Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Vedastus Mathayo Manyinyi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Musoma Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. VEDASTUS M. MANYINYI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuweza kunipa nafasi na mimi niweze kuwa mchangiaji siku hii ya leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu kutujalia kuwepo katika hii siku njema ya leo, lakini nampongeza sana Mheshimiwa Rais Magufuli kwa kazi yake nzuri anayoifanya. Ni ukweli usiopingika, wote tunayafahamu na hata yale ambayo yalikuwa ni mambo magumu ambayo tulikuwa tunadhani kwamba hayawezekani ameweza kuyatekeleza katika kipindi kifupi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia mfano suala la kuhamia Dodoma ilikuwa ni hadithi ya toka miaka ya 70 lakini ndani ya kipindi cha mwaka mmoja na huu wa pili tayari wote tumekubali na Serikali nzima imehamia Dodoma.

Vilevile kuna suala la nidhamu ya uwajibikaji, nadhani hilo ni suala ambalo halipingiki kila mmoja anakubali kwamba sasa ile nidhamu imekuwepo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ni sisi hawa hawa tulikuwa tunapenda kusema kwamba katika nchi hii wapo wale vigogo hawashughulikiwi wanapokosa lakini leo imedhihirika kwamba nchi hii ni ya kila Mtanzania, uwe mkubwa ama mdogo ukikosea sheria inafuata mkondo wake. Kwa hiyo, hiyo yote ni kazi kubwa ambayo Mheshimiwa Rais ameifanya na jukumu letu sisi ni kuendelea kumwombea uzima katika hii kazi nzuri anayoendelea nayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mheshimiwa Dkt. Mpango kwa maana ya uwasilishaji wake wa Mpango huu ambao ni wa 2018/2019. Nadhani ukiangalia katika ukurasa wa tano ameweza kusema vizuri kwamba yeye kama Waziri ameweza kutuletea sisi kama Wabunge tuweze kushauri lakini vilevile tuweze kutoa maoni kwa namna bora zaidi ya utekelezaji wa Mpango huu. Kwa hiyo, kumbe sasa ameanza na yale aliyoyaona kwamba yanastahili halafu ametupatia na sisi tuweze kuchangia kwa maana ya kujaziliza. Nikiangalia kuna ile Kamati ya Bajeti imeweza kusema mambo mazuri sana na katika hayo basi kazi yetu ni kuendelea kujaziliza pale penye ushauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu wa kwanza, pamoja na kazi kubwa na nzuri ambayo Serikali ya Awamu ya Tano imefanya lakini tuna tatizo moja kubwa kwamba Watanzania hali ya uchumi wetu imeendelea kudorora. Huo ni ukweli usiopingika karibu kila mmoja wetu ukimgusa iwe mkulima wa kawaida hali ya uchumi imekuwa mbaya, lakini hata wafanyabishara, biashara nyingi zimesimama na zimefungwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia nini kinachangia haya yote, pamoja na vile viashiria vizuri vinavyoonesha kwamba uchumi wa nchi unakua lakini unapokuja kwenye uchumi wa mtu mmoja mmoja bado hali inaelekea kuwa mbaya. Hii moja, leo Serikali imezuia uuzaji wa mazao ya
chakula hasa mahindi na mchele. Kwa wale wenzetu ambao bahati nzuri wamebahatika kulima na wakavuna, Serikali imeweka mpango mzuri wa kuzuia kile chakula kisiende nje ili kije kitusaidie Watanzania, kumbe Serikali ilikuwa na kila aina ya sababu ya kununua kile chakula iweke kwenye maghala ya Taifa halafu iendelee kusambaza katika yale maeneo ambayo yana upungufu wa chakula.

Mheshimiwa Spika, kilichofanyika tumemzuia asiuze lakini vilevile hatuko tayari kununua, kwa kweli hali hii tafsiri yake ni kwamba imeendelea kumpa yule mwananchi wa kawaida hali ngumu ya maisha. Kwa hiyo, hilo ni kati ya suala ambalo Serikali inahitaji iliangalie na ione ni kwa kiasi gani inaweza ikawasaidia hawa wananchi wa kawaida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tumeambiwa na wote tumeendelea kufahamu kwamba mazao kama mbaazi hayana soko, lakini wale wakulima walishalima na wanayo kwenye maghala. Zao kama tumbaku halina soko, wakulima walishalima na tayari yapo kwenye maghala. Tafsiri yake ni kwamba lazima hali ya uchumi, ya kipato iendelee kuwa duni na maisha yao yaendelee kuwa magumu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, katika huu Mpango wa leo ambao umeletwa mbele yetu nami nina ushauri ufuatao. Ukiangalia katika nchi yetu zaidi ya asilimia 70 ya Watanzania ni wakulima lakini pamoja na hayo huu Mpango haujasema unafanya nini katika kipindi kifupi na kirefu kuwasaidia wakulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ushauri wangu leo wa nini kifanyike ni lazima tuwe na mpango na muda mfupi, wa kati na muda mrefu. Katika mpango wa muda mfupi leo ungeniuliza na kama Dkt. Mpango atakubaliana na ushauri huu ili ikiwezekana ndani ya mwaka kesho na mwaka keshokutwa tuanze kuona matokeo tena matokeo makubwa, hebu tutambue mabonde mazuri yanayostahili kilimo katika kila Mkoa.

Mheshimiwa Spika, mfano sisi pale Mara tunalo shamba lisilopungua ekari 20,000 linaitwa shamba la Bugwemu. Maeneo kama hayo yote tukiyatambua, kazi ya Serikali ni kuhakikisha kwamba kwenye hayo maeneo yote inapeleka maji, bahati nzuri tunayo REA. Kwa hiyo, tukiweka mkakati wa muda mfupi kwamba yale mabonde yote yatambulike na maji yaweze kwenda pale itasaidia sana na hiyo ni hatua ya kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua ya pili, ukiangalia vijana wengi leo wanaomba kwenda kujiunga kwenda JKT wakitegemea wakitoka hapo kwanza watapata mafunzo lakini kuna uwezekano mkubwa wa kuja kupata kazi. Sasa hebu tusiwafundishe zaidi kushika bunduki kule JKT, tuwafundishe zaidi kulima na kazi za mikono. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachokijua ndani ya kipindi kifupi, wale JKT tukiwawezesha vijana wengi wakaweza kwenda kule wakajifunza kilimo na kile kitakachopatikana na hicho kilimo kikaja kuwa mtaji wao kwa maisha ya baadaye watakapotoka pale waende kuanza maisha. Mimi naamini tatizo kubwa la chakula litakuwa limekwisha lakini hata hili ambalo linatuzuia kupeleka chakula katika nchi jirani kumbe tutakuwa tumezalisha chakula sasa ambacho kina soko kila mahali.

Mheshimiwa Spika, leo ukizungumza suala la mchele, katika nchi zote zinazotuzunguka mchele wa Tanzania una soko kubwa sana, lakini mchele wenyewe ndiyo huo wakitaka kupeleka hawaruhusiwi kwa sababu hautoshelezi. Kwa hiyo, tunadhani kwamba katika mpango wa muda mfupi, hiyo ni namna pekee inayoweza kutuwezesha au kuwawezesha watu wetu wakaweza kupata kipato ambacho kinaweza kikawasaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hebu tuone namna ya kuendelea kuisaidia SIDO, kuendelea kuiongezea uwezo ili itoe mafunzo kwa watu wengi zaidi. Mnajua kwa bahati mbaya sana yawezekana hili wengi hatulifahamu, bidhaa nyingi kinachotakiwa ni ile packaging. Labda nitoe mfano
mdogo, ukienda pale sokoni utakuta kuna ile asali ya Pinda, kwa jinsi ilivyokuwa packed ile robo kilo bei yake ni zaidi ya kilo nzima ya asali inayotoka Tabora. Kumbe kilichofanyika pale ni packaging na utaalam huo SIDO wanao, kwa hiyo wanaweza kuwafundisha watu wengi zaidi na wakawafanya watu wengi zaidi wakapata ujuzi na wakawa wanafanya packaging ya bidhaa mbalimbali tulizonazo na wakawa wanajipatia kipato kizuri na hata katika masoko ya export. Kwa hiyo, tunadhani kwamba SIDO yetu tukiendelea kuisaidia basi nayo itatusaidia zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mpango wa muda wa kati, kati ya eneo ambalo nadhani tunahitaji kulifanyia kazi ni pamoja na elimu yetu. Leo tumesikia hapa juhudi kubwa tuliyonayo ni kuhakikisha kwamba mikopo inapatikana, vijana wetu wanamaliza vyuo vikuu lakini tumesahau kwamba tuna tatizo kubwa leo la kuwapatia hao vijana ajira. Maana masomo mengi wanayoyasoma baada ya pale uwezo wa kuwaajiri hatuna. Kwa bahati mbaya vijana wengi wa Kitanzania huko nje wanashindwa kupata ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda duniani kote, kila ukikutana na watu weusi watatu wanafanya kazi mahali popote pale duniani, wawili lazima utamkuta ni Mkenya, sanasana utamkuta ni Mganda lakini kwa Watanzania ni wachache sana. Hiyo tafsiri yake ni nini? Ni kwamba inaonekana kumbe ile elimu tunayoitoa haiwapi nafasi kubwa ya ushindani wa ajira katika masoko ya nje. Kwa hiyo, leo watoto tunawasomesha, wanamaliza chuo halafu wanarudi hapa sasa hakuna ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nini kifanyike? Hebu tuangalie namna ya kuboresha vyuo hivi vya kati. Wale wanaomaliza kidato cha nne, wanaomaliza kidato cha sita, tuongeze hivi vyuo vya VETA na vyuo vya ufundi ili wanafunzi wengi zaidi wapate ujuzi. Tunadhani kwa kufanya hivyo itawafanya sasa hao vijana wajiajiri wao wenyewe. Kwa utaratibu tulionao wanafunzi wengi wanasoma sociology na political science, maana yake ni kwamba wakimaliza tunaendelea kukaa nao mitaani. Kwa bahati mbaya sana unakuta kuna baadhi ya wanafunzi wamemaliza chuo kikuu lakini anazidiwa na aliyemaliza kidato cha nne akaenda VETA kwa sababu yeye tayari anao ujuzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunang’ang’ana na tunajitahidi kusomesha lakini naamini kwamba baada ya muda tutafika mahali tunatengeneza bomu kubwa na tunayo mifano ya nchi. Ukienda kwenye nchi kama Nigeria, ni kati ya nchi ambazo zina wasomi wengi lakini walioajiriwa huko duniani ni wachache. Sasa inaonekana huo ndiyo mfumo wa elimu tulionao. Kwa hiyo, nina imani kwamba kama hatukuuangalia vizuri basi itatusumbua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo lingine ambalo tunahitaji kulifanya, ukiangalia kwetu sisi Tanzania ni kati ya nchi ambayo ina madini kushinda nchi nyingi, inashinda Kenya, Uganda, Rwanda, karibu nchi zote zinazotuzunguka. Cha ajabu unakuta katika nchi kama Kenya wana-export zaidi madini kutushinda sisi na hizo nchi nyingine zote hizo za Rwanda, lakini haya tunaendelea kuyasema mwisho wa yote yanabaki kama yalivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hatuna udhibiti kamili…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi, naunga mkono Mpango.