Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Athumani Almas Maige

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tabora Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kuniruhusu na mimi nichangie Mpango huu wa Maendeleo unaopendekezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa vile natoka Mkoa wa Tabora siwezi kuanza vyovyote kwa sababu siasa ya Tabora ni tumbaku. Ndiyo maana kila Mbunge aliyesimama leo hapa ameongelea tumbaku. Kilimo cha tumbaku kimetulea Tabora kwa miaka 50 iliyopita lakini tukio la sasa la tumbaku kutonunuliwa limekuwa tatizo. Wakulima wa tumbaku ambao walitakiwa wauze tumbaku miezi sita iliyopita leo wanayo tumbaku ndani ya maghala na matokeo yake hawana chakula wala mavazi, watoto wa shule wamefaulu, wengine wamepewa ufadhili wa kulipiwa vyuo vikuu, wameshindwa kulipia ile registration fee lakini pia hata kuwasafirisha wameshindwa, pia kuna wagonjwa wameshindwa kutibiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatusaidia sana, Mheshimiwa Waziri Mkuu amekuja mara mbili ameongea na wakulima, ameongea na wanunuzi wa tumbaku. Mimi nimefanya kazi ya kukutana na wanunuzi wote watatu wa tumbaku, TLTC, Aliance One na GTI. Wote hawakuwa na bajeti ya tumbaku iliyolimwa kwa mwongozo wa Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwepo Morogoro wakati Serikali iliposema wakulima limeni tumbaku, itanunuliwa. Wamelima tumbaku nje ya makubaliano ya makampuni yale ya ununuzi, tumbaku ile ndiyo ilikuwa tegemeo la wakulima ambao wengine walikuwa hawajalima, wanakopeshwa mbolea na vyama vya ushirika vikuu WETCO, sasa hawawezi kuuza tumbaku, walikopa mabenki, wanauziwa mali zao, hali ni mbaya sana.

Mheshimiwa Spika, Makampuni haya hayakuwa na bajeti ya tumbaku ya ziada, yamejikunakuna, yamejivuta, mimi sitetei makampuni lakini nasema kama biashara, wametafuta hela za ziada, wako tayari kununua tumbaku kwa dola 1.25, Serikali imewapangia bei ya dola 1.75, hawana hela hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimetoka kutembea kwenye Jimbo langu lote la Tabora Kaskazini wananchi wako tayari kuuza tumbaku hata kwa dola 1 ambayo ni sawasawa na Sh.2,250 kwa kilo, Serikali imekataa. Sasa wananchi hawataki hata kumwona Waziri wa Kilimo kwa sababu ameleta chuki kubwa sana. Kwa nini Serikali isiruhusu wananchi hawa wauze tumbaku kwa sababu tumbaku sasa baada ya mwezi mmoja itakuwa haina thamani tena. Tumbaku itakuwa imeoza, itakuwa imeharibika na imekuwa nyepesi, haina thamani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba suala hili la tumbaku Serikali imeona kila Mbunge wa Tabora akisimama anaongelea tumbaku, sisi sio wajinga, tuna uchungu, tunahurumia wananchi. Mimi nikienda jimboni nafukuzwa, simu yangu imejaa maswali tumbaku inanunuliwa lini na sina majibu. Serikali kama ina huruma kweli kwa wakulima tofauti ya bei ambayo Serikali inataka wanunuzi wanunue dola 1.75 na wanunuzi wako tayari kununua kwa dola 1.25, Serikali itoe ruzuku ya senti 50 kwa tumbaku iliyopo ya kilo milioni 14.7, thamani yake ni shilingi bilioni 15. Basi itoe ruzuku hiyo kwa wakulima ili waweze kuuza tumbaku iliyopo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumbaku imekuwa tatizo kubwa sana na Serikali ndiyo imekamata kwenye mpini. Wananchi wanasikitika sana, wanailaumu Serikali kwa nini imezuia. Kwanza tumbaku wameilima wao wenyewe, wamekopa mikopo wao wenyewe, wanataka kuuza hata kwa dola moja, makampuni yametoa dola 1.25 kwa nini Serikali inakataa? Maana kuna mwaka wa hasara na faida, tukubali wakulima wa tumbaku safari hii tupate hasara lakini itakuwa hasara zaidi kama mwezi mmoja utapita bila kununua tumbaku hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya tumbaku, lipo suala ambalo tunafikiri ni zuri sana. Serikali imefanya kazi nzuri sana ya kujenga reli ya standard gauge, lakini bajeti inayowekwa kwenye standard gauge ni ndogo, itachukua muda mrefu sana kuja kufika Tabora. Tuna habari kwamba imefika mpaka Morogoro, inawezekana ikafika mpaka Dodoma lakini kuja kufika Tabora kwa bajeti hii ya kusuasua hatuwezi kumaliza hiyo standard gauge. Ni wazo zuri, ni mpango mzuri lakini tufanye mpango wa kumalizia, siyo mpango wa kwenye makaratasi halafu hauishi. Nakumbuka tulipanga mwaka mmoja uliopita na leo reli haipo hata kilometa 40.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo suala zuri pia la anga. Tabora tunajengewa kiwanja kipya cha ndege lakini vilevile tunajengewa na jengo la wageni, hii ni hatua nzuri sana. Hata hivyo, lipo tatizo, uendeshaji wa Shirika hili la Ndege mimi sidhani kama tuko kibiashara zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo pia tatizo la ndege zetu kukamatwa huko nje. Mimi nalijua suala hili kwamba Shirika la Ndege halikuweza kununua ndege zake kwa sababu ndege yetu yoyote ambayo ingeruka nje ingekamatwa. Tunapenda kujua, ndege ambayo imekamatwa huko nje inakuja? Serikali iwe wazi iseme ndege inakuja lini ili wananchi tuendelee kushangilia mafanikio ya anga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, upo mradi wa bomba la kutoka Uganda kuja Tanzania, ni mradi mzuri ambao Serikali na wananchi wote tunashangilia kwa sababu bomba hili lilikuwa na ushindani na jirani zetu. Kwa hiyo, mafanikio haya tunayapongeza, ni jambo zuri, Serikali imepambana na kupata mradi huu ambao utaleta faida. Kwanza kupitisha mafuta tutapata hela lakini italeta ajira kubwa kwa wananchi ambao watajenga bomba hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la miundombinu, nashukuru sana pia kwamba barabara sasa zitajengwa lakini katika barabara za mikoa ipo barabara ya kutoka Tabora kwenda Mambali inaunganisha Shinyanga, ipo kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi lakini sioni utekelezaji wake ukitokea, hata upembuzi wake hakuna. Ilikuwa ni hadithi tu au kweli barabara hii itajengwa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii ikijengwa itasaidia kuunganisha Mikoa ya Tabora na Shinyanga. Pia ipo kwenye corridor ya mazao, kwa hiyo barabara hii kwetu ni muhimu sana kwa watu wa Tabora, Bukene na Shinyanga. Katika Mpango huu siioni barabara hii. Naomba Serikali itakapojibu ituambie barabara hii ya Tabora – Mambali imo au haimo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la REA, nimeshangaa sana, nimetembea jimbo zima siioni REA na REA III tumezindua Sikonge kule, kwenye jimbo langu mbona simwoni mkandarasi, yuko wapi, kimetokea nini, kiini macho gani? Wananchi wananiuliza REA vipi Mheshimiwa Mbunge wetu, sina jibu. Serikali ituambie hatua kwa hatua utekelezaji wa kuweka umeme vijijini, ni muhimu. Sisi kule tumbaku tunalima halafu tunakausha kwa kukata miti, ili kulikimbia jangwa tukaushe tumbaku kwa umeme.

