Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Sonia Jumaa Magogo

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. SONIA J. MAGOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Awali ya yote, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyeniwezesha kuwa na afya njema mpaka wakati huu na kuweza kusimama mbele yenu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, napenda kukishukuru Chama changu cha Wananchi CUF chini ya uongozi mahiri wa Mwenyekiti wetu, Profesa Ibrahim Haruna Lipumba, akisaidiana na Naibu Katibu Mkuu, Mheshimiwa Magdalena Sakaya. (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nitakuwa sijafanya busara kama sitalishukuru Bunge lote kwa kutupokea vizuri na kutupa ushirikiano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeupitia Mpango wa Mheshimiwa Waziri, kwa kweli Mpango uko vizuri. Pamoja na uzuri wa Mpango huo, nami ninayo machache ambayo natamani yaingie au yatiliwe mkazo katika Mpango ambao upo mbele yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza kabisa ni suala la lishe. Katika Mpango huo sikuona kama suala la lishe limetiliwa umuhimu sana kama lilivyo katika jamii yetu. Kila mtu anafahamu umuhimu wa lishe na hata sisi tusingekuwa hapa kama tusingekuwa na afya njema na kupata lishe iliyo bora. Hivyo, naishauri Serikali iliangalie sana suala la lishe. Iziwezeshe taasisi ambazo zinahusika na suala la lishe ili wananchi wapate elimu na kuelewa umuhimu wa lishe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania tuna utajiri wa vyakula na kama wananchi wangepata elimu ya kutosha, tusingekuwa na watoto wanaozaliwa wakiwa wamedumaa akili. Hivyo, naishauri Serikali itilie mkazo kwenye suala la lishe kwa sababu kuna usemi unasema prevention is better than cure. Kwa hiyo, naishauri Serikali i-stick katika kuepusha maradhi kwa kizazi kilichopo na kijacho kuliko kusubiri tumeshapata matatizo tunanunua dawa kwa pesa ambazo zingesaidia kwenye vitu vingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa viwanda, kitu cha kwanza napenda tujiulize ni kwa nini vile viwanda vilivyokuwepo vilikufa. Je, zile sababu zilizosababisha vile viwanda vikafa leo hazipo tena? Kama zipo tunafanyaje ili kuhakikisha kwamba viwanda hivyo ambavyo vinakwenda kuanzishwa tena havitakufa na vitakuwa endelevu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano suala la malighafi. Naishauri Serikali ijiandae vizuri kwenye suala la malighafi kabla ya kuanzisha viwanda vingi. Tulikuwa na mazao ambayo sasa hivi tunaona yameshuka ama mengine hayapo kabisa, kama mazao ya mkonge, pamba na michikichi. Kwa hiyo, naishauri Serikali, kabla hatujaenda kufungua viwanda vingine zaidi tuangalie uwepo wa malighafi ili viwanda hivyo visije vikaenda na vyenyewe vikafa kama vile ambavyo vilikufa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tuangalie workforce, je, workforce iliyopo inatosha kwa hivyo viwanda ambavyo tunahitaji kuvianzisha? Elimu ikoje kwa wale watu ambao wanakuja kufanya kazi kwenye viwanda hivyo, ujuzi wao ni kiasi gani katika kuendesha viwanda hivyo? Kwa sababu kama tukiwa hatuna workforce ya kutosha hivyo viwanda na vyenyewe vitakwenda kufa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ni mitaji, nauliza Serikali imejipangaje kwa suala la mitaji ya kuendesha viwanda hivyo. Je, tumeiandaa vipi Benki yetu ya TIB katika suala hilo la kuendesha viwanda? Kama tunategemea watu binafsi, je, Serikali imejiandaaje katika kukusanya kodi kuhakikisha kwamba kodi zetu hazipotei na zinapatikana kwa wakati muafaka na kuendeleza Taifa letu kama tulivyopanga? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kugusia suala la elimu, natamani kuona Serikali ikiwa imetilia sana mkazo kwenye suala la elimu hasa elimu ya msingi. Watoto wanajazana kwenye madarasa na pale hatutegemei ma- engineer, ma-doctor wala Wabunge na Mawaziri ambao watakuwa na akili tulivu kama tulivyo sisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wengi wetu tumesoma kwenye shule za kulipia lakini population kubwa iko kwenye shule zile ambazo tunaita za kata, lakini ukiangalia wale watoto mazingira wanayosomea ni magumu sana, hata wale Walimu wanaowafundisha hawapati ile motisha ya kutosha kuweza kuwahudumia wale watoto. Hivyo, naishauri Serikali iangalie kwa sababu msingi wa elimu unaanzia chini, hata sisi tusingekuwa na msingi mzuri mimi na wewe leo tusingekuwa hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tuangalie elimu zinazotolewa kwenye vyuo vyetu. Wasomi wengi wanatoka vyuoni lakini wanakuwa kama wame-cram, ukimpeleka kwenye kufanya kazi ile aliyoisomea, hawezi. Kwa hiyo, tuangalie ile quality ya elimu inayotolewa katika vyuo vyetu na inatolewa kwa namna gani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tutoe elimu ya ujasiriamali hasa kwa vijana. Vijana wengi wanamaliza vyuo wakiwa na mentality ya kwamba nakwenda kuajiriwa Serikalini. Tunaweza kuwajengea uwezo kuanzia chini ya kwamba sio lazima kila mtu aajiriwe, unaweza kujiajiri na ukawa na maendeleo zaidi hata ya yule mtu aliyeajiriwa. Hivyo, naiomba Serikali iangalie sana juu ya elimu ya ujasiriamali kwa vijana na vilevile kuwawezesha mitaji pale wanapopata hiyo elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kila aliyesimama hapa aligusia suala la maji. Mimi pia naomba nichangie kuhusu maji. Maji imekuwa ni tatizo kubwa katika nchi yetu, kuendesha viwanda kunahitaji maji, shughuli zote maofisini zinahitaji maji, hospitali zinahitaji maji na shule zinahitaji maji. Hivyo, tunaomba sana Mpango huu utilie mkazo suala la maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi vijijini wanateseka sana na suala la maji. Kama mwananchi ananunua ndoo moja ya maji kwa Sh.1,000/= kijijini, je, ana uwezo kweli wa kuhimili maisha yake? Kwa sababu tunajua kipato cha wananchi wa chini, wale wa vijijini, lakini kama anatakiwa
kununua ndoo moja ya maji ya Sh.1,000/= kwa siku maisha yake yanakuaje? Naomba sana na hilo litiliwe mkazo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba na mimi kukazia kwenye bomba la mafuta linalopita Tanga. Huu ni mradi mkubwa sana unaopita mkoani kwetu. Naiomba Serikali iwasaidie wananchi wa Tanga kupitia mradi huu waweze kunufaika zaidi kwa kuwapa elimu na vitendea kazi na kuwapa kipaumbele hata katika zile ajira ambazo zinatokea ili kuinua uchumi wa Mkoa wa Tanga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hayo machache, ahsante sana.