Kila mwaka unawekwa mpango haukamiliki, unawekwa mpango haukamiliki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninakuomba ukienda pale Ocean Road kwenye asilimia 100 ya wagonjwa asilimia 60 ya wagonjwa wa saratani wanatoka Kanda ya Ziwa. Sasa ni lazima tufikiri namna ya kuiwezesha hospitali yetu ya Bugando ili iwe na uwezo wa kujisimamia tukihakikisha kwamba tunapeleka fedha kwa ajili ya kutengeneza na kufanya ukarabati wa vifaa hivi, lakini bila kusahau ujenzi wa jengo la wodi ambalo litatusaidia kuepukana na matatizo haya ambayo tunadhani tukifanya vizuri yanaweza yakatusaidia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumze juu ya habari ya miundombinu. Umezungumza juu ya habari ya miundombinu na focus yetu kubwa ni kwenye TANROADS. Lakini nikushukuru kwenye kitabu chako umesema, japo kwa uchache sana umeitaja TARURA kama chombo mbadala kinachokwenda kutatua tatizo la ardhi mijini na vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kutatua tatizo la barabara Mijini na Vijijini. Kazi wanayokwenda kufanya sasa hivi hawa TARURA moja ya kazi wanayokwenda kufanya sasahivi kubwa, uko mradi wa TSCP, uboreshaji wa Miji na Majiji kwenye Manispaa miji karibu Nane nchi nzima. Wana fedha nyingi zaidi ya shilingi bilioni 183 kujenga barabara kilometa nne, kumi, kulingana na mji wenyewe jinsi ambavyo ulivyo, lakini mkakati wa kuifanya TARURA kiwe chombo chenye nguvu, kiwe chombo ambacho leo hata Mbunge anayehudhuria kwenye Baraza la Madiwani kinapokwenda kutoa taarifa na yeye ajue, leo katika wigo wa Halmashauri hakuna sehemu yoyote Halmashauri inatoa taarifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hapa lazima tuzungumze pamoja. Kwenye mkakati tulionao TARURA kama ni chombo kitakachotusaidia, mkakati wetu ni nini wa kukifanya chombo hiki kiwe na uwezo, kiwe na fedha, lakini sisi ambao tunahangaika na barabara za wananchi tupate nafasi ya kuhoji na kujua ni nini kinachofanywa na kazi yake inafanyika wakati gani, ili tuweze kushauri, tuweze kusaidia na tujue umuhimu wa chombo hiki. (Makofi)

Mwisho tuliongelea bajeti iliyopita iko Mikoa iliyotajwa maskini, ukiwemo Mkoa wa Mwanza, Kagera, Mara, Singida na mingine. Moja ya kitu ambacho kimenishangaza sijaona mkakati wowote kwenye kitabu hiki unaozungumzia namna ya kukuza na kuondoa umaskini kwenye Mikoa hii.

Sasa utakapokuja na taarifa kamili kwamba, huu ndiyo mpango, Mheshimiwa Mpango naomba tuone ni namna gani tumejipanga kupunguza matatizo na kuondoa umaskini kwenye hii Mikoa mitano ambayo zaidi ya Mikoa minne iko Kanda ya Ziwa, tunafanya nini kuhakikisha kwamba, tatizo hili linaondoka? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, lakini sio mwisho kwa umuhimu kama muda utakuwa unaniruhusu ni suala la viwanda. Serikali tunaipongeza sana kwa kuamua kuchukua Shirika la National Milling ambalo lina vipuri vyake karibia nchi nzima maeneo mbalimbali. Sasa ni lazima tujue mkakati wa Serikali kwenye hizi National Milling, pamoja na kazi kubwa itakayofanya kununua mahindi na mpunga kuyaongeza thamani kwa kuyasaga, na mimi nimshukuru sana Mheshimiwa Jenista hapa, kwa namna ya kipekee kabisa walivyofikiria hii mifuko ya jamii kuwekeza fedha huku ambako zinakwenda kuonesha tija kwenye hawa watu ambao wanashughulika na haya.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaamini tukisimamia vizuri ajira kwa vijana zitapatikana, lakini wakulima wanaolia leo watakuwa na sehemu ya kupeleka mazao yao. Wakiyauza yanasagwa yanatengenezwa yanaongeza thamani na tunaona umuhimu wa Serikali hii kuwahudumia Watanzania hawa wakulima na wanyonge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niipongeze Serikali kwa namna ya kipekee kuanzisha mpango wa kurasimisha ajira zisizo rasmi kwa vijana, ikiwemo kuwaongezea uwezo, kuwawekea ujuzi na stadi za kazi, ni idadi kubwa sana ya vijana, zaidi ya vijana 3,400 wako kwenye vyuo mbalimbali ikiwemo Don Bosco na TIA. Tunaamini vijana hawa wakikamilika na mpango wa vijana milioni nne kufikia mwaka 2021, tunaweza kuwa tumefanya jambo la maana kama mipango yetu inavyozungumza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na mwisho tu niseme jambo moja kwamba, tuko hapa kwa ajili ya kujenga nchi yetu, nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mwenyekiti wa Kambi ya Upinzani, leo amezungumza vizuri na hivi ndivyo tunavyotakiwa tuseme, kwa sababu lengo letu ni kujenga nchi moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na Mungu akubariki. Ahsante sana.