Mheshimiwa Spika, tunaomba REA iwe na mpango ambao unaeleweka sasa hatuelewi REA inaenea kweli vijijini au ilikuwa hadithi? Mbona imekuwa tofauti sana na ilivyoanza REA I na II, REA III imetokea nini, limetokea jini limemeza umeme, mbona hatuoni maendeleo ya umeme?

Mheshimiwa Mwenyekiti, liko suala la elimu, licha ya kizungumkuti ambacho Mheshimiwa Waziri wa Elimu leo amekielezea hapa kuhusu jinsi ya kuwa-sponsor wanafunzi lakini mimi nina wanafunzi baba zao walifariki, nimeiandikia Bodi ya Mikopo, mwaka jana wamekosa na mwaka huu pia wamekosa. Vigezo nimesikia hapa anasema moja ni kutokuwa na wazazi au uwe mwenye ulemavu, mimi nina wanafunzi wawili ambao nimechukua jukumu la kuwaandikia barua na kumwandikia Mkurugenzi wa Bodi ya Mfuko wa Elimu lakini wamekosa tena na hawana baba, mama hawana mtu yeyote wataenda wapi na wamefaulu division one wote lakini wamekosa, sasa mfumo ukoje?

Mheshimiwa Spika, kama kigezo ni kuwa yatima na hawa ni yatima wamekosa, kama kigezo ni kufaulu vizuri wamefaulu, kama kigezo ni masomo ya sayansi wamechukua sayansi tena mmoja alikuwa Chuo cha Sokoine akaondolewa. Nataka Serikali iniambie nikiwapa majina ya hawa wanafunzi wawili ambao wamefaulu vizuri na mmoja alikuwa anaendelea na masomo watampa mkopo na kwa nini walimpa mara ya kwanza halafu wamemkata na hana baba wala mama?

Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu ndiyo inayosomesha wataalam watakaofanya kazi viwandani. Kwa sababu ambayo siijui Waziri aliyepita na bahati mbaya alishafariki aliondoa elimu ya ufundi ambayo ilikuwa na mfumo wa kupata watu wenye Full Technician Certificate (FTC). Kwa mfano, mtu alikuwa anatoka Ifunda Technical, Dar Technical, Moshi Technical au Tanga Technical kwenda Chuo cha Ufundi, miaka minne amechagua kozi ya umeme kwa mfano, anakwenda Technical College miaka mitatu anapata cheti cha FTC, lakini baadaye akirudi miaka mitatu anakuwa na miaka 10 katika field ile, kwa hiyo akienda kufanya kazi ni mtaalam aliyefaulu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi bahati mbaya sana mfumo huo umevurugika wala hakuna anayejali. Matokeo yake ni nini? Hakuna mafundi viwandani, mafundi sanifu wenye FTC hawapo lakini Kanuni za Mainjinia wanasema kila Mhandisi mmoja katika kiwanda anatakiwa asimamie technicians 25 sasa hao technicians hawapo na mainjinia tunatoa wa white colour. Mimi watu wa Engineering wa University wanapochora maboksi (Geometrical and Techninical Drawing) niliifanya form one na form two lakini sasa wanayafanya chuo kikuu wanatoka pale white colour hawana wa kuwasimamia, FTC tumeifuta.

Mheshimiwa Spika, napenda vyuo vya ufundi virudishwe lakini pia chuo cha ufundi kiendeleze kozi ya FTC inayotoa mtaalam wa fundi sanifu. Nashukuru Serikali imenisaidia hela jimboni kwa ajili ya high school ya Ndono na shule ya msingi lakini pia naomba kabisa kabisa mjaribu kurudisha mfumo ule wa Ujerumani wa Technical Engineers na Academic Engineers, hiyo peke yake ndiyo mkombozi wa watumishi viwandani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utawala bora. Nililalamika humu ndani ya Bunge lako kwamba jamani kama Mahakama inaongelea kuweka Mahakama nyingi kila Kata au katika Kila Wilaya kule Upuge kwangu Mahakama imetelekezwa. Mahakama ya mwaka 1954 imefanya kazi mpaka baada ya uhuru na kuendelea lakini sasa imetelekezwa, majengo yake mazuri yako wazi, panya na nyoka wameingia, mwisho wakulima wamevamia wanakaa mle mwenye majengo mazuri.

Mheshimiwa Spika, palepale mbele yake kuna kituo cha afya hakuna Madaktari kwa sababu hakuna nyumba. Nikasema kama kulikuwa na sababu nzuri basi ya kuiacha hiyo Mahakama zile nyumba zitumiwe na Idara nyingine za Serikali na nillikuwa nalenga kituo cha afya.

Mheshimwa Mwenyekiti, kituo cha afya tunajenga vizuri, tumepata shilingi milioni 500 kukiboresha kwa kujenga wodi za wagonjwa lakini sasa Madaktari hakuna, hakuna nyumba na mita 500 kuna majengo ya Mahakama ambayo hayana kazi. Kwa bahati mbaya Mheshimiwa mmoja alijibu humu ndani kwamba Mahakama inafanya kazi jambo ambalo si kweli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushirikishaji wa sekta binafsi. Waziri Mpango amesimama juzi hapa akasema sisi tunajua injini ya uchumi ni sekta binafsi, injini gani haina mafuta? Mnasema ndiyo uti wa mgongo, uti wa mgongo hauna mfupa, hamuisaidii, sisi tumekuwa tunalalamika hapa ndani kwamba sheria zilizopo hazitupi competitiveness na jirani zetu, tukishindana tunashindwa katika ushindani, tender wanapata wenzetu, makampuni ya hapa yaki-bid yanashindwa kwa sababu ndani yake kuna kitu kwa mfano kinaitwa SDL. Sisi hapa Tanzania tunalipa SDL ya 4.5% ndiyo ya highest duniani.

Mheshimiwa Spika, muda wote waajiri tumeomba mtupunguzie highest ya SDL iko Kenya 1.2% lakini kwa ajili ya Idara moja tu ya Utalii kwingine kote hakuna, Uganda, Rwanda na Burundi hakuna, sisi tuki-bid tender za international maana lazima tuweke SDL tunakosa hizo tender competitiveness hakuna Tanzania. Sasa mnasema private sector ndiyo injini, injini gani bila mafuta?

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia Serikali haiko tayari kufanya PPP, nina mfano mzuri sana. Mimi baada ya kwenda Jimboni kwangu nikagundua kwamba watu hawana elimu kubwa sana kuhusu mambo yanayotokea duniani nikaamua kufungua kituo cha redio na kwa sababu Halmashauri ndiyo nailenga itumie kituo hicho nikaipa 30% kama PPP.

Lakini tangu tumeingia ubia huo Halmashauri imeshindwa kupata kibali cha kuwaruhusu tufanye PPP. Kwa sababu lazima tupitie Kamati ya Fedha na Uongozi, Baraza la Wilaya, Baraza la Mkoa, Mkuu wa Mkoa, Waziri wa TAMISEMI, Waziri wa Fedha, Kamishna wa Bajeti ndiyo wapate kibali kwamba ingieni, imeshindikana, mwaka mzima sasa mradi umesimama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na naunga mkono hoja